◼️ Tume ya Ushirika yawamwagia sifa Heifer
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. David Silinde amesema kuwa Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeelekeza nguvu kubwa kwenye vyama vya ushirika kwa sababu inaamini ndio utakuwa mkombozi kwa wakulima, wafugaji na wavuvi nchini.
Mhe. Silinde amebainisha hayo Juni 27, 2023 wakati akifungua Maadhimisho ya kitaifa ya Siku ya Duniani yanayofanyika kwenye viwanja vya Nanenane mkoani Tabora ambapo ameweka wazi hatua mbalimbali zilizochukuliwa na Wizara za Kilimo na Mifugo na Uvuvi katika kuhakikisha Ushirika nchini unaimarika na unakuwa na tija kwa wananchi hasa wenye kipato cha chini.
“Kwa mujibu wa takwimu wa takwimu hadi kufikia mwezi Januari 2023, kuna vyama vya ushirika vya wafugaji 216 ambavyo ni kutoka mikoa ya Arusha, Dar-es-salaam, Dodoma, Geita, Katavi. Kigoma, Kilimanjaro, Manyara, Mara, Mbeya, Morogoro, Mwanza, Njombe, Pwani, Shinyanga, Tanga na Songwe vikiwa na jumla ya wanachama 637,000” Amebainisha Mhe. Silinde.
Aidha Mhe. Silinde amesema kuwa mbali na vyama hivyo vya ushirika kwa upande wa wafugaji, takwimu zinaonesha kuwa vipo vyama vya ushirika 130 vinavyojishughulisha na shughuli za uvuvi kutoka mikoa ya Dar-es-salaam, Dodoma, Geita, Katavi, Kigoma, Lindi, Mara, Mbeya, Morogoro, Mtwara, Mwanza, Pwani, Rukwa, Ruvuma, Tabora na Tanga vyenye jumla ya wanachama 415,000.
“Vyama hivi vimekuwa msaada mkubwa sana katika kuwatafutia wanachama wake pembejeo, maeneo bora ya malisho, huduma za ugani na vifaa bora kwa gharama nafuu, mashine za kuchakata na kusindika mazao ya mifugo na uvuvi, uhifadhi na masoko ya mazao na bidhaa zinazotokana na shughuli za uvuvi na ufugaji” Amesisitiza Mhe. Silinde.
Kwa upande wake Mrajis wa Tume ya Ushirika nchini Dkt. Benson Ndiege amesema kuwa Tume yake imeendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuhamasisha ushirika kwa upande wa sekta za Mifugo na Uvuvi ikiwemo Wizara ya Mifugo na Uvuvi huku kwa upande wa sekta binafsi akilitaja Shirika la kimataifa la Heifer.
“Shirika la Heifer limekuwa mstari wa mbele katika kuanzisha vyama vya Ushirika kwa upande wa sekta ya Mifugo na kuvifanya viendeshe shughuli zao kisasa zaidi na katika mradio wao uliokamilika wa mwaka 2029/2022 walitumia zaidi ya shilingi milioni 522 kwa ajili ya kuimarisha vyama vya Ushirika nchini.
Maadhimisho ya Siku ya Ushirika Duniani kwa mwaka huu yamebebwa na kauli mbiu isemayo “Ushirika kwa Maendeleo Endelevu” ambapo yatafanyika mpaka Julai 1, 2023.
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. David Silinde akikata utepe kuashiria ufunguzi wa Maadhimisho ya kitaifa ya Siku ya Ushirika Duniani tukio lililofanyika Juni 27,2023 kwenye Viwanja vya Nanenane mkoani Tabora yanakofanyika Maadhimisho hayo.
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. David Silinde (katikati) akimuangalia samaki aliyekaushwa kwa teknolojia ya mionzi ya jua muda mfupi baada ya kufika kwenye banda la mkoa wa Mwanza lililopo kwenye Viwanja vya NaneNane Mkoani Tabora Juni 27, 2023 yanakofanyika Maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Ushirika Duniani.
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. David Silinde akizindua kitabu cha programu zitakazotekelezwa kwenye Maadhimisho ya kitaifa ya Siku ya Ushirika Duniani tukio lililofanyika Juni 27, 2023 kwenye viwanja vya Nanenane mkoani Tabora yanakofanyika Maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Ushirika Duniani.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni