Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeweka mikakati endelevu ya kuhakikisha inazalisha kwa wingi vifaranga vya samaki na kutoa elimu juu ya ufugaji wa samaki kwa wananchi ili kuongeza tija na kipato kwa Wafugaji na Taifa kwa ujumla.
Mkurugenzi wa Ukuzaji Viumbe Maji wa Wizara hiyo , Dkt. Nazael Madalla alisema hayo Februari 1,2022 katika mafunzo rejea kwa maofisa ugani wa halmashauri za mikoa ya Dar es Salaam, Tanga , Arusha , Pwani na Kilimanjaro yanayofanyika Mkoani Morogoro.
Dkt. Madalla alisema mafunzo hayo yamelenga kuhamasisha, kuendeleza , kusimamia tasnia ya ukuzaji viumbe maji nchini na kuzalisha kwa tija .
Aliendelea kusema kuwa vituo vinavyozalisha vifaranga wa samaki kwa Sasa ni vitatu ambavyo ni Ruhila kilichopo mkoa wa Ruvuma, Mwamapuli mkoani Tabora, na Kingolwira Morogoro.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo, mwaka 2020/2021 vituo hivyo vitatu viliwezakuzalisha jumla ya vifaranga vya samaki 1,901,717.
“Uzalishaji wa vifaranga vya Samaki katika vituo hivyo ni kama ifuatavyo, Kituo cha Ruhila kilizalisha vifaranga 972,305, Mwamapuli vifaranga 457,812 na cha hapa Kingolwira vifaranga 471,600 ", alisema Dk Madalla.
Aliongeza kwa kusema kuwa wizara imejipanga kuhakikisha ufugaji wa samaki unakuwa endelevu na wenye tija kwa wafugaji.
“kuanzishwa kwa vituo hivyo vya ukuzaji viumbe maji unakwenda sambamba na utoaji elimu sahihi ya ufugaji wa samaki pamoja na uzalishaji vifaranga vya Samaki", alifafanua
Aidha, aliwahimiza Watanzania kujitokeza kufuga samaki na viumbe maji wengine ili kujiongezea kipato chao na Taifa kwa ujumla.
Pamoja na hayo alitumia fursa hiyo kuwahimiza wananchi kupenda kula samaki na dagaa kwa wingi akisema kuwa madini mengi yanayopatikana ndani yake yanasaidia katika kupambana na magonjwa kwenye mwili wa binadamu.
Naye Katibu Tawala Msaidizi, Uchumi na Uzalishaji Mali Mkoa wa Morogoro, Dkt. Rozalia Rwegasira akisoma hotuba ya Katibu Tawala wa Mkoa huo, Mariam Mtunguja alisema kuwa wizara inatarajia kufikia lengo la mpango wa tatu wa maendeleo wa Taifa wa miaka mitano kwa kuzalisha tani 50,000 za mazao ya ukuzaji wa viumbe maji kwa mwaka ifikapo mwaka 2025/2026.
Hivyo aliwataka Watanzania kuchangamkia fursa zilizopo katika uchumi
wa bluu kutokana na kuwepo rasilimali maji ikiwemo bahari, maziwa, mito na
maeneo oevu ambayo yanatoa wigo mpana wa kufanya shughuli za ufugaji wa samaki
na viumbe wengine wa majini.
Dkt. Rwegasira aliongeza kuwa pamoja na Serikali kuwekeza nguvu kubwa katika sekta ya mifugo na uvuvi, bado kuna uzalishaji mdogo wa mazao ya viumbe maji ukilinganisha na fursa zilizopo nchini.
“Tasnia ya ukuzaji viumbe maji inakabiliwa na upungufu wa maofisa ugani 15,323 ambapo kwa sasa kuna maofisa ugani 677 ikilinganishwa na mahitaji ya maofisa ugani 16, 000” alisema Dk Rwegasira.
Dk Rwegasira aliwataka maofisa ugani waliopo kupeleka teknolojia walioipata kwa watanzania ili waweze kufuga samaki na viumbe maji wengine kwa njia ya kisasa zaidi ili kukidhi mahitaji ya soko la kimataifa kwani kwa sasa kuna uhitaji mkubwa wa kitoweo cha samaki.
Kwa upande wao washiriki wa mafuzo hayo Lucia Balilemwa pamoja na Emmanuel Ntobi kwa nyakati tofauti waliishukuru serikali kwa kuwapatia mafunzo rejea hayo na kwamba watayatumia kubadirisha maisha ya wananchi katika maeneo walikotoka juu ya ufugaji bora wa samaki na hivyo itapunguza changamoto ya uvuvi haramu.
Picha ya Pamoja ya Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Uchumi na
Uzalishaji (Morogoro), Dkt. Rozalia Rwegasila (katikati waliokaa) Mkurugenzi wa
Idara ya Ukuzaji Viumbe Maji, Dkt. Nazael Madalla (kushoto), Mkurugenzi
Msaidizi wa Ukuzaji Viumbe Maji Baridi, Dkt. Imani Kapinga (kulia) na Washiriki
wa Mafunzo Rejea ya Ukuzaji Viumbe Maji kutoka mikoa ya Dar es Salaam, Tanga,
Kilimanjaro na Pwani mara baada ya kufunguliwa kwa mafunzo hayo,yanayoendelea
katika kituo cha Kingolwira Mkoani Morogoro. (01.02.2022).*
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni