DKT. LUTEGE: MAFUNZO YA MADAKTARI WA MIFUGO YATAIMARISHA FURSA ZA MASOKO YA NJE

Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeendelea kuimarisha uwezo wa wataalamu wa mifugo nchini kwa kuwapatia mafunzo yanayolenga kukidhi viwango vya kimataifa katika sekta ya mifugo, hatua itakayochangia kuongeza fursa za masoko ya mifugo na mazao yake ndani na nje ya nchi.

Akizungumza katika hafla ya kuhitimu mafunzo kwa Madaktari wa Mifugo iliyofanyika leo Juni 25, 2026 katika Ukumbi wa Royal Hotel jijini Dodoma, Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo nchini, Dkt. Benezeth Lutege, amesema mafunzo hayo yamekuja kufuatia tathmini iliyofanywa na Shirika la Afya ya Wanyama Duniani (WOAH) ili kubaini kama wataalamu wa mifugo nchini wanaendana na viwango vya kimataifa vinavyohitajika katika biashara ya mifugo na mazao ya mifugo.

"Kupitia ushirikiano kati ya Shirika la Afya ya Wanyama Duniani na Chuo Kikuu cha Minesota, Tanzania imepata fursa ya kushiriki katika mafunzo hayo ambapo wataalamu tisa (9)wamehitimu, huku wataalamu wengine 26 wakitarajiwa kuanza mafunzo kwa njia ya mtandao." Amesema Dkt. Lutege 

Aidha, Dkt. Lutege amesema mafunzo hayo yataendelea kutolewa kwa madaktari wa wanyama nchini kote ili kuongeza ufanisi katika usimamizi wa afya ya mifugo na usalama wa chakula, jambo litakaloisaidia Tanzania kufungua masoko zaidi ya kimataifa kutokana na kuongezeka kwa uaminifu wa bidhaa za mifugo zinazozalishwa nchini.

Kwa upande wake, mmoja wa wahitimu wa mafunzo hayo, Dkt. Nyalekwa Mashimo kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa, ameishukuru Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kuwezesha mafunzo hayo, akisema yamewaongezea uwezo wa kufanya tafiti na kutoa elimu kwa jamii kuhusu usalama wa chakula pamoja na namna ya kushirikisha wadau mbalimbali katika kuboresha afya ya mifugo na maendeleo ya sekta hiyo.






Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

UTEKELEZAJI WA UFUGAJI SAMAKI KWA VIZIMBA WAANZA ZIWA TANGANYIKA

LESENI, VIBALI VYA MAZAO YA MIFUGO NA VYAKULA VYA SAMAKI KUTOLEWA KWA NJIA YA KIELEKTRONIKI

DKT. MHEDE AONGOZA ZOEZI LA UCHANJAJI WA MIFUGO MKOANI IRINGA, WAFUGAJI WAPONGEZA HATUA YA SERIKALI