DKT. BASHIRU AITAKA LITA KUENDANA NA MABADILIKO YA SEKTA YA MIFUGO
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi. Dkt. Bashiru Ally Kakurwa ameitaka Wakala ya Mafunzo ya Mifugo Tanzania (LITA) kuendelea kuboresha mafunzo na kutoa wataalamu wenye uwezo wa kukabiliana na mahitaji na mabadiliko yanayoendelea katika sekta ya mifugo nchini.
Waziri Dkt. Bashiru ameyasema hayo leo Septemba 14, 2026 alipotembelea Kampasi ya LITA Temeke, Dar es Salaam, ambapo amesisitiza umuhimu wa taasisi hiyo kutoa mchango mkubwa katika maendeleo ya sekta ya mifugo, hususan kupitia mafunzo, tafiti, mawazo na ushauri wa kitaalamu, akiitaka LITA kutoa mawazo na mapendekezo yatakayosaidia katika maboresho ya sera za mifugo ili ziendane na utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2050.
Amesema sekta ya mifugo kwa sasa ina umuhimu wa kipekee kutokana na kuongezeka kwa idadi ya watu, kukua kwa mahitaji ya protini, kufunguka kwa masoko pamoja na mabadiliko ya ufugaji kuelekea mifumo ya kisasa, hivyo LITA inapaswa kuendana na mabadiliko hayo kwa kutoa huduma na mafunzo yenye ubora.
Waziri pia ameitaka LITA kuimarisha mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi pamoja na kuboresha nyenzo za kufundishia, akielekeza taasisi hiyo kuandaa bajeti na kuainisha mahitaji muhimu ya vifaa vya mafunzo ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa.
Kwa upande wake, Meneja wa Kampasi ya LITA Temeke, Bi. Bernadetha Kessy, amemshukuru Waziri kwa maelekezo aliyoyatoa na kusema kuwa taasisi hiyo imeyapokea na itayafanyia kazi. Amesema mwenendo wa udahili unaonesha kuongezeka kwa idadi ya wanafunzi wanaojiunga na taaluma mbalimbali za sekta ya mifugo, jambo linaloonesha umuhimu wa kuendelea kuimarisha uwezo wa LITA katika kutoa mafunzo yanayokidhi mahitaji ya sekta.






Maoni
Chapisha Maoni