Nav bar

Ijumaa, 24 Juni 2022

KAMATI YA BUNGE YA KILIMO MIFUGO NA MAJI YAITAKA NAIC KUTOA ELIMU NA UHAMASISHAJI WA UHIMILISHAJI MBEGU BORA ZA MIFUGO

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji, Dkt. Christine Ishengoma amekitaka Kituo cha Taifa cha Uhimilishaji (NAIC) kutoa elimu na uhamasishaji juu ya umuhimu na faida za kufanya uhimilishaji ili kuweza kupata mifugo na mazao bora ya mifugo.

Maelekezo hayo yametolewa leo Juni 18, 2022 wakati wa ziara ya kamati hiyo iliyotembelea kituo hicho pamoja na Chuo cha Mafunzo ya Mifugo Kampasi ya Tengeru mkoani Arusha ambapo walisema kuwa pamoja na kituo hicho kuwa cha muda mrefu na kuwa na matawi katika Kanda mbalimbali bado mwamko wa wafugaji katika kufanya uhimilishaji ni mdogo kutoka na wafugaji kukosa elimu sahihi juu ya suala hilo.

Dkt. Ishengoma alisema kuwa kamati wametembelea na wameona teknolojia ya hali ya juu na yenye manufaa kwa wafugaji iliyopo katika kituo hicho lakini changamoto iliyopo ni mwitikio mdogo wa wafugaji katika kutumia teknolojia hiyo.

“Tumeona kuanzia ukusanyaji wa mbegu na jinsi zinavyofanyiwa vipimo lakini pia tumeelezwa kila dume na aina ya mbegu yake ambapo sasa kinachotakiwa ni elimu na uhamasishaji kwa wafugaji ilib waweze kuitikia jambo hili la uhimilishaji na kuweze kubadilisha na kuboresha mifugo yao na kuboresha mazao yao,” alisema Dkt. Ishengoma.

Mbunge wa Moshi Vijiji, Profesa Patrick Ndakidemi alisema kuwa hali ni mbaya kwa wafugaji katika majimbo yao hivyo kwa mbegu walizoziona katika kituo hicho ni vema wagani wakawafikia wafugaji na kuwapa elimu juu ya teknolojia hiyo  ili waweze kuboresha mifugo yao.

“Kusema ukweli hali ni mbaya huko kuna maeneo mengine ambayo hawataamini kuwa tuna kitu kikubwa hivi ambacho kinaweza kutoa huduma nchi nzima kwahiyo langu kubwa na muomba Mhe. Waziri na timu yake ya wataalamu kuboresha shughuli za ugani juu ya uhimishaji ili iweze kuwafikia wafugaji huko waliko, tuweze kuboresha wale Ng'ombe wa kienyeji kwani bila ugani mambo hayataenda vizuri,” alisema Profesa Ndakidemi.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega alisema kuwa pamoja na kuwa na mifugo wengi nchini lakini kuna wakati viwanda vinakosa usambazaji hivyo wizara kwa sasa ina mpango wa kwenda kuzungumza na wafugaji ili waipokee teknolojia hiyo ya uhimilishaji lakini pia kutoa mafunzo wa wataalam wa mifugo ili waweze kazi ya uhimilishaji iweze kufanyika kwa kuzingatia utaalam.

“Lakini pia tutaviongezea vituo hivi nguvu ili kuweza kuboresha zaidi kwasababu vimechoka lakini pia kuendelea kufanya tafiti za kina ili kuweza kupata matokeo mazuri zaidi kulingana na aina ya Ng'ombe lengo likiwa ni kuboresha mifugo yetu hapa nchini lakini pia na vipato vya wafugaji,” Alisema Ulega.

Vilevile Wizara kupitia kupitia Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo hapa nchini imepanga kutoa mafunzo ili wahitimu katika vyuo hivyo waweze kujiajiri kwenye ufugaji na sio kutegemea kuajiriwa. wajasiriamali wa mifugo na uvuvi lakini pia

Awali akisoma taarifa Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha Taifa cha Uhimilishaji (NAIC), Dkt. Dafay Bura alisema kuwa lengo la kuanzishwa kwa huduma ya uhimishaji ni kusambaza mbegu bora zitakazoweza kuongeza uzalishaji wa nyama na maziwa ili kuinua pato la mfugaji na taifa kwa ujumla pamoja na kuimarisha lishe.

Dkt Bura alisema uhimilishaji huo unasaidia kuongeza uzalishaji wa Ng'ombe wa kisasa, kuinua kiwango cha Ng'ombe wa asili pamoja na kuokoa fedha za kigeni ambazo zingetumika kuagiza nje ya nchi mazao yatokanayo na mifugo kama vile nyama na maziwa.

“Uhimilishaji huu una faida nyingi mojawapo ni kuzuia kuenea kwa magonjwa ya vizazi, kupunguza gharama za kutunza madume, kuepukana na hatari za madume kujeruhiwa, kupata ndama wengi kutoka kwa dume bora, kutumia mbegu za dume bora kwa muda mrefu hata kama amevunjika au amekwisha kufa pamoja na kuwa na wigo mpana wa aina ya mbegu unayohitaji,” Alisema Dkt Bura.

“Tuna jumla ya madume ya Ng'ombe 33 ambapo kutokana na takwimu za Ng'ombe nchini kuwa kubwa wizara kwa kushirikiana na kituo hiki tuanendelea na uhamasishaji wa shughuli za uhimilishaji  kupitia programu maalum ya jambo ya uhimilishaji katika halmashauri mbalimbali na kwa mwaka wa fedha 2021/2022 zaidi ya Ng'ombe 3000 walihimishwa bure ikiwemo wilaya ya Ngorongoro, Pangani, Muweza, Lushoto na Mkinga lakini pia bado tunakabiliwa na changamoto ya mwitikio mdogo wa wafugaji hivyo tunahitaji kufanya kazi zaidi ili kukuza uelewa kuhusu manufaa ya uhimishaji,” Alisema.

Naye mtendaji mkuu wa wakala wa mafunzo ya mifugo (LITA), Dkt. Pius Mwambele akisoma taarifa ya chuo hicho alisema kuwa chuo kina wajibu wa kuchangia upatikanaji wa wataalamu wa mifugo nchini kwani waliopo ni 3800 huku mahitaji yakiwa ni 17,400 lakini pia kuwezesha umahiri wa ujasiriamali kwa vijana ili waweze kujiajiri pamoja na kuongeza upatikanaji wa mbegu na bidhaa bora za mifugo kwa ajili ya kuwahudumia jamii ya watanzania.


“Mafanikio tuliyonayo ni pamoja na kuongezeka kwa udahili kutoka 798 mwaka 2012/2013 hadi kufikia 3,972 ya mwaka 2021/2022 pamoja na kuongezeka kwa mapato ya ndani kutoka bilioni 3 hadi bilioni 4.7 lakini pia tunakabiliwa na changamoto miundombinu mibovu ya madarasa na mabweni kutokana na uchakavu,” alisema Dkt Mwambele.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji, Mhe. Dkt. Christine Ishengoma (Mb) akiwasalimu Viongozi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi pamoja na Mkoa wa Arusha mara baada ya kufika kwenye Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kwa ajili ya kusaini kitabu cha wageni. Kulia kwake ni Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega na kushoto kwake ni Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Mhe. Mhandisi Richard Ruyango. Kushoto ni Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Dkt. Charles Mhina. (18.06.2022)

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega (Mb) akizungumza kwenye kikao kifupi na Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji wakati kamati hiyo ilipotembelea Chuo cha Mafunzo ya Mifugo Kampasi ya Tengeru ambapo amewaeleza wajumbe hao kuwa Serikali imepanga kutoa mafunzo yatakayowasaidia wahitimu kwenda kujiajiri na sio kutegemea kuajiriwa. Kushoto kwake ni Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Dkt. Christine Ishengoma (Mb) na kulia ni Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Dkt. Charles Mhina. (18.06.2022)


Wataalam kutoka Kituo cha Taifa cha Uhimilishaji (NAIC) wakitoa maelezo juu ya namna kituo hicho kinavyofanya kazi kwa Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji wakati kamati hiyo ilipotembelea kituoni hapo kwa lengo la kuona namna kinavyofanya kazi. (18.06.2022)


Viongozi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi na Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji wakifuatilia maelekezo yaliyokuwa yanatolewa na wataalam wa Kituo cha Taifa cha Uhimilishaji (hawapo pichani) wakati kamati hiyo ilipoingia kwenye maabara ya iliyopo hapo kituoni kwa lengo la kuona jinsi maabara hiyo inavyofanya kazi. (18.06.2022)


Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo (LITA), Dkt. Pius Mwambene (kushoto) akitoa maelezo kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji wakati kamati hiyo ilipotembelea Kumbi za Mihadhara zilizojengwa kwenye Chuo cha Mafunzo ya Mifugo Kampasi ya Tengeru. (18.06.2022)

Viongozi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi na Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji wakimsikiliza Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo (LITA), Dkt. Pius Mwambene (kushoto) wakati kamati hiyo ilipotembelea maabara zilizopo kwenye Chuo cha Mafunzo ya Mifugo Kampasi ya Tengeru. (18.06.2022)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni