Nav bar

Ijumaa, 24 Juni 2022

MIFUGO NA UVUVI YATUNUKIWA TUZO YA UTAWALA BORA

Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Sekta ya Mifugo) imeshika nafasi ya pili kwenye tuzo za Utawala Bora zinazotolewa na Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa kufanya vizuri kwenye upande wa utendaji bora katika utoaji wa huduma kwa watumishi na wananchi kwa mwaka wa fedha 2021/2022.


Akipokea tuzo hiyo kwenye ofisi za Wizara zilizopo Mtumba Jijini Dodoma Juni 21, 2022 Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Sekta ya Mifugo, Bwana Tixon Nzunda alisema kuwa tuzo hiyo imepatikana kutokana na ushirikiano mkubwa ulipo katika kufanya kazi kama timu, kwa weledi, uadilifu na uwajibikaji kwa umma.


“Nitumie fursa hii kuwashukuru watumishi wote wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kuwezesha tuzo hii kupatikana, tumefanyiwa tathimini kwenye eneo la utawala bora ambapo tumeshika nafasi ya pili, tuchukue hii kama changamoto kwa kufanya vizuri zaidi kwenye tuzo zingine,” 


“Nishani hii ni kama chachu ya kufanya mabadiliko makubwa ili mwaka ujao tusiongoze tu kwenye masuala ya utawala bora, masuala ya ushughulikiaji wa malalamiko, taarifa za watumishi, lakini pia tuwe vinara katika kusimamia miradi ya maendeleo katika sekta zetu, kuanzia minada, mabwawa, visima, majosho, ufuatiliaji wa miradi na kuhakikisha kwamba thamani ya fedha ya miradi yetu inapatikana.” Alisema Bwana Nzunda


Akiongea kwenye makabidhiano ya Tuzo hiyo, Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu Sekta ya Mifugo, Dtk. Charles Mhina alisema tuzo hiyo ya Utendaji Bora imetolewa Mei 27, 2022 kwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Sekta ya Mifugo) kwa kufanya vizuri kwenye uingizwaji wa taarifa sahihi katika mfumo wa taarifa za utumishi na mishahara. 


Vigezo vingine ni pamoja na uhuishaji wa taarifa kwenye mfumo kwa wakati, ushughulikiaji wa malalamiko ya watumishi na wananchi kwa wakati, kuzingatia na kutekeleza sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma na sheria mbalimbali za nchi katika kazi zote za kila siku.


Tuzo hizi za Utawala Bora zinazotolewa na Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kila mwaka na zinajumuisha wizara zote zilizopo Tanzania bara ambapo nafasi ya kwanza imechukuliwa na Ofisi ya Rais Ikulu, nafasi ya pili imechukuliwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi na nafasi ya tatu imechukuliwa na  Wizara ya Fedha na Mipango.


Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughurikia Sekta ya Mifugo, Bwana Tixon Nzunda (aliyeshika Tuzo) akiongea na baadhi ya watumishi kwenye ofisi za Wizara zilizopo Mtumba Jijini Dodoma mara baada ya kukabidhiwa Tuzo ya mshindi wa pili ya Utawala Bora iliyotolewa na Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa kufanya vizuri kwenye upande wa utendaji bora katika utoaji wa huduma kwa watumishi na wananchi kwa mwaka wa fedha 2021/2022,  Juni 21, 2022.

Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dtk. Charles Mhina (kushoto) akitoa maelezo kwa Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Sekta ya Mifugo Bwana Tixon Nzunda kuhusu vigezo vilivyotumiwa na Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwenye utoaji wa Tuzo za Utawala bora na kupelekea Wizara ya Mifugo na Uvuvi kushika nafasi ya pili kwa mwaka wa fedha 2021/2022, kwenye ofisi za Wizara zilizopo Mtumba Jijini Dodoma Juni 21, 2022.

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Sekta ya Mifugo Bwana Tixon Nzunda akiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya watumishi kwenye ofisi za Wizara zilizopo Mtumba Jijini Dodoma mara baada ya kukabidhiwa Tuzo ya mshindi wa pili ya Utawala Bora iliyotolewa na Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa kufanya vizuri kwenye upande wa utendaji bora katika utoaji wa huduma kwa watumishi na wananchi kwa mwaka wa fedha 2021/2022, Juni 21, 2022.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni