Na Mbaraka Kambona,
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega ameitaka taasisi ya Utafiti wa Mifugo(TALIRI) na taasisi inayoshughulika na kilimo biashara(PASS) kuhakikisha wanakuwa na vipaumbele vichache watakavyoweza kutekeleza vyema ili mradi wa kunenepesha mbuzi wanaoutekeleza uweze kufikia malengo waliyokusudia.
Ulega alitoa maelekezo hayo katika kikao kazi cha kupata taarifa ya utekelezaji wa mradi wa kunenepesha mbuzi unaotekelezwa kwa ushirikiano na taasisi hizo mbili kilichofanyika jijini Dodoma Juni 22, 2022.
Alisema kwa sasa sekta ya mifugo inakabiliwa na changamoto kubwa ya malisho na uhaba wa malighafi zinazotokana na mifugo hivyo ni muhimu wakajikita katika kuzalisha malisho ili mifugo iwe na malisho ya kutosha wakati wote jambo litakalopelekea mifugo hiyo kuwa na uzito na kuwa na thamani sokoni.
"Katika taarifa zenu nimewasikia hapa mmeeleza mambo mengi mnayotarajia kufanya kupitia mradi mnaotekeleza, ushauri wangu ni muhimu mkachagua mambo machache mtakayoweza kutekeleza vizuri awamu kwa awamu kuliko kubeba mambo mengi na mwisho wa siku msiweze kufikia malengo," alisema Ulega
Aliongeza kwa kuwahimiza kujikita hasa katika unenepeshaji wa mbuzi na uzalishaji wa malisho huku akiwataka kutumia utaalamu wao kufundisha vijana ufugaji wa biashara ili waweze kujiajiri na kujiongezea kipato.
Aidha, kufuatia changamoto ya kufa kwa mifugo iliyoikumba nchi hivi karibuni aliwataka wao kama Wataalamu kuhakikisha wanatumia taaluma zao kikamilifu ili kupunguza vifo vya mifugo nchini.
Halikadhalika aliitaka Benki ya Maendeleo ya Kilimo(TADB) kusaidia wadau hao wa sekta ya mifugo kwa kuandaa mipango mizuri ya biashara na kutoa mikopo nafuu kwa wafugaji ili waweze kufanya ufugaji wenye tija.
Naye, Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti, Mafunzo na Ugani, Dkt. Angelo Mwilawa alisema kuwa kwa muda sasa viwanda vingi vya kuchakata nyama hapa nchini vimekuwa vikifanya kazi chini ya uwezo wake hivyo kupitia mradi huo unaotekelezwa na TALIRI kwa kushirikiana na PASS ukisimamiwa vizuri utakwenda kuwa sehemu ya utatuzi wa changamoto hiyo.
Aliongeza kwa kusema kuwa mradi huo pia utashirikisha Halmashauri nchini ili vijana waliopo katika maeneo hayoo waweze kushirikishwa vizuri katika kujifunza unenepeshaji wa mifugo na kuboresha maisha yao.
Kaimu Mkurugenzi, Idara ya Sera na Mipango (sekta ya mifugo), Bw. Mbaraka Stambuli akifafanua jambo katika kikao kazi cha kupata taarifa ya utekelezaji wa mradi wa kunenepesha mbuzi unaotekelezwa na taasisi ya Utafiti wa Mifugo(TALIRI) na taasisi inayojishughulisha na masuala ya kilimo biashara(PASS) katika kituo cha Kongwa kilichofanyika jijini Dodoma Juni 22, 2022.
Pichani ni Sehemu ya washiriki wa kikao kazi cha kupata taarifa ya utekelezaji wa mradi wa kunenepesha mbuzi unaotekelezwa na taasisi ya Utafiti wa Mifugo(TALIRI) na taasisi inayojishughulisha na masuala ya kilimo biashara(PASS) katika kituo cha Kongwa kilichofanyika jijini Dodoma Juni 22, 2022.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni