Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki amewataka wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi kuwekeza katika sekta ya mifugo huku akisisitiza kuwa mazingira ya uwekezaji kwa sasa hapa nchini ni salama chini ya Uongozi wa Rais wa jamuhuri wa muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan.
Aliyasema hayo katika uzinduzi wa shamba la kuku wazazi
la kuzalisha babu na bibi (grand
parent stock) uliofanyika wilayani siha Mkoani Kilimanjaro Septemba 2, 2022.
Amesema Uzinduzi wa mradi
huo uliogharimu Dola za kimarekani Milioni 15 utasaidia kupanua sekta ya kuku
nchini pamoja na kuongeza lishe kwa
watanzania kutokana na bidhaa zitokanazo
na kuku.
"Sisi kama Wizara
tunapongeza uwekezaji huu utakaosaidia kupanua sekta ya kuku nchini,
utachechemua biashara na kuongeza mzunguko wa fedha, hivyo tunamshukuru
Rais Samia kwa kuweka mazingira mazuri
ya uwekezaji hapa nchini na matokeo
yake tunayaona," alisema
Aliongeza kwa kusema kuwa
kuku watakaozalishwa katika shamba hilo
watauzwa maeneo mbalimbali hapa nchini pamoja na nje ya nchi hali
itakayopelekea ongezeko la kipato kwa mtu mmoja moja na taifa kwa ujumla.
Aidha aliwataka wananchi wa
wilaya ya Siha kuwakumbatia wawekezaji
wa shamba hilo lengo likiwa ni kunufaika na ufugaji huo ikiwa ni pamoja na
kuuza vifaranga hao kwa nchi za jirani.
" Tumekuwa tukiagiza vifaranga wazazi kutoka nje na kutumia fedha nyingi, uwepo wa mradi huu utapunguza matumizi ya fedha za kigeni na kukuza uchumi wa nchi kwa kuwa tutakuwa tunazalisha hapa hapa nchi, aliongeza
Pia, alifafanua kuwa uwepo
wa wawekezaji hao utasaidia kutekeleza adhma ya serikali ya kutengeneza ajira zaidi ya milioni 8 ifikapo 2025 pamoja na kuongeza
kipato cha mtu mmoja mmoja.
Akielezea mradi huo
mwenyekiti wa kampuni ya Aviagen Afrika Mashariki Bw. Kester lyaruu alisema
kuwepo kwa mradi huo kutachangia kuleta usalama wa chakula pamoja na kuzuia
uingizwaji wa vifaranga visivyo salama kutoka nje ya nchi.
"Mradi huu utasaidia
uchumi wa nchi na kuongeza lishe kwa wananchi wa kawaida ambao wataweza kupata
vifaranga hao kwa bei nafuu" alisema Lyaruu
Aidha Mkuu wa Wilaya ya Siha Mhe. Thomas Apson alisema mradi huo wa kuku ni wa kuzalisha vifaranga wazazi mababu na mabibi watakaoendelea kuzalisha kuku wengi zaidi.
Naye mwananchi kutoka
Wilaya ya Siha Bi. Witness Philemon alisema, wanapata ajira mbalimbali kutokana
na uwekezaji huo na kuiomba Serikali kuanzisha miradi ya ufugaji kuku katika
vijiji na vitongoji Ili kusaidia kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa
ujumla.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi
Mhe. Mashimba Ndaki akiongea na wananchi pamoja na watendaji wa shamba la
uzalishaji wa kuku wazazi (Aviagen East Africa) ( hawapo pichani) wakati wa
uzinduzi wa shamba hilo uliofanyika kwenye Wilaya ya Siha Mkoani kilimanjaro,
Septemba 2, 2022
Waziri wa Mifugo na Uvuvi
Mhe. Mashimba Ndaki ( wa tatu kutoka kulia) akikata utepe ishara ya uzinduzi wa
shamba la uzalishaji kuku wazazi lililopo kwenye Wilaya ya Siha Mkoani
kilimanjaro Septemba 2, 2022.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni