Nav bar

Jumapili, 6 Julai 2025

HATUNA DENI NA RAIS SAMIA-WAFUGAJI

 Na. Omary Mtamike

◼️Takribani Mifugo 3000 yachanjwa na kutambuliwa mkoani Mara

Chama cha Wafugaji nchini kupitia Mwenyekiti wao Bw. Murida Mshota kimemshukuru Rais wa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuboresha sekta ya Mifugo na kuwawezesha kufuga kisasa.

Bw. Mshota amesema hayo Julai 04, 2025 Wilayani Bunda wakati wa ziara ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji iliyolenga kukagua utekelezaji wa kampeni ya kitaifa ya Chanjo na Utambuzi wa Mifugo mkoani Mara ambapo amebainisha namna wanavyotarajia kunufaika na fursa ya ruzuku ya chanjo hizo kwa kipindi cha miaka 5 ya utekelezaji wake.

“Hii chanjo ambayo inatolewa leo  kwa ng’ombe mmoja zamani mfugaji alikuwa akitoa elfu 17 lakini leo Serikali imesema tutoe 500 tu hiyo nyingine wataibeba wenyewe, mbuzi wetu watachanjwa kwa shilingi 300 tu na Kuku watachanjwa bure lakini pia hapa limejengwa josho la kisasa lililogharimu Mil.28 kwa kweli tunasema Asante Dkt. Samia “Ameongeza Bw. Mshota.

Akizungumza na Wafugaji wa mkoa huo Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji amesema kuwa ni mara ya kwanza kwa Serikali kuendesha zoezi hilo kwa mtindo wa kampeni ya kitaifa tofauti na ilivyokuwa ikifanyika awali ambapo kila mfugaji alikuwa akichanja kwa wakati wake. 

“Mhe. Rais anataka kuona tunaongeza thamani ya mifugo tuliyonayo na anahitaji tuidhihirishie dunia utajiri tulionao kupitia sekta ya Mifugo” Ameongeza Mhe. Dkt. Kijaji.

Aidha Mhe. Dkt. Kijaji amebainisha kuwa kufanikiwa kwa kampeni hiyo kumetokana na ushirikiano mkubwa walioupata kutoka kwa wafugaji ambapo amewataka kuendelea kushirikiana na Serikali katika zoezi hilo litakaloiwezesha Mifugo yao kushindana kwenye soko la kimataifa.

Ziara hiyo ya Mhe. Dkt. Kijaji iliyolenga kukagua utekelezaji wa kampeni ya kitaifa ya Chanjo na Utambuzi wa Mifugo iliyozinduliwa Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu Juni 16, 2025 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan itaendelea katika mikoa ya Simiyu, Geita, Pwani, Morogoro, Tabora na Dodoma.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (kulia) Akitoa chanjo ya mdondo wa kuku kama ishara ya kuanza kwa utekelezaji wa kampeni ya kitaifa ya Chanjo na Utambuzi wa Mifugo mkoani Mara Julai 04,2025. Kushoto ni Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Evance Mtambi.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji, Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Evance Mtambi na Viongozi wa Chama cha Wafugaji nchini wakishuhudia namna zoezi la utoaji wa chanjo za Mifugo linavyofanyika mara baada ya kuanza kwa utekelezaji wa kampeni ya kitaifa ya Chanjo na Utambuzi wa Mifugo mkoani humo Julai 04,2025.






Hakuna maoni:

Chapisha Maoni