Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega
amelihakikishia bunge kuwa uchumi wa buluu kwa upande wa Tanzania bara
utatekelezwa katika eneo kubwa zaidi kutokana na kuamua kuutekeleza katika
vyanzo vyote vya maji vilivyopo nchini.
Mhe. Ulega ameyasema hayo wakati akijibu swali la mmoja wa wajumbe wa kamati ya kudumu ya bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji ambaye alitaka kufahamu namna uchumi wa buluu unavyotekelezwa kwa upande wa Tanzania bara wakati wa kikao cha kamati hiyo kilichofanyika (03.02.2022) kwenye moja ya kumbi za Bunge jijini Dodoma
Mhe. Ulega amesema kuwa upande wa Tanzania bara una vyanzo vingi zaidi vya maji ikilinganishwa na Zanzibar na tayari Wizara yake imeanza hatua ya awali ya utekelezaji wa dhana hiyo kwa vitendo kwa kuwaelimisha wavuvi juu ya fursa mbalimbali zilizopo kwenye mazao mbalimbali ya Uvuvi.
“Mhe. Mwenyekiti hivi karibuni nilikuwa mkoani Tanga nikiwaelimisha wananchi juu ya fursa mbalimbali zilizopo kwenye uchumi wa buluu kwa sababu uchumi huu hauishii tu kuvua kwenye vyanzo vya asilli bali zipo fursa pana zaidi ikiwemo ufugaji wa viumbe maji kwa upande wa baharini au maji ya ndani kama vile Ziwa Nyasa na vyanzo vingine” Amesema Mhe. Ulega
Mhe. Ulega amebainisha kuwa Uchumi wa buluu utawafanya wavuvi waliopo hapa nchini kujipatia kipato kikubwa zaidi ukilinganisha na kile wanachokipata kwa hivi sasa kwa sababu watapata fursa ya kujipatia fedha za kigeni kupitia mazao mbalimbali ya Uvuvi kama vile kaa, majongoo bahari, lulu na mwani.
“Leo ukimwambia mvuvi kuwa kuna fedha nyingi sana inapatikana kwenye samaki aina ya kaa anaweza asikuelewe lakini kwa hivi sasa kilo moja ya kaa inauzwa shilingi 25, 000 na kilo moja hiyo ni wastani wa kaa wawili tu tena ambao hawana gharama kwenye utunzaji wao kwa sababu unawaweka tu kwenye maji ya baharini na kila kitu wanakipata humu, kama utawawekea chakula basi ni kidogo sana” Amesisitiza Mhe. Ulega.
Mhe. Ulega amebainisha kuwa hatua inayofuata baada ya kuwaelimisha wananchi juu ya fursa zilizopo kwenye uchumi wa buluu ni kuandaa mikutano na warsha mbalimbali zitakazojumuisha wawekezaji wa ndani na nje ya nchi ili kuufungua uchumi huo kwa wadau hao wa sekta binafsi ambao aliwataja kama walengwa wakuu katika utekelezaji wa uchumi huo.
Kwa upande wake mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo ambaye pia ni Mbunge wa jimbo la Simanjiro, Mhe. Christopher Ole Sendeka amesema kuwa sekta ya Uvuvi pamoja na kazi kubwa wanayofanya bado kiasi cha bajeti kilichotengwa na kinachopelekwa kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali ni kidogo na hivyo aliwaomba wajumbe wa kamati hiyo kuungana kwa pamoja na kuwasilisha chagamoto hiyo kwa wahusika.
Kabla ya kuhitimisha kikao hicho, Mwenyekiti wa kamati hiyo Mhe. Christine Ishengoma amewataka wataalam wa sekta hiyo kuendelea kuwa karibu na wadau wake hasa wale waliojiingiza kwenye shughuli za ukuzaji viumbe maji ambapo alisema kuwa suala hilo ndo litapunguza upungufu wa samaki uliopo hapa nchini kwa hivi sasa.
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (kulia)
akiwaeleza wajumbe wa kamati ya kudumu ya bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji namna
uchumi wa buluu ulivyoanza kutekelezwa kwa upande wa Tanzania bara wakati wa
kikao cha kamati hiyo kilichofanyika (03.02.2022) kwenye moja ya kumbi za
bunge jijini Dodoma.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni