PROF. SHEMDOE AIPONGEZA WIZARA YA MIFUGO NA UVUVI KWA HUDUMA NZURI KWA WAFUGAJI NA UVUVI
Na Chiku Makwai – Dodoma
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM–TAMISEMI), Prof. Riziki Shemdoe, ameipongeza Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kutoa Huduma nzuri na elimu nzuri kwa wafugaji na wavuvi, pamoja na mafanikio makubwa walioyapata katika kufanya mageuzi katika Sekta zote mbili, huku akisisitiza umuhimu wa kuendelea kuwahudumia wananchi kwa weledi, uwajibikaji na kujali mahitaji yao ili kuongeza uzalishaji nchini.
Pongezi hizo amezitoa leo Juni 23, 2026 alipotembelea banda la Wizara ya Mifugo na Uvuvi katika kuhitimisha Maadhimisho ya Wiki ya Kitaifa ya Utumishi wa Umma kwa mwaka wa 2026, kwa niaba ya Katibu Mkuu Kiongozi, Dkt. Moses Kusiluka, yaliyofanyika katika viwanja vya Chinangali Park jijini Dodoma.
Akizungumza katika kilele cha Maadhimisho hayo, Prof. Shemdoe alisema ameridhishwa na ushiriki wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi katika maonesho hayo na juhudi zinazoendelea kufanywa na wataalamu wa sekta hiyo katika kuboresha huduma kwa wananchi na kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa.
“Hongereni sana Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kushiriki kikamilifu katika Wiki ya Kitaifa ya Utumishi wa Umma, na ninafuraha kuwaona mko hapa, na ninawapongeza kwa kazi nzuri mnayoifanya, pia muendelee kuwatumikia wananchi, na muendelee kuwasikiliza watumishi wenzetu ili kuweza kutatua changamoto zao na kuwawezesha kwa kutoa huduma bora kwa wananchi wote,” amesema Prof. Shemdoe.
Aidha, Prof. Shemdoe amesema kuwa Sekta ya Mifugo na Uvuvi ina mchango mkubwa katika kuimarisha usalama wa chakula, kuongeza kipato cha wananchi na kuchochea maendeleo ya kiuchumi nchini, na ni muhimu kuendelea kutumia teknolojia na ubunifu katika kuongeza tija ya uzalishaji na thamani ya mazao ya Mifugo na Uvuvi.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Dkt. Fabian Madele, aliwataka wataalamu wa Mifugo nchini kuendelea kuzalisha kwa wingi mbegu bora za malisho pamoja na Mifugo yenye tija ili kukidhi mahitaji ya wafugaji na kuongeza uzalishaji wa bidhaa za mifugo.
Pia, Dkt. Madele alisema Serikali inaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wataalamu na Taasisi za Sekta ya mifugo ili kuimarisha Tafiti, uzalishaji wa mbegu bora za malisho na kuboresha Mifugo, hatua ambazo zitasaidia kuongeza uzalishaji, kuimarisha lishe na kuinua kipato cha wafugaji nchini.
Dkt. Madele amebainisha kuwa Maadhimisho ya Wiki ya Kitaifa ya Utumishi wa Umma 2026 yamekuwa Jukwaa muhimu kwa Taasisi za umma kuonesha huduma mbalimbali wanazotoa kwa wananchi, ambapo Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeendelea kutoa elimu, huduma za ushauri wa kitaalamu pamoja na kuonesha mafanikio mbalimbali yaliyopatikana katika maendeleo ya sekta ya Mifugo na Uvuvi nchini.










Maoni
Chapisha Maoni