DKT. MADELE AFUNGUA MAFUNZO YA MFUMO WA JINSIA GALS KUCHOCHEA UZALISHAJI WA MAZIWA
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Sekta ya Mifugo, 𝐃𝐤𝐭. 𝐅𝐚𝐛𝐢𝐚𝐧 𝐌. 𝐌𝐚𝐝𝐞𝐥𝐞,leo Septemba Mosi, 2026 amefungua rasmi mafunzo ya siku sita ya kuwajengea uwezo Wakufunzi kuhusu 𝐌𝐟𝐮𝐦𝐨 𝐰𝐚 𝐉𝐢𝐧𝐬𝐢𝐚 𝐤𝐰𝐚 𝐕𝐢𝐭𝐞𝐧𝐝𝐨 (𝐆𝐀𝐋𝐒), yanayoratibiwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia Mradi wa Mageuzi ya Tasnia ya Maziwa na Mabadiliko ya Tabianchi (C-SDTP).
Mafunzo hayo yanayofanyika katika Hoteli ya Edema jijini Dodoma yamelenga kuwaandaa washiriki ambao ni Maafisa Maendeleo ya Jamii kutoka katika Halmashauri mbalimbali nchini kuwa Wakufunzi na Mawakala wa Mabadiliko watakaofikisha maarifa ya GALS hadi ngazi ya jamii, kwa lengo la kuimarisha ushirikiano na ushirikishwaji wa wanawake na wanaume katika kupanga, kuweka malengo ya kaya na biashara, kufanya maamuzi na kusimamia rasilimali kwa pamoja.
Dkt. Madele amewataka washiriki kuhakikisha elimu hiyo inaleta mabadiliko ya kimtazamo, usawa na maamuzi ya pamoja katika kaya, ili ongezeko la uzalishaji wa maziwa utakaochangia kipato, lishe bora na maisha bora kwa familia za wafugaji.
Kupitia mfumo wa GALS, Mradi wa C-SDTP unalenga kuzijengea kaya ushirikiano na maendeleo jumuishi na endelevu.






Maoni
Chapisha Maoni