Nav bar

Ijumaa, 24 Juni 2022

VIJANA KUWEZESHWA UFUGAJI KIBIASHARA

Na Mbaraka Kambona,


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega ameitaka taasisi ya Utafiti wa Mifugo(TALIRI) na taasisi inayoshughulika na kilimo biashara(PASS) kupitia mradi wanaoutekeleza wa  kunenepesha mbuzi kuhakikisha vijana wengi wanapata ujuzi huo ili waweze kuwa na fursa pana ya ajira na kukuza uchumi wao .


Ulega alitoa maelekezo hayo katika kikao kazi cha kupata taarifa ya utekelezaji wa mradi wa kunenepesha mbuzi unaotekelezwa kwa ushirikiano na taasisi hizo mbili kilichofanyika jijini Dodoma Juni 22, 2022.


Alisema mradi huo ni lazima ujikite katika kuwasaidia vijana wengi kupata ujuzi wa kufuga kibiashara na kuwawekea mfumo mzuri utakaowasaidia kuwezeshwa kifedha ili wawe na mitaji ya kutosha kuendesha biashara ya mifugo.


“Tunataka tutoe ajira kwa vijana, hivyo ni lazima kuwatengeneza vijana wengi watakaokuwa na ujuzi wa kunenepesha mifugo, sasa hivi wanaofanya unenepeshaji wapo na wanawezeshwa na benki zetu, lakini tunataka tupate vijana wengi zaidi watakaotengenezwa kupitia mradi huu, tukiweka nguvu yetu hapo vizuri naamini tutawezesha vijana wengi kujiajiri,”alisema


Aidha, aliongeza kwa kusema kuwa sasa sekta ya mifugo inakabiliwa na changamoto kubwa ya malisho  hivyo ni muhimu wakajikita katika kuzalisha malisho ili mifugo iwe na malisho ya kutosha wakati wote jambo litakalopelekea mifugo hiyo kuwa na uzito wenye thamani sokoni.


"Katika taarifa zenu nimewasikia hapa mmeeleza mambo mengi mnayotarajia kufanya kupitia mradi mnaotekeleza, ushauri wangu ni muhimu mkachagua mambo machache mtakayoweza kutekeleza vizuri awamu kwa awamu kuliko kubeba mambo mengi na mwisho wa siku msiweze kufikia malengo," alisema Ulega


Kufuatia changamoto ya kufa kwa mifugo iliyoikumba nchi hivi karibuni aliwataka wao kama Wataalamu kuhakikisha wanatumia taaluma zao kikamilifu ili kupunguza vifo vya mifugo nchini.


Halikadhalika aliitaka Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) kusaidia wadau hao wa sekta ya mifugo kwa kuandaa mipango mizuri ya biashara na kutoa mikopo nafuu kwa wafugaji ili waweze kufanya ufugaji wenye tija. 


Naye, Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti, Mafunzo na Ugani, Dkt. Angelo Mwilawa alisema kuwa kwa muda sasa viwanda vingi vya kuchakata nyama hapa nchini vimekuwa vikifanya kazi chini ya uwezo wake hivyo kupitia mradi huo unaotekelezwa na TALIRI kwa kushirikiana na PASS ukisimamiwa vizuri utakwenda kuwa sehemu ya utatuzi wa changamoto hiyo.


Aliongeza kwa kusema kuwa mradi huo pia utashirikisha Halmashauri nchini ili vijana waliopo katika maeneo hayoo waweze kushirikishwa vizuri katika kujifunza unenepeshaji wa mifugo na kuboresha maisha yao.


Mradi  huo wa kunenepesha mbuzi umeanzishwa mahsusi kwa lengo la kuwaanda na kuwawezesha vijana kushiriki mafunzo ya ujasiriamali kwa vitendo ili hatimaye kuwekeza kwenye ufugaji kibiashara na kuongeza fursa za ajira kupitia sekta ya mifugo nchini.



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni