SERIKALI YAHIMIZA MATUMIZI BORA YA MIKOPO KWA WANUFAIKA WA PROGRAMU YA UWEZESHAJI VIJANA KIUCHUMI

Jumla ya vijana 69 kutoka Mkoa wa Lindi katika wilaya za Kilwa, Mtama na Ruangwa wanaonufaika na Programu ya Uwezeshaji wa Vijana Kiuchumi katika Sekta ya Mifugo na Uvuvi wamepatiwa mafunzo ya kuwajengea uwezo wa kusimamia miradi yao kibiashara na kuhakikisha mikopo waliyopewa inatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.

Mafunzo hayo yamefanyika Julai 30, 2026, katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Lindi, yakiratibiwa na wataalamu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana, pamoja na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB). Kupitia mafunzo hayo, wanufaika wamepatiwa maarifa kuhusu kanuni bora za ufugaji wa kuku, kondoo, nguruwe na mbuzi, sambamba na elimu ya ujasiriamali, usimamizi wa biashara, stadi za maisha na mbinu za kuongeza tija na mafanikio katika miradi yao.

Akifungua mafunzo hayo, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa Ndg. Mwinjuma Mkungu amewataka wanufaika kutumia fursa hiyo kwa ufanisi ili kujijengea msingi imara wa kiuchumi. Amesisitiza umuhimu wa vijana kushiriki moja kwa moja katika utekelezaji wa miradi yao kwa kufanya baadhi ya shughuli kwa nguvu zao wenyewe, ikiwemo ujenzi wa mabanda na utunzaji wa mifugo, hatua itakayosaidia kupunguza gharama za uendeshaji na kuongeza faida.

Aidha, amewahimiza kutafuta masoko ya uhakika kwa bidhaa zao mapema, kutumia mikopo kwa nidhamu na kwa malengo yaliyokusudiwa, kuweka kumbukumbu sahihi za mapato na matumizi, pamoja na kuanzisha miradi mingine inayoweza kwenda sambamba na ile waliyochagua ili kupanua vyanzo vya mapato na kuongeza ustahimilivu wa kiuchumi.










Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

WATAALAMU WATAKIWA KUKUSANYA TAKWIMU SAHIHI ZA KITAFITI

UTEKELEZAJI WA UFUGAJI SAMAKI KWA VIZIMBA WAANZA ZIWA TANGANYIKA

TANZANIA DAIRY BOARD