Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi, upande wa sekta ya Mifugo imebainisha mikakati iliyoiweka ili kukabiliana na athari za ukame ulioiathiri mifugo katika maeneo mbalimbali hapa nchini.
Hayo yamesemwa na Kaimu Mkurugenzi wa Sera na Mipango kwa upande wa sekta hiyo, Mbaraka Stambuli wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji ya robo mwaka mbele ya kamati ya kudumu ya Kilimo, Mifugo na Maji kwenye kikao kilichofanyika (02.02.2022) kwenye moja ya Kumbi za Bunge jijini Dodoma.
“Mhe. Mwenyekiti moja ya mikakati tuliyoiweka kama Wizara ni kupeleka lita 2906 za dawa ili kuua kupe na mbung’o katika Halmashauri zilizoathirika zaidi lakini pia Wizara inajenga majosho 32 yenye thamani ya shilingi milioni 500 ili kuchochea uogeshaji kwa lengo la kudhibiti magonjwa kwenye maeneo yaliyoathirika zaidi” Amesema Stambuli.
Stambuli amebainisha mkakati mwingine kuwa ni pamoja na Wizara yake kushirikiana na Wizara ya Maji kuchimba visima virefu 6 katika Wilaya za Simanjiro, Same, Kibaha, Chalinze na Morogoro pamoja na miundombinu yake ambavyo vyote kwa pamoja vina thamani ya shilingi bilioni 1 jambo ambalo litapunguza hali ya ukame kwa kiasi kikubwa.
“Lakini pia mkakati wa muda wa kati utakaoanza mwaka ujao wa fedha, Wizara itatenga fedha kwa ajili ya uanzishaji wa miundombinu ya maji, majosho na malisho ya mifugo katika maeneo yaliyoathiriwa zaidi na ukame wa mwaka huu” Amesema Stambuli.
Akichangia suala hilo, Mbunge wa Viti maalum kutoka mkoa wa Manyara Mhe. Yustina Rahhi amewashauri wafugaji kote nchini kuanza kufuga kisasa kwa kuzingatia maeneo na malisho yaliyopo badala ya kufuga mifugo mingi bila kuzingatia hali ya upatikanaji wa maji na malisho.
“Mhe. Mwenyekiti ni wakati sasa kwa wafugaji kuachana na ufugaji usio na tija kwa sababu unakuwa na ng’ombe 1000 au 2000 afu mwisho wa siku idadi kubwa wanakufa kwa kukosa malisho na maji na unakuta hata hao wanaobaki ukienda kupima uzito wao wanaishia kwenye kilo 100” Amesema Mhe. Rahhi.
Akizungumzia yale ambayo kamati imeyaona kupitia taarifa waliyowasilishiwa kwa upande wa Sekta ya Mifugo, Mwenyekiti wa kamati hiyo Mhe. Christine Ishengoma amesema kuwa kamati yake inatambua namna changamoto ya ufinyu wa bajeti inavyokwamisha utekelezaji wa shughuli mbalimbali za sekta hiyo ambapo ameahidi kuifanyia kazi changamoto hiyo.
“Lakini pia nitoe rai kwa Wataalam wote wa Sekta ya Mifugo kuendelea kutumia kiasi cha fedha mnacholetewa kutekeleza zaidi maeneo ya vipaumbele ili kupunguza changamoto za wafugaji zilizopo hivi sasa” Amesema Mhe. Ishengoma.
Akitoa neno la shukrani kwa wajumbe wa kamati hiyo, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega ameahidi kufanyia kazi maoni na ushauri uliotolewa na wajumbe wa kamati hiyo ambapo ameihakikishia kamati hiyo kushirikiana na wataalam wake katika kuhakikisha wanaendelea kushughulikia changamoto zinazowakabili wafugaji nchini.
Kikao cha kamati hiyo kitaendelea tena kesho (03.02.2021) ambapo sekta ya Uvuvi itawasilisha taarifa yake ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali zinazohusu sekta hiyo.
Kaimu Mkurugenzi wa Sera na Mipango (Mifugo) Bw. Mbaraka
Stambuli (kulia) akiwasilisha taarifa ya utekelezaji ya Wizara ya Mifugo na
Uvuvi (Mifugo) kwa wajumbe wa Kamati ya kudumu ya Kilimo, Mifugo na Maji wakati
wa kikao cha kamati hiyo kilichofanyika (02.02.2022) kwenye moja ya kumbi za Bunge
jijini Dodoma.
Baadhi ya wajumbe wa kamati ya kudumu ya Bunge ya Kilimo,
Mifugo na Maji wakifuatilia uwasilishaji wa taarifa ya utekelezaji ya Wizara ya
Mifugo na Uvuvi (Mifugo) iliyowasilishwa na Kaimu Mkurugenzi wa Sera na Mipango
(Mifugo) Bw.Mbaraka Stambuli (hayupo pichani) wakati wa kikao cha kamati hiyo
kilichofanyika (02.02.2022) kwenye
moja ya kumbi za Bunge jijini Dodoma.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni