Wizara ya Mifugo na Uvuvi imetoa vifaranga vya kuku 3060 kwa vikundi vya wanawake Wilayani Ruangwa Mkoani Lindi ikiwa ni katika utekelezaji wa sera ya kuwakwamua wananchi kiuchumi.
Akizungumza wakati wa kukabidhi vifaranga hivyo Februari 9, 2022 kwa vikundi vya kina mama, Mkurugenzi Msaidizi wa Utafiti na Mafunzo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt Hassan Mruttu alisema mradi huo wa ufugaji kuku utakuwa wa shamba darasa.
Alisema Wizara iliona ni vyema kuanza kutoa kuku kwa vikundi viwili (2) cha Alonga na Kichawana kama shamba darasa ambapo baada ya wiki 4 watatakiwa kusambaza katika vikundi vingine ili navyo viweze kufuga.
"Sisi kama Wizara tunatekeleza ilani ya CCM tukiwa chini ya Rais wetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ambaye ni mbunge wa hapa kwa hiyo katika kubuni namna ya kumkwamua mwanachi tukasema hatuwezi kumfikia mtu mmoja bali kwa kuanzisha mashamba darasa ambapo vikundi vinakuwa vikijifunza na baada ya wiki nne vinapatiwa kuku kama mtaji wao" alisema
Akitoa shukrani kwa niaba ya ofisi ya Mbunge wa jimbo la Ruangwa, Msaidizi wa Waziri jimboni, Bw. Ramadhani Matola alisema wanaishukuru Wizara kwa kuendelea kutekeleza vyema ilani ya CCM ambayo kwa asilimia kubwa inalenga kumkwamua mwananchi wa chini.
Alisema kwa kupatiwa kuku hao kutawasaidia wananchi wa jimbo hilo kuondokana na umasikini kwa kufuga kisasa na kibiashara ambapo wataweza kuinua kipato chao na taifa kwa ujumla.
Kampuni ya AKM GLITTER ndio iliyopewa dhamana na Serikali ya kuzalisha na kusambaza kuku hao katika wilaya ya Ruangwa ambapo wameahidi kutekeleza zoezi hilo kwa ufanisi na kuhakikisha kila kikundi tarajiwa kinanufaika na mradi huo.
Kupitia Afisa Mifugo wa kampuni hiyo Bw.Hamim Dauri alisema kampuni inaamini kupitia vikundi vya kina mama na vijana wakiwezeshwa kufuga mifugo midogo kama kuku wanaweza kuinua maisha yao kwasababu hawatumii gharama kubwa katika ukuzaji
"Tunashukuru Serikali kutuamini na tunaahidi kufanya kazi kwa umakini kuhakikisha malengo ya Serikali yanafikiwa kwa sababu tunaamini katika ufugaji wa kibiashara na pia tunaamini tukimuwezesha kijana au mama kufuga mifugo midogo itamuondolea umasikini" alisema
Kwa upande wa baadhi ya wanakikundi ambao ndio wanufaika walisema wanatambua kuwa dhamana waliyopewa ni kubwa kwa kuanza na shamba darasa hilo kwani vikundi vingine vinategemea kupata kuku kutoka kwao.
Mkurugenzi Msaidizi wa Utafiti na Mafunzo kutoka Wizara ya
Mifugo na Uvuvi Dkt. Hassan Mruttu akiongea na akina mama wa kikundi cha
Kichawana mara baada ya kukabidhiwa vifaranga vya kuku na kuwasihi kuvitunza
vifaranga hivyo kwani ni mtaji utakao wasaidia kujikwamua kiuchumi Februari 09,
2022 Ruangwa Mkoani Lindi.
Msaidizi wa Mhe. Waziri Mkuu jimboni Bw. Ramadhani Matola
akikabidhi vifaranga vya kuku kwenye shamba darasa litakalo simamiwa na kikundi
cha akina mama cha Alonga Ruangwa Mkoani Lindi, Februari 09,2022.
Mkurugenzi Msaidizi wa Utafiti na Mafunzo kutoka Wizara ya
Mifugo na Uvuvi, Dkt. Hassan Mruttu (wa tano kutoka kushoto) akiwa kwenye picha
ya pamoja na akina mama wa kikundi cha Alonga, maafisa Mifugo na Msaidizi wa
Waziri wa Ruangwa mara baada ya kukabidhi vifaranga vya kuku kwa wanakikundi
hao. Februari 09, 2022.