Na Mbaraka Kambona, Mwanza
Waziri wa Mifugo na uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki amewaagiza Watendaji wa wizara hiyo kwa kushirikiana na Watendaji wa Halmashauri kote nchini kuhakikisha wafanyabiashara wanaotoka nje ya nchi wananunua mazao ya uvuvi katika masoko yaliyopangwa na serikali na sio kwenye mialo kama baadhi yao wanavyofanya sasa ili kuepuka kupoteza mapato ya serikali yatokanayo na mazao hayo.
Waziri Ndaki alitoa agizo hilo wakati alipofanya kikao kilichohusisha watendaji wa wizara ya mifugo na uvuvi (sekta ya uvuvi), wafanyabiashara na wadau wa sekta hiyo kutoka halmashauri ya jiji la Mwanza Februari 2, 2022.
Alitoa agizo hilo baada ya wafanyabiashara wanaofanya shughuli zao katika soko la Kimataifa la Kirumba kumweleza kuwa wapo baadhi ya wafanyabiashara kutoka mataifa ya jirani ambao wananunua mazao ya uvuvi katika mialo badala ya kwenda sokoni na kusababisha serikali kukosa mapato.
“Kama kuna wafanyabiashara kutoka nje ya nchi wanakwenda kununua mazao ya uvuvi huko visiwani, hao wanatenda makosa, wanapaswa wakamatwe na wafunguliwe mashitaka, naomba mamlaka husika kuanza kufuatilia malalamiko hayo ili kukomesha upotevu wa mapato,” alisema Mhe. Ndaki
Aidha, alitumia nafasi hiyo pia kusema kuwa kama kuna baadhi ya viongozi na watendaji wa serikali wanashirikiana na wafanyabiashara hao nao watafuatiliwa na kupelekwa kwa mamlaka zao husika ili wachukuliwe hatua.
Awali, akizungumza katika kikao hicho, Mwenyekiti wa Soko la Kimataifa la Kirumba lililopo jijini Mwanza, Fikiri Magafu alimweleza Waziri Ndaki kuwa kuna wafanyabiashara wengi kutoka nchi jirani wanaokwenda katika visiwa vilivyopo ndani ya Ziwa Viktoria na kununua mazao hayo bila kufuata utaratibu jambo ambalo linafanya wao kuwa na wakati mgumu wa kibiashara.
Katika hatua nyingine, wafanyabiashara hao waliiomba serikali kurekebisha baadhi ya tozo na kuangalia upya utoaji wa leseni za biashara kwa wafanyabiashara wa ndani na wa nje ili kuwajengea mazingira mazuri ya kulipa kodi kwa serikali jambo ambalo Waziri Ndaki alisema wamepokea maombi hayo huku akiahidi kuwa wao kama wizara kwa kushirikiana na watendaji wa halmashauri watapitia upya kodi na tozo zilizopo kwa mujibu wa sheria na kuzirekebisha ili kuwawezesha wafanyabiashara kufanya shughuli zao kwa tija.
Waziri wa
Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki akiongea na Wafanyabiashara wa mazao ya
uvuvi wanaofanya shughuli zao Mkoani Mwanza katika Mkutano wa kusikiliza kero
za Wafanyabiashara hao kilichofanyika mkoani mwanza Februari 2, 2022. Baada
ya kusikiliza kero zao alizitolea maelekezo huku akiahidi kuwa watapitia upya
kodi na tozo na kurekebisha zile zinazoonekana kuwa kikwazo ili kuwawezesha
wafanyabiashara kufanya shughuli zao kwa tija.
Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid
Tamatamah (kulia) akitoa neno la utangulizi wakati akiongea na Wafanyabiashara
wa Mazao ya Uvuvi wanaofanya shughuli zao Mkoani Mwanza katika Mkutano wa
kusikiliza kero za Wafanyabiashara hao kilichofanyika mkoani mwanza Februari 2, 2022.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni