WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI AHIMIZA MATUMIZI BORA YA ARDHI KUMALIZA MIGOGORO YA WAKULIMA NA WAFUGAJI RUFIJI
Na. Daudi Nyingo
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa, amesema Serikali imejipanga kupata suluhisho la kudumu la migogoro kati ya wakulima na wafugaji kwa kuimarisha mipango ya matumizi bora ya ardhi na kuhamasisha ufugaji wa kisasa, ili sekta hizo ziendelee kuchangia usalama wa chakula na ukuaji wa uchumi wa Taifa.
Mhe. Dkt. Kakurwa alitoa kauli hiyo Julai 20, 2026 wakati wa ziara yake ya kikazi katika Wilaya ya Rufiji mkoani Pwani, ambapo alitembelea wafugaji na wakulima wa Kijiji cha Chumbi, kukagua maendeleo ya mpango wa Ranchi Ndogo, Vitalu vya Kilimo vya Kijiji cha Nyamwage na baadaye kufanya mkutano wa hadhara katika Tarafa ya Ikwiriri kwa lengo la kusikiliza na kutatua changamoto zinazowakabili.
“Wakulima na wafugaji ni nguzo muhimu za maendeleo ya Taifa kwani ndiyo wanaohakikisha upatikanaji wa chakula na malighafi za mifugo, hivyo migogoro baina yao inapaswa kutatuliwa kwa njia ya mazungumzo na usimamizi mzuri wa ardhi.”
"Bila wakulima na wafugaji, Taifa haliwezi kuwa na usalama wa chakula. Kadri idadi ya watu, wakulima na wafugaji inavyoongezeka, ndivyo mahitaji ya ardhi yanavyoongezeka, wakati ukubwa wa ardhi hauongezeki. Suluhisho ni kupanga matumizi ya ardhi na kuhakikisha kila mmoja anaheshimu maeneo yaliyotengwa kwa shughuli zake," alisema Mhe. Balozi Dkt. Kakurwa.
Alieleza kuwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais – TAMISEMI pamoja na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi itapeleka timu ya wataalamu kupitia mipango ya matumizi ya ardhi katika maeneo yenye changamoto ili kurekebisha kasoro zilizopo na kupanga maeneo ambayo hayajapangwa vizuri.
Aidha, aliwataka wafugaji kuachana na utegemezi wa malisho ya asili pekee kwa kuanza kuzalisha malisho yao wenyewe, kuyavuna na kuyahifadhi wakati wa masika ili yaweze kutumika kipindi cha kiangazi.
"Mfugaji wa kisasa anatakiwa azalishe malisho yake kama mkulima anavyozalisha chakula chake. Serikali ipo tayari kuwasaidia wafugaji kufanikisha jambo hili ili kuongeza tija katika uzalishaji wa mifugo," alisisitiza.
Awali, Mkuu wa Wilaya ya Rufiji, Mhe. Luteni Kanali Frederick Komba, alisema tangu mwaka 2023 wilaya hiyo imeanzisha vitalu 371 vya Ranchi Ndogo, ambapo vitalu 334 tayari vimegawiwa wafugaji na baadhi yao wameanza kuvitumia.
Alisema pamoja na mafanikio hayo bado zipo changamoto zinazotokana na baadhi ya wafugaji kuchelewa kukubali kuacha mfumo wa ufugaji wa kuhamahama na kuhamia mfumo wa ufugaji wa kukaa eneo moja, lakini elimu inayoendelea kutolewa imeongeza mwitikio wa wafugaji wengi kujiunga na mpango huo.
Mhe. Komba alisema Serikali ya Wilaya itaendelea kutoa elimu kuhusu faida za Ranchi Ndogo pamoja na kufuatilia viashiria vyote vinavyoweza kusababisha migogoro kati ya wakulima na wafugaji ili kudumisha amani, usalama na maendeleo ya wananchi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Rufiji, Ndugu Rajabu Mbonde, alimpongeza Waziri kwa kufika wilayani humo na kusikiliza changamoto za wananchi, akisema viongozi wa chama na Serikali wamejizatiti kuhakikisha wakulima na wafugaji wanaendelea kuishi kwa amani.
Alisisitiza kuwa pamoja na umuhimu wa uzalishaji wa nyama na maziwa, uzalishaji wa mazao ya chakula unapaswa kulindwa kwa kuhakikisha kila mmoja anazingatia matumizi sahihi ya ardhi.
"Tunahitaji nyama, tunahitaji maziwa, lakini tunahitaji chakula zaidi. Hatuwezi kukubali kuona mkulima na mfugaji wanaingia kwenye migogoro. Tunataka ng'ombe wabaki kwenye maeneo ya ranchi na wakulima wafanye kilimo katika maeneo yaliyotengwa kwa shughuli hiyo," alisema Ndugu Mbonde.
Ziara ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuimarisha usimamizi wa matumizi ya ardhi, kuhamasisha ufugaji wa kisasa kupitia mfumo wa Ranchi Ndogo na kutafuta suluhisho la kudumu la migogoro kati ya wakulima na wafugaji ili sekta zote mbili ziendelee kuchangia maendeleo ya uchumi na usalama wa chakula nchini.





Maoni
Chapisha Maoni