Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Bw. Tixon Nzunda amewataka vijana kuchangamkia fursa mbalimbali zinazotolewa na Serikali pamoja na Asasi binafsi ili kuweza kupambana na tatizo la ukosefu wa Ajira nchini
Nzunda ameyasema hayo jana tarehe 29Juni 2022 Mjini Morogoro wakati wa hafla ya tathimini na ufungaji wa mradi wa uchumi kwa Vijana uliokuwa unafadhiliwa na shirika la Care International Tanzania.
"Kupitia maradi huu wa Uchumi kwa Vijana, baadhi ya vijana waliobahatika kuingia katika Mradi huu wameweza kunufaika na Mafunzo ya ufugaji na kujitegemea, sasa ni wajibu wao kuhakikisha elimu hii inawafikia vijana wengine pamoja na makundi mengine". Alisema Nzunda.
Aidha, Nzunda aliongeza kwa kusema, “Ripoti ya mradi huu imeonyesha kwamba mpaka kufikia Mei 2022, vikundi 1040 viliundwa vikiwa na idadi kubwa ya Vijana wa Kike na wanawake kwa asilimia 64. Natoa pongezi za dhati kwa Halmashauri zote katika Mikoa ya Morogoro, Njombe na Mbeya kwani ndio waliosimamia kazi ya uundaji wa vikundi hivi.”
Nzunda alisema kuwa kwa mfumo huo ni dhahiri kwamba, hata shirika la Care International Tanzania au wadau wengine wasipo kuwepo, vijana wataendelea na wanaweza kuendelea kuhamasishana kaunda Vikundi mbalimbali vya Ufugaji kwa lengo la kujikwamua kiuchumi.
Vilevile, Katibu Mkuu Mifugo Bw. Nzunda ametoa maelekezo kwa Maafisa Maendeleo ya Jamii wa Mikoa na Halmashauri kuhakikisha vikundi vyote 1040 vilivyoundwa na kuwezeshwa na Care International Tanzania vinafuatiliwa na kusaidiwa kwa kutoa ushauri wa kitaalam ikiwa ni pamoja na kusaidiwa kupata mikopo ya asilimia 15 kwa ajili wa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
Nzunda amewataka Maafisa Biashara wa Halmashauri kushirikiana na maafisa maendeleo ya Jamii, ili vikundi ambavyo vimeanza uzalisha katika maeneo mbalimbali katika Mikoa ambayo mradi huo wa Uchumi kwa Vijana ulikuwa unatekelezwa, kuhakikisha vikundi hivyo vinapata uhakika wa soko la bidhaa hizo zinazozalishwa.
"Tumefahamishwa kuwa katika mradi huu wa uchumi, vijana wengi wamejikita katika ufugaji wa Kuku, Ng’ombe na Nguruwe, hivyo naelekeza kurugenzi ya Utafiti, Mafunzo na Ugani kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) pamoja na LITA kuhakikisha mnafuatilia vikundi hivi vilivyoanza uzalishaji, na kushirikiana nao katika kutafuta masoko ya uhakika ya bidhaa hizo za Mifugo wanazozalisha".Alisema Nzunda.
Pia, ninaelekeza Kurugenzi za Mafunzo, utafiti na Ugani katika Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) na Wizara ya Kilimo kuona namna bora zitakavyotumia miongozo na mikakati mbalimbali iliyotumika kutekeleza mradi huu wa Uchumi kwa Vijana na kuchukua baadhi ya mbinu bora na kuzijumuisha katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali za kurugenzi zao katika Wizara zote mbili ili kuleta ufanisi mkubwa.
Katibu Mkuu Mifugo Bw. Tixon Nzunda amesema kuwa Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mama Samia Suluhu Hassan itaendelea kuweka mazingira rafiki kwa kuhakisha vijana wanaweza kujiajili kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo nchini.
Awali Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Bw.Tixon Nzunda alibainisha Misingi ya Mafanikio kwa Vijana kuwa ni pamoja na kuwa na Moyo wa kupenda kazi na kujituma, Uadilifu na uaminifu ili vijana waendelee kuaminika, Ubunifu na uthubutu.
Msingi mwingine wa Mafanikio kwa Vijana Nzunda alitaja kuwa ni Matumizi sahihi ya rasirimali, Kuwa na Maono na malengo ya kuona mbali, utunzaji na matumizi sahihi ya taarifa na uzalendo na utu mwema.
Katika Hatua nyingine, Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro Bi. Mariamu Mtunguja aliwaomba wasimamizi wa mradi huo kutoka Care International Tanzania kuhakikisha wanawafikia vijana wengi katika maeneo ambayo mradi huo haujafika ili kuweza kuwanusuru vijana ambao hawana ajira.
Naye mkurugenzi Mkazi wa Care International Tanzania Bi. Prudence Masako amesema kuwa Care International imekuwa na miradi kadhaa wa kadhaa ikiwemo ya kuimarisha afya ya mama na mtoto, Usawa wa Kijinsia na kwa sasa wamejikita katika kuimarisha uchumi wa vijana.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Miradi kutoka Care International Tanzania, Haika Mtui amesema kuwa waliamua kuja na mradi wa Uchumi kwa Vijana mara baada ya kugundua kuwa kundi kubwa la Vijana halina ajira hivyo kuja na mbinu ya kuwajengea uwezo katika Ufugaji, Kilimo na ufundi ili waweze kujiajiri.