DKT. BASHIRU AZINDUA BODI YA TAFIRI, ATAKA TAFITI ZA UVUVI ZENYE SULUHISHO
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Balozi Dkt. Bashiru Ally, ameitaka Bodi Mpya ya Wakurugenzi ya Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) kuhakikisha tafiti zinazofanywa na Taasisi hiyo zilenge kutatua changamoto halisi zinazoikabili Sekta ya Uvuvi, hususani katika ukuzaji wa viumbe maji na kusisitiza kipaumbele kinapaswa kuwa tafiti za uzalishaji wa mbegu bora na chakula bora cha samaki ili kuongeza uzalishaji.
Akizungumza leo Septemba 05, 2026 katika Hoteli ya Gerwill Jijini Dodoma wakati wa kuzindua Bodi hiyo, Balozi Dkt. Bashiru ameitaka TAFIRI kuanzisha na kusimamia kwa uthabiti programu ya kuboresha mbari za samaki (breeding program), pamoja na kufanya tafiti na uhaulishaji wa teknolojia zinazotumika katika ufugaji wa samaki kwa vizimba katika maji baridi na baharini.
“Bodi hii iisimamie TAFIRI kufanya tafiti zenye suluhisho katika Sekta ya Uvuvi, kusimamia sheria na utawala bora, ili Taasisi iweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi na kutoa mchango mkubwa katika maendeleo ya sekta ya uvuvi na ukuzaji viumbe maji,” amesema Dkt. Bashiru.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bi. Agnes Kisaka Meena, amemshukuru Balozi Dkt. Bashiru kwa usimamizi wake tangu apewe dhamana hiyo na kueleza kuwa ana imani kubwa na wajumbe wa Bodi ya TAFIRI aliyowateua na kwamba kutokana na weledi na uzoefu wao watasaidia kuisimamia Taasisi hiyo kutekeleza majukumu yake.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI), Dkt. Ismael Kimirei, amesema TAFIRI ilianzishwa mwaka 1980 na kwa sasa ina jumla ya vituo vitano na watumishi 211 na kuahidi kuwa Taasisi hiyo itaendelea kushirikiana na Bodi katika kuhakikisha majukumu ya Taasisi yanatekelezwa kwa kuzingatia sheria, taratibu na miongozo ya Serikali.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya TAFIRI, Alhaj Yahya Ibrahim Mgawe, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kumteua kuwa mwenyekiti wa Bodi hiyo na kuahidi kuwa mwenyekiti wa bodi hiyo na kuahidi kutekeleza maelekezo na maagizo ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi ya kuhakikisha bodi hiyo inaisimamia TAFIRI kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia sheria, taratibu na misingi ya utawala bora.
Bodi ya TAFIRI ina jumla ya wajumbe saba na itaiongoza Taasisi hiyo kwa kipindi cha miaka mitatu.






Maoni
Chapisha Maoni