PROF. SHEIKH AONGOZA KIKAO CHA UZINDUZI WA UTAFITI WA KUANDAA MRADI WA UCHUMI WA BULUU

Naibu Katibu Mkuu, Prof. Mohamed Sheikh, leo Julai 28, 2026, ameongoza kikao cha uzinduzi wa utafiti wa awali utakaoweka msingi wa kuandaliwa kwa andiko la Mradi wa Uchumi wa Buluu unaojulikana kama "Leading an Ecological and Inclusive Ocean-Based Economic Growth in the United Republic of Tanzania".

Lengo la kikao hicho lilikuwa kujadili utekelezaji wa utafiti huo, kubainisha majukumu ya wadau mbalimbali na kukusanya maoni na mapendekezo yatakayosaidia kufanikisha uandaaji wa andiko la mradi.

Akizungumza wakati wa kikao hicho, Prof. Sheikh alisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa taasisi zote zinazoshiriki katika kuhakikisha utafiti huo unafanyika kwa ufanisi na unazalisha matokeo yatakayochangia maendeleo ya uchumi wa buluu nchini kwa kuzingatia matumizi endelevu ya rasilimali za bahari na mazingira yake.

Kikao hicho kilihudhuriwa na wawakilishi kutoka Shirika la Maendeleo la Ufaransa (Agence Française de Développement – AFD), wataalamu washauri kutoka BRLi, pamoja na wawakilishi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Wizara ya Maliasili na Utalii, Ofisi ya Makamu wa Rais, na Ujumbe wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania (EU Delegation).

Mradi huo unatarajiwa kufadhiliwa kwa ushirikiano kati ya Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD) na Umoja wa Ulaya (EU), ukiwa na lengo la kuimarisha ukuaji wa uchumi wa buluu unaozingatia uhifadhi wa mazingira, matumizi endelevu ya rasilimali za bahari na fursa shirikishi za maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi wa Tanzania.




Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

WATAALAMU WATAKIWA KUKUSANYA TAKWIMU SAHIHI ZA KITAFITI

TANZANIA DAIRY BOARD

LESENI, VIBALI VYA MAZAO YA MIFUGO NA VYAKULA VYA SAMAKI KUTOLEWA KWA NJIA YA KIELEKTRONIKI