Nav bar

Jumanne, 1 Februari 2022

WAFUGAJI KIBAHA WAKABIDHIWA DUME LA KISASA

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe.  Abdallah Ulega amekabidhi Ng'ombe dume wa kisasa kwa wafugaji wa kijiji cha Miziguni kata ya Magindu, halmashauri ya Kibaha Vijijini, Mkoani Pwani kwa ajili ya kuboresha koosafu za mifugo yao.

Akizungumza wakati wa kukabidhi dume hilo Januari 30, 2022 Naibu Waziri Ulega alisema kuwa Ng'ombe huyo ametolewa na mdau wa mifugo kutoka shamba la Canbe ikiwa ni katika jitihada za kuunga mkono Serikali ya awamu ya sita katika ufugaji wa kisasa na kuboresha Mifugo.

Aliwataka wafugaji hao kuweka utaratibu mzuri kwa watu wote ambao wanahitaji mbegu ya dume hilo pamoja na kulitunza vizuri ili liweze kuhudumia majike mengi na kwa muda mrefu zaidi.

"Nawaombeni sana dume hili litumike kwa ajili ya kuboreshea mifugo yetu, wekeni utaratibu mzuri wafugaji wote wanaotaka kupandisha majike yao wasikose fursa hiyo hapa, pia mlifanyie uchunguzi wa mara kwa mara lisije likapata ugonjwa wa kutupa mimba kwasababu atakuwa anahudumia mitamba mingi kwa hiyo ni rahisi sana kuhamisha ugonjwa" alisema Ulega

Katika hatua nyingine Naibu Waziri Ulega amewataka wanawake jamii ya wafugaji wanaojishughulisha na uuzaji wa maziwa kuanzisha chama vya ushirika kitakacho wasaidia kuuza maziwa  bila changamoto yeyote.

Alisema pamoja na mambo mengine ushirika huo pia utawasaidia akina mama kupata mikopo kutoka katika benki ya kilimo (TADB).

Aliongeza kuwa mpango wa Serikali ni pamoja na kuleta miradi ya maji maeneo ya ukame Ili kuondokana na adha iliyotokea hapo nyuma ya kupoteza Mifugo mingi, na hivyo kuchimba mabwawa na malambo yatakayoenda kuwasaidia wafugaji.

"Tayari wadau wetu kutoka Heifer international wameahidi kutoa mabirika 10 ya kuwekea   maziwa na jokofu moja kwa ajili ya kusaidia akina mama wa Magindu wanaouza maziwa kuweza kuboresha bidhaa zao na kuuza kwa bei nzuri"

Kwa upande wake Mbunge wa Kibaha vijijini Mhe. Michael Mwakamo amemshukuru Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi kwa hatua nzuri wanazozichukua katika kukabiliana na changamoto ya malisho.

Alisema wamepokea maelekezo ya Wizara pamoja na elimu waliyoipata ikiwemo ya kilimo cha Malisho na uanzishwaji wa chama cha ushirika cha akina mama wauza maziwa ambapo wataanza kufanyia kazi mara moja ili kuunga mkono jitihada za Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan.


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega akabidhi ng'ombe dume aina ya borani kwa wafugaji wa kijiji cha Miziguni kata ya Magindu na kuwataka wafugaji hao walitunze dume hilo na kuhakikisha halipati ugomjwa wa kutupa mimba ili liweze kuwasaidia zaidi katika kuboresha Mifugo yao na kupata mbegu Bora zaidi. Januari 30, 2022 Mkoani Pwani. 


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni