Nav bar

Alhamisi, 29 Septemba 2022

WAZIRI NDAKI: "TALIRI FANYENI TAFITI ZENYE TIJA KUELEKEA SERA MPYA YA MIFUGO."

Na. Edward Kondela


Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (Mb) ameitaka Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) kushiriki kikamilifu katika tafiti zitakazoleta tija kwa wafugaji wakati serikali ikielekea kuwa na sera mpya ya mifugo.


Waziri Ndaki amebainisha hayo (22.09.2022) jijini Dodoma wakati akizindua rasmi bodi ya TALIRI na kubainisha kuwa ni vigumu kuwa na sera bila kuwa na tafiti hivyo TALIRI inapaswa kufanya tafiti hizo kwa kuzingatia maelekezo, ubora na mahitaji ya wafugaji kwa kuwa mahitaji ni mengi na changamoto ni nyingi zinazohitaji utatuzi.


Amefafanua kuwa kwa vile serikali inaelekea kuwa na sera mpya ya mifugo TALIRI inapaswa kushiriki kikamilifu ili kufahamu muelekeo wa namna sekta ya mifugo inaweza kuendeshwa kwa kuzingatia hali halisi ya sasa.


“Kutokana na mabadiliko ya tabia ya nchi, tukizingatia wingi wa shughuli za binadamu, mazingira ya sasa kwa namna ya masoko ya bidhaa za mifugo uzalishaji na biashara ya mifugo kwa ujumla masuala ya namna hiyo lazima kwenye sera yatuelekeze namna ya kuendesha sekta ya mifugo.” Amesema Waziri Ndaki


Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) Prof. Sebastian Chenyambuga amesema bodi hiyo itahakikisha inasimamia masuala ya utafiti kadri inavyotakiwa kwa kutoa matokeo ya namna ya kuendesha sekta ya mifugo na kutatua changamoto zilizopo.


Prof. Chenyambuga ameongeza kuwa bodi itaisimamia pia TALIRI kufanya tafiti za masuala mbalimbali ambayo yamekuwa yakiibuka ghafla na mengine kusababisha taharuki kwa umma.


Awali, katika kikao hicho kabla ya bodi hiyo kuzinduliwa rasmi na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (Mb), Katibu Mkuu katika wizara hiyo anayesimamia sekta ya mifugo Bw. Tixon Nzunda amewaambia wajumbe wa bodi ya TALIRI kuwa na mpango wa upatikanaji wa fedha ili taasisi iweze kupata rasilimali za kufanya tafiti kwa kuwa gharama za utafiti ni kubwa.


Aidha, amesema bodi ni lazima ije na mpango wa mabadiliko ya taasisi hiyo ambao unalingana na mahitaji ya sasa ambao utashirikisha sekta binafsi wakiwemo wachakataji na wazalishaji wa viwandani.


Bodi ya Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) ambayo imezinduliwa rasmi na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (Mb) itakaa madarakani kwa kipindi cha miaka mitatu.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (Mb) akimkabidhi Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) Prof. Sebastian Chenyambuga (kushoto) baadhi ya nyaraka za taasisi hiyo baada ya Mhe. Ndaki kuzindua rasmi bodi ya TALIRI wakati wa kikao kilichowahusisha wajumbe wa bodi na menejimenti ya taasisi hiyo jijini Dodoma. (22.09.2022)

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (Mb) akikata utepe kwenye baadhi ya nyaraka za Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) kuashiria kuzindua rasmi bodi ya taasisi hiyo wakati wa kikao kilichowahusisha wajumbe wa bodi wakiongozwa na mwenyekiti wao pamoja na menejimenti ya taasisi hiyo jijini Dodoma. (22.09.2022)

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (Mb) akizungumza wakati wa uzinduzi wa bodi ya Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) uliofanyika jijini Dodoma ambapo ameitaka TALIRI kushiriki kikamilifu katika tafiti zitakazoleta tija kwa wafugaji wakati serikali ikielekea kuwa na sera mpya ya mifugo. (22.09.2022)

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Tixon Nzunda akizungumza wakati wa uzinduzi wa bodi ya Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) uliofanyika jijini Dodoma ambapo ameitaka TALIRI kuwa na mpango wa upatikanaji wa fedha ili taasisi iweze kupata rasilimali za kufanya tafiti pamoja na kuwa na mpango wa mabadiliko ya taasisi hiyo ambao unalingana na mahitaji ya sasa kwa kushirikisha sekta binafsi wakiwemo wachakataji na wazalishaji wa viwandani. (22.09.2022)

Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) Prof. Sebastian Chenyambuga akizungumza wakati wa uzinduzi wa bodi ya TALIRI uliofanyika jijini Dodoma ambapo amesema bodi hiyo itahakikisha inasimamia masuala ya utafiti kadri inavyotakiwa kwa kutoa matokeo ya namna ya kuendesha sekta ya mifugo na kutatua changamoto zilizopo na itaisimamia pia TALIRI kufanya tafiti za masuala mbalimbali ambayo yamekuwa yakiibuka ghafla na mengine kusababisha taharuki kwa umma. (22.09.2022)

Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) Prof. Erick Komba akizungumza wakati wa uzinduzi wa bodi ya TALIRI uliofanyika jijini Dodoma ambapo amesema atahakikisha anasimamia maelekezo yote yatakayotolewa na bodi na kwamba taasisi hiyo itafanya utafiti wenye kuleta matokeo chanya kwa wafugaji na watumiaji wa bidhaa za mifugo. (22.09.2022)


Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (Mb), (aliyekaa katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na wajumbe wa bodi ya Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) mara baada ya kuzindua rasmi bodi hiyo jijini Dodoma. (22.09.2022)

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (Mb), (aliyekaa katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na menejimenti ya Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) mara baada ya kuzindua rasmi bodi ya taasisi hiyo jijini Dodoma. (22.09.2022)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni