Nav bar

Jumapili, 6 Julai 2025

ZAIDI YA MIFUGO MILIONI 70 KUCHWANJWA NCHI NZIMA

Na. Hamisi Hussein, RUVUMA

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi  Bi. Agnes Meena amesema Kampeni ya Kitaifa ya Chanjo na utambuzi wa mifugo kwa mwaka 2024/2025 itakamilika mwezi agosti ambapo zaidi ya mifugo milioni 70 itachanjwa nchi nzima kukingwa dhidi ya magonjwa yanayoathiri  biashara ya mifugo na mazao yake.

Bi. Meena amesema hayo Julai 5, 2025 wakati wa uhamasishaji wa  kampeni ya Kitaifa ya Uchanjaji na Utambuzi wa mifugo katika  katika kijiji cha Mpandangindo Halmashauri ya Wilaya ya Songea mkoani ni Ruvuma ambapo amewahakikishia wafugaji wote nchini kuwa chanjo za mifugo ni salama  kwa mifugo yote. 

" Kampeni hii ni ya miaka mitano sahivi tunachanja na hadi  mwezi agosti mwaka huu mpango huu utakuwa umekamilika ambapo tutakuwa tumechanja ng'ombe milioni 19, Mbuzi na Kondoo milioni 17 na Kuku milioni 40, chanjo zetu ni salama kwa ajili ya mifugo yetu" amesema Bi. Meena.

Aidha Katibu Mkuu Bi. Meena amewahimiza wafugaji wote nchini kushiriki kikamilifu katika zoezi hilo kwa kutoa mifugo yao kupata chanjo.

Kwa upande wake Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma Jumanne Mwankhoo amesema mkoa huo utaendelea kumilikisha ardhi  kwa wafugaji ili kuondoa migogoro inayojitokeza  baina  ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi.

"Sisi kama mkoa tutawamilikisha wafugaji  maeneo  kwa ajili ya malisho ikiwa ni hatua muhimu za kukabiliana na migogoro ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi." Alisema Jumanne.

Kwa upande wake  Katibu wa Chama cha Wafugaji Tanzania Kanda ya Kusini (CCWT) Prisca Kaponda amemewahimiza wafugaji wote wa kanda huo kushirki kikamilifu Kampeni ya chanjo na Utambuzi wa Mifugo kwani Chanjo hizo ni salama kwa sababu zimezalishwa ndani ya nchi.

Katibu Mkuu wa Wizara  ya Mifugo na Uvuvi Bi. Agnes Meena (Wa pili, kutoka kulia) Akishuhudia Dkt. Justinian Lutatina Afisa Mfawidhi (ZVC) Kanda ya Kusini  akionyesha jinsi mfumo wa utambuzi mifugo wa Kielekitroniki unavyofanya kazi wakati ziara ya kukagua  Utekelezaji wa Kampeni ya Kitaifa ya Chanjo na Utambuzi wa Mifugo mkoani Ruvuma Julai 05,2025.

Katibu Mkuu wa Wizara  ya Mifugo na Uvuvi Bi. Agnes Meena (Kushoto) Akimpa Kuku chanjo ya mdondoo kuashiria kuanza kwa utekelezaji wa kampeni ya Kitaifa ya Chanjo na Utambuzi wa Mifugo mkoani Ruvuma Julai 05, 2025, wengine ni Kaimu Katibu wa Mkoa wa Ruvuma Jumanne Munkhoo (Katikati) na Katibu wa Chama cha Wafugaji Tanzania (CCWT) kulia .


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni