MHE. REGINA AITAMBUA WIZARA YA MIFUGO NA UVUVI KWA UBORA WA HUDUMA, AHIMIZA VIJANA KUNUFAIKA NA FURSA ZA SEKTA HIZO
Na Chiku Makwai— Dodoma,
Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais – UTUMISHI, Mhe. Regina Qwaray, ameipongeza Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa ushiriki wake mzuri katika Maadhimisho ya Kitaifa ya Wiki ya Utumishi wa Umma 2026, huku akieleza kuridhishwa na huduma, elimu na teknolojia mbalimbali zinazotolewa katika banda la wizara hiyo.
Mhe. Regina ametoa pongezi hizo leo Juni 22, 2026, wakati wa ziara yake ya kutembelea mabanda mbalimbali yaliyoshiriki katika Maadhimisho ya Kitaifa ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea katika viwanja vya Chinangali Park jijini Dodoma.
Akiwa katika banda la Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Mhe. Regina alipata fursa ya kujionea huduma mbalimbali zinazotolewa na wataalamu wa wizara pamoja na taasisi zake, ikiwemo elimu kuhusu teknolojia za kisasa za ufugaji wa kuku na samaki, huduma za ugani, pamoja na fursa za kiuchumi zinazopatikana katika sekta za mifugo na uvuvi.
Aidha, amewahimiza wananchi, hususan vijana, kujitokeza kutembelea banda hilo ili kupata elimu, maarifa na taarifa sahihi kuhusu fursa zilizopo katika sekta hizo ambazo zina mchango mkubwa katika ajira, uzalishaji na maendeleo ya uchumi wa taifa.
"Vijana wanapaswa kutumia fursa hii kujifunza teknolojia za kisasa za ufugaji na uvuvi pamoja na huduma zinazotolewa na Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi ili kujiongezea kipato na kuchangia maendeleo ya nchi," alisema Mhe. Regina.
Kwa upande wake, Afisa Rasilimali Watu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bi. Angeline Ungelle, ambaye alimkaribisha Naibu Waziri huyo katika banda la wizara, alieleza kuwa ushiriki wa wizara katika maadhimisho hayo unalenga kuwafikia wananchi kwa kutoa elimu, ushauri wa kitaalamu na kuhamasisha matumizi ya teknolojia za kisasa katika sekta za mifugo na uvuvi.
Bi. Ungelle aliongeza kuwa wataalamu kutoka wizara na taasisi zake wanaendelea kutoa huduma mbalimbali kwa wananchi wanaotembelea banda hilo, ikiwa ni pamoja na elimu kuhusu uzalishaji, afya ya mifugo, ufugaji wa samaki, uongezaji thamani wa mazao ya mifugo na uvuvi pamoja na fursa za uwekezaji zilizopo katika sekta hizo.








Maoni
Chapisha Maoni