Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Tixon Nzunda amebainisha kuwa wafugaji wanaovamia maeneo ya ranchi ni wahalifu na wanapaswa kukamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria kama ilivyo kwa wahalifu wengine.
Nzunda ameyasema hayo leo (29.09.2022) wakati wa kikao baina yake na wawekezaji wa ranchi ya Mzeri iliyopo Handeni mkoani Tanga ambapo amesisitiza wafugaji kufuata sheria wakati wote wa utekelezaji wa shughuli zao.
"Imezuka tabia ya baadhi ya wananchi kuvamia maeneo yaliyotengwa na Serikali kwa dhana kuwa watamilikishwa maeneo hayo baada ya muda mfupi, sasa niwahakikishie hilo kwa upande wa ranchi halipo na halitatokea kamwe" Ameongeza Nzunda.
Aidha Nzunda ametoa onyo kwa wavamizi wa ranchi hiyo waliomjeruhi Meneja wa ranchi hiyo Bw. Mbelwa Lutagwelera ambapo ameweka wazi kuwa mkondo wa sheria hautawaacha salama na kutoa rai kwa wananchi wengine wenye tabia kama hiyo kuacha mara moja.
"Kwenye hili eneo la kuboresha ranchi zetu tupo very "serious" kwa sababu ndio maono ya Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan na kwa kuanzia ametoa fedha za kununua ng'ombe 500 watakaoanza kufugwa kwenye ranchi hii ya Mzeri" Amesema Nzunda.
Katika hatua nyingine Nzunda ameendelea kuwasisitiza wawekezaji waliopo kwenye ranchi zote zilizopo hapa nchini kufuga kisasa na kuhakikisha wanalipa kodi za vitalu wanazodaiwa ambapo ameweka wazi kwa wasio tayari kufanya hivyo waondoke mara moja kwenye ranchi hizo.
Mbali na kuitembelea ranchi ya Mzeri, Nzunda alihitimisha ziara yake mkoani Tanga kwa kufika kwenye moja ya mashamba yanayomilikiwa na Taasisi ya Utafiti wa Mifugo nchini (TALIRI) ili kuona ilipofikia hatua ya moja ya vituo atamizi vya mafunzo ya unenepeshaji wa mifugo kinachotarajiwa kuwepo kwenye mashamba hayo.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Bw. Tixon Nzunda (kushoto) akimueleza mmoja wa wawekezaji wadogo waliopo Ranchi ya Mzeri mkoani Tanga Bw. Twalib Mwaita (kulia) kuhusu umuhimu wa kuweka hereni za kielektroniki kwenye mifugo yake wakati wa Ziara yake kwenye ranchi hiyo iliyofanyika leo (29.09.2022).
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Bw. Tixon Nzunda akitoa maelekezo ya namna ya kufanya ufugaji wenye tija kwa wawekezaji waliopo kwenye ranchi ya Mzeri iliyopo Mkoani Tanga wakati wa ziara yake kwenye ranchi hiyo iliyofanyika leo (29.09.2022)
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Bw. Tixon Nzunda (kulia) akiwaeleza baadhi ya vijana waliochaguliwa kwenye kituo atamizi kitakachoanza hivi karibuni mkoani Tanga kwenye moja ya mashamba ya Taasisi ya Utafiti wa Mifugo (TALIRI) kuhusu umuhimu wa ushiriki wao kwenye mafunzo ya Unenepeshaji wa mifugo alipofika kituoni hapo leo (29.09.2022)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni