Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki amesema kuwa maeneo yote ya malisho yaliyotengwa kwenye halmashauri yanatakiwa kusajiliwa na kutangazwa kwenye Gazeti la Serikali.
Waziri Ndaki ameyasema hayo leo (26.06.2022)
kwenye mkutano wa hadhara na wafugaji uliofanyika kwenye Kijiji cha Kongwa
wilayani Morogoro ambapo aliwaeleza wafugaji hao kuwa halmashauri zikishatenga
maeneo kwa ajili ya malisho zinatakiwa kuyawasilisha kwenye Wizara ya Mifugo na
Uvuvi ili yasajiliwe na kutangazwa kwenye gazeti la serikali.
"Halmashauri zinatakiwa mara baada ya
kutenga maeneo ya malisho katika vijiji, zinatakiwa kuyawasilisha maeneo hayo Wizarani
ili yasajiliwe na kutangazwa kwenye gazeti la serikali, kwa kufanya hivyo
itakuwa ni vigumu mtu kubadilisha matumizi ya maeneo hayo kwa kuwa yatakuwa
yanalindwa kisheria," alisema
Waziri Ndaki amewataka wafugaji hao kupanda
malisho kwenye maeneo ambayo tayari yameshatengwa kwa ajili ya malisho badala
ya kutegemea malisho ya asili peke yake. Wizara inaendelea kutoa elimu na
kuhamasisha wafugaji kupanda malisho ili kuweza kukabiliana na tatizo la
upungufu wa malisho hasa kipindi cha kiangazi.
Wafugaji wametakiwa kuacha tabia ya
kuwakaribisha wafugaji kutoka maeneo mengine kuja kulisha mifugo kwenye maeneo
yao kutokana na uchache wa malisho katika maeneo waliyopo. Hivyo pindi
wanapowakaribisha wafugaji kutoka nje malisho katika maeneo hayo humalizika kwa
haraka na kusababisha mifugo kuanza kufa kwa kukosa malisho.
Vilevile wafugaji hao wametakiwa kuanza kufanya
tathmini ya kiasi cha mifugo waliyonayo na kiasi cha malisho kilichopo mpaka
kuelekea msimu wa mvua kuanza. Wafugaji wametakiwa endapo wataona mifugo ni
mingi kuliko malisho yaliyopo, kuanza kuvuna mifugo hiyo na kubakiza kiasi cha
mifugo kitakachoendana na malicho yaliyopo badala ya kusubiri mifugo ikabiliane
na kiangazi kikali ianze kufa ndipo waiuze kwa bei ya hasara kwa kuwa mifugo
afya yake haitakuwa nzuri.
Waziri Ndaki pia amewaahidi wafugaji kwenye Jimbo la Morogoro
Kusini kuwa Wizara itawajengea Malambo matatu na Majosho tatu, hii ni baada ya
kusikiliza changamoto zinazowakabili wafugaji zilizowasilishwa na Katibu wa
Chama cha Wafugaji wakati anawasilisha taarifa yake.
Naye Mbunge wa Jimbo la Morogoro Kusini, Mhe.
Innocent Kalogeris amesema kuwa kwa sasa upo umuhimu wa kuupitia upya mpango wa
matumizi bora ya ardhi kwenye vijiji kwa kuwa lipo ongezeko kubwa la wafugaji
na wakulima ili mpango huo uweze kwenda sawa na hali halisi ya sasa.
Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Albert Msonda
naye amesema kuwa serikali imeshafanya mambo mengi katika kutengeneza mazingira
mazuri ya kuwawezesha wafugaji, kinachotakiwa sasa ni kila mmoja kuhakikisha
anatimiza wajibu wake na wafugaji kufuata maelekezo / ushauri wanaopewa na
wataalam.
Aidha, amesema kuwa zipo changamoto ambazo
zinatakiwa kutatuliwa kwenye ngazi ya Kijiji, Kata na Wilaya ambazo hazihitaji
ngazi ya Wizara, hivyo atawasimamia wahusika ili kuhakikisha changamoto hizo
zinatatuliwa kwenye ngazi hizo.
Katika ziara yake Wilayani Morogoro, Waziri
Ndaki pia alifanya mkutano wa hadhara na wafugaji katika Jimbo la Morogoro
Kusini Mashariki ambapo aliwasihi wafugaji hao kushiriki kwenye zoezi la Sensa
ya Watu na Makazi kwa kuwa ni muhimu kwa mipango ya maendeleo ya nchi.
Pia aliendelea kuwahamasisha wafugaji kuhakikisha wanavalisha mifugo yao hereni za utambuzi zoezi ambalo linaendelea ambalo nalo lina faida kubwa katika kukuza Sekta ya Mifugo. Waziri Ndaki pia amewaahidi wafugaji wa Jimbo hilo kuwa Wizara itawajengea Majosho matatu.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki akizungumza na wafugaji wa Kata ya Mvua kwenye Kijiji cha Kongwa wilayani Morogoro ambapo amewataka wafugaji hao kuanza kulima malisho katika maeneo yao na kutunza nyanda za malisho zilizopo, vilevile kutojihusisha na migogoro ya aina yoyote katika jamii wanazoishi. (26.06.2022)
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (kulia)
akimkabidhi Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Albert Msando (kushoto) kadi ya
uanachama wa Chama cha Wafugaji wakati wa mkutano wa hadhara na wafugaji
uliofanyika kwenye Kijiji cha Kongwa wilayani Morogoro. (26.06.2022)
Baadhi ya wafugaji wa Kata ya Mvua wakimsikiliza Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (hayupo pichani) wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Kijiji cha Kongwa wilayani Morogoro. (26.06.2022)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni