Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki amekabidhi injini za boti kwa ajili ya wavuvi katika Halmashauri za Wilaya za Pangani, Mtwara Mjini na Iringa.
Akizungumza kabla ya kukabidhi injini hizo leo
(24.06.2022) Waziri Ndaki alisema kuwa Wizara imeendelea na utaratibu wake wa
kuwawezesha wavuvi kwa kuwapatia vifaa vinakavyowasaidia kuongeza uwezo wa
kuvua mazao ya uvuvi kwa wingi ili kuongeza uzalishaji wa mazao ya uvuvi hapa
nchini.
“Injini za Boti tunazozikabidhi leo zina uwezo
wa nguvu ya farasi 15 na tunazitoa kwenye Halmashauri za Wilaya za Pangani,
Mtwara Mjini na Iringa ambapo kila Halmashauri itapata injini moja kwa ajili ya
kuwawezesha wavuvi kuongeza uwezo wao wa kuvua lakini pia kulinda rasilimali za
uvuvi,” alisema
Waziri Ndaki amewasihi wavuvi kuhakikisha
wanavitunza vifaa wanavyopatiwa na Wizara pamoja na Wadau wengine wa uvuvi na
kuhakikisha wanavitumia kwa matumizi yaliyokusudiwa ikiwa ni pamoja na ulinzi
wa rasilimali za uvuvi.
Aidha, Waziri Ndaki amesema kuwa Serikali
kupitia Wizara imejipanga kununua injini nyingine 250 za boti katika mwaka wa
fedha wa 2022/2023 na kama kutakuwa na uwezakano zinaweza kuongezeka injini 70
zaidi ambapo kutakuwa na jumla ya injini 320.
Lengo ni kuhakikisha uzalishaji wa mazao ya
uvuvi unaongezeka na mchango wake katika kukuza kipato cha mvuvi na taifa kwa
ujumla kinaongezeka. Kwa kufanya hivyo lengo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan litakuwa limetimia kwa kuhakikisha kipato
cha wavuvi kinaongezeka na mchango wa uvuvi kwenye pato la taifa unaongezeka.
Vilevile Waziri Ndaki amesema kuwa injini hizo
zitakazo nunuliwa zitatolewa kwenye vyama vya ushiriki vya wavuvi na hata kwa
mvuvi mmoja mmoja mwenye uwezo kwa kuwa zitakuwa zikikopeshwa kwa riba ndogo
sana ambayo haitawaumiza wavuvi.
Naye Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso
akizungumza baada ya kupokea injini moja ya boti kwa niaba ya wananchi wa
Pangani ameishukuru Wizara kwa kuwapatia injini hiyo na kwamba itakwenda kuwa
msaada mkubwa kwa wavuvi katika shughuli zao za uvuvi ikiwa ni pamoja na ulinzi
wa rasilimaliza uvuvi. Lakini pia ameishukuru wizara kwa kuamua kujenga soko la
samaki Pangani na kwamba wanapangani wataendelea kutoa ushirikiano kwa Wizara.
Mbunge wa Mtwara Mjini, Mhe. Hassan Mtenga
licha ya kuishukuru Wizara kwa kuwakabidhi injini ya boti, ameiomba Wizara kuendelea
kuwawezesha wavuvi kwenye vifaa vingine vya uvuvi ikiwemo majokofu ya
kuhifadhia mazao ya uvuvi.
Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb) akiipongeza Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Sekta ya Uvuvi) kwa kuipatia Jimbo lake la Pangani Injini moja ya Boti yenye uwezo wa nguvu ya farasi 15 kwa kuwa itakwenda kuwasaidia wavuvi katika shughuli zao za uvuvi lakini pia katika kulinda rasilimali za uvuvi. Hafla hii imefanyika kwenye ofisi ndogo za Wizara zilizopo kwenye jengo la Benki ya NBC Jijini Dodoma. (24.06.2022)
Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti, Mafunzo na Ugani kutoka Sekta ya Uvuvi, Prof. Mohammed Sheikh akielezea uwezo wa Injini tatu za Boti ambazo zina uwezo wa nguvu ya farasi 15 wakati wa hafla ya kukabidhi injini hizo. Lakini pia alisema kuwa mpaka sasa Wizara imeshanunua jumla ya injini za boti 26. Hafla hii imefanyika kwenye ofisi ndogo za Wizara zilizopo kwenye jengo la Benki ya NBC Jijini Dodoma. (24.06.2022)
Mbunge wa Kalenga, Mhe. Jackson Kiswaga (Mb) akiipongeza
Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Sekta ya Uvuvi) kwa kuipatia Jimbo lake la
Pangani Injini moja ya Boti yenye uwezo wa nguvu ya farasi 15 wakati wa
hafla ya kukabidhi kwa kuwa itakwenda kuwasaidia wavuvi katika shughuli zao za
uvuvi lakini pia katika kulinda rasilimali za uvuvi. Hafla hii imefanyika
kwenye ofisi ndogo za Wizara zilizopo kwenye jengo la Benki ya NBC Jijini
Dodoma. (24.06.2022)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni