DKT. BASHIRU APIGA MARUFUKU UUZAJI HOLELA WA NYAMA, MACHINJIO BUBU

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa ameiagiza Bodi ya Nyama Tanzania (TMB) kuzifunga mara moja bucha zinazouza kiholela nyama na mazao yake bila kuzingatia sheria na kueleza kwamba hali hiyo inaweza kuathiri afya ya walaji.

Mhe. Balozi Dkt. Bashiru  amesema hayo leo Julai 27, 2026 baada kuelezwa kuwepo kwa changamoto hiyo kutoka kwa wachinjaji wa mifugo katika machijio ya Vingunguti yaliyopo Halmashauri ya Jijini Dar es Salaam.

Amesema kumekuwa na uholela wa uchinjaji wa mifugo hususan mbuzi na Kondoo hali inayorudisha nyuma jitihada za serikali ambayo imewekeza Shilingi Bilioni 19.5 kwa ajili ya machinjio ya kisasa.

Aidha, amewaagiza viongozi wa Halmashauri hiyo kukamilisha haraka mchakato wa kupata wawekezaji kwa ajili ya kuendesha machinjio hayo kwa kukidhi taritibu na vigenzo vinavyokubaliwa na serikali kuhusu uendeshaji vinginevyo machinjio hayo itafungwa.

Bodi ya Nyama Kamateni wote wanaouza nyama kiholela ni hatari kiafya kuuza nyama na mazao yake kiholela" amesema Dkt. Bashiru.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dar ea Salaam, Mhe. Albert Chalamila amesema uendeshaji wa machinjio hayo unapaswa kuwa shirikishi kuanzia wizara za kisekta na kutafuta njia nzuri ya kuendesha machinjio ili kuleta tija iliyokusudiwa na serikali.

Awali, akisoma taarifa kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Jiji la Dar es Salaam, Meneja wa Machinjio ya Vingunguti Dkt. James Kawamala alisema kufikia mwaka 2025/2026 mapato yaliyokusanywa kutokana na machinjio hiyo ni shilingi bilioni 2.075 sawa asilimia 90.02 ya lengo la kukusanya shilingi bilioni 2.3 kutokana na uchinjaji wa mifugo ambapo ng'ombe 500, mbuzi na kondoo 1,000 huchinjwa kwa siku.

Mwonekano wa Nyama ya ng'ombe inayopatikana katika bucha za Vingunguti baada ya kuchakatwa kutoka machinjioni.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa (wapili kulia) akisikiliza maoni kutoka kwa wafanyabiashara wa nyama wa Vingunguti Jijini Dar es Salaam wakati wa ziara yake leo Julai 27, 2026. Viongozi wengine alioambatana nao ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Albert Chalamila na Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe. Edward Mpogolo.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa (wa pili kushoto) akitoa maelekezo wa wataalam na watendaji wa machinjio ya Vingunguti alipotembelea na kukagua shughuli zinazofanyika kwenye machinjio hayo leo Julai 27, 2026.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa akiwa ameongozana na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila kufanya ukaguzi wa machinjio ya Vingunguti jijini Dar es Salaam leo Julai 27, 2026

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa akizungumza na viongozi na wataalam wa machinjio ya Vingunguti wakati wa ziara yake leo Julai 27, 2026.

Baadhi ya Wananchi na wachakataji wa mazao ya mifugo kutoka katika Machinjio ya Vingunguti wakisikiliza  kikao cha Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa leo Julai 27, 2026

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

WATAALAMU WATAKIWA KUKUSANYA TAKWIMU SAHIHI ZA KITAFITI

UTEKELEZAJI WA UFUGAJI SAMAKI KWA VIZIMBA WAANZA ZIWA TANGANYIKA

TANZANIA DAIRY BOARD