DKT. BASHIRU APIGA MARUFUKU KUKAMATWA KWA MALI ZISIZOHUSIKA NA UVUVI HARAMU
◼️Aelekeza kufutwa “ubalozi” wa Uvuvi haramu ziwa Tanganyika
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi. Dkt. Bashiru Ally Kakurwa amepiga marufuku wataalam kukamata mali zisizohusika wakati wa utekelezaji operesheni za udhibiti wa uvuvi usiofuata sheria kwenye maeneo yote nchini.
Balozi Dkt. Bashiru amesema hayo leo Juni 25,2026 Bungeni jijini Dodoma wakati wa kikao baina yake na wabunge wa mikoa ya Kigoma na Katavi ambacho kililenga kujadili zana za uvuvi wa ziwa Tanganyika.
“Nimeshamwelekeza Mkurugenzi wa Sheria Wizarani kwangu zifuatwe taratibu zote za kisheria ili vyombo na mali zote zilizokamatwa zirejeshwe kwa wahusika na kuanzia sasa wanaotekeleza operesheni hizo wakamate nyavu na wavuvi wanaojihusisha na Uvuvi huo usiofaa” Amesisitiza Balozi Dkt. Bashiru.
Aidha Balozi Dkt. Bashiru pia amewaelekeza wataalam kutowadhalilisha wavuvi hao wakati wa utekelezaji wa operesheni hizo ambapo amesisitiza kumchukulia hatua mtaalam yoyote atakayethibika kufanya hivyo.
Katika hatua nyingine Balozi Dkt. Bashiru amemwelekeza Mkurugenzi wa Uvuvi nchini kufuta na kuondoa cheo cha “balozi” wa uvuvi haramu kinachotumika kwa upande wa ziwa Tanganyika ambapo amesisitiza kuwa uongozi wake hautambui ubalozi wa aina hiyo.
Kwa upande wao wabunge wa mikoa ya Kigoma na Katavi mbali na kuipongeza Serikali kwa uamuzi wake wa kutofunga ziwa Tanganyika kwa sasa wamemuomba Balozi Dkt. Bashiru kupitia Wizara yake kuangazia fursa mbalimbali za sekta za Mifugo na Uvuvi zilizopo mkoani humo ikiwa ni pamoja na kuhamasisha ufugaji samaki kwa njia ya vizimba, ufugaji wa kuku na ng’ombe wa maziwa.





Maoni
Chapisha Maoni