DKT. BASHIRU AKUTANA NA GATSBY AFRICA KUJADILI MKAKATI WA UZALISHAJI WA CHAKULA CHA SAMAKI NA KUKU

Serikali imeendelea kuimarisha ushirikiano na wadau wa maendeleo katika kuongeza tija ya sekta za mifugo na uvuvi, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kukuza uzalishaji, kuimarisha usalama wa chakula na kuongeza mchango wa sekta hizo katika uchumi wa Taifa.

Katika hatua hiyo, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa, leo Julai 24, 2026 amekutana na timu ya wataalam kutoka Taasisi ya Gatsby Africa katika Ofisi za Wizara ya Mifugo na Uvuvi zilizopo Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma, na kujadiliana kuhusu uwekezaji katika ukuzaji wa viumbemaji na kuongeza upatikanaji wa chakula cha samaki na kuku.

Mazungumzo hayo yalijikita katika namna Serikali na Gatsby Africa zinavyoweza kushirikiana kuendeleza sekta za mifugo na uvuvi kupitia uwekezaji katika uzalishaji wa malighafi za chakula cha mifugo, matumizi ya teknolojia za kisasa na kuimarisha mnyororo wa thamani wa uzalishaji.

Akizungumza katika kikao hicho, Dkt. Bashiru alisema Serikali inaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wadau wa maendeleo na sekta binafsi kuwekeza katika miradi yenye tija itakayoongeza uzalishaji, ajira na kipato cha wafugaji pamoja na wafugaji wa samaki.

Alisema upatikanaji wa chakula bora na cha gharama nafuu kwa samaki na kuku ni msingi muhimu wa kuongeza tija katika uzalishaji, hivyo ushirikiano na taasisi mbalimbali una mchango mkubwa katika kufanikisha malengo ya Serikali ya kuendeleza sekta hizo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa programu hizo kutoka Taasisi ya Gatsby Africa, Bw. Yisambi Mwanshemele alielezea kuwa mradi unaopendekezwa unalenga kuimarisha uzalishaji wa chakula cha samaki na kuku kwa kutumia zao la Soya kwa kupitia uwekezaji katika uzalishaji wa malighafi, matumizi ya teknolojia bunifu, kujenga uwezo wa wazalishaji na kuvutia ushiriki mkubwa wa sekta binafsi.

Aidha, alibainisha kuwa utekelezaji wa mradi huo unatarajiwa kuongeza upatikanaji wa chakula bora cha samaki na kuku, kupunguza gharama za uzalishaji, kuongeza ushindani wa bidhaa za mifugo na uvuvi katika soko, pamoja na kuchochea ukuaji wa uchumi na ajira, ambapo Taasisi hiyo imejipanga kuwafikia wafugaji 300,000.

Pande hizo mbili zilikubaliana kuandaa Mpango Mkakati mzuri wa Uzalishaji wa Vyakula hivyo, na kuendelea na mazungumzo ya kitaalamu yatakayoweka msingi wa utekelezaji wa maeneo ya ushirikiano kwa lengo la kuimarisha maendeleo ya sekta za mifugo na uvuvi nchini.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa (wa kwanza kushoto), akimsikiliza Mtaalam kutoka Taasisi ya Gatsby Africa (hayupo pichani), katika kikao kifupi cha kujadili kuhusu uwekezaji katika ukuzaji wa viumbemaji na kuongeza upatikanaji wa chakula cha samaki na kuku, kikao kilichofanyika katika Ofisi za Wizara ya Mifugo na Uvuvi zilizopo Mji wa Serikali - Mtumba, Julai 24, 2026 Dodoma.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa (wa kwanza kushoto), akizungumza na Wataalam wa Taasisi ya Gatsby Africa, katika kikao kifupi cha kujadili kuhusu uwekezaji katika ukuzaji wa viumbemaji na kuongeza upatikanaji wa chakula cha samaki na kuku, kikao kilichofanyika katika Ofisi za Wizara ya Mifugo na Uvuvi zilizopo Mji wa Serikali - Mtumba, Julai 24, 2026 Dodoma.

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

WATAALAMU WATAKIWA KUKUSANYA TAKWIMU SAHIHI ZA KITAFITI

UTEKELEZAJI WA UFUGAJI SAMAKI KWA VIZIMBA WAANZA ZIWA TANGANYIKA

TANZANIA DAIRY BOARD