Nav bar

Ijumaa, 29 Oktoba 2021

LITA YATAKIWA KUENDELEA KUTOA MAFUNZO YA MUDA MFUPI KWA WAFUGAJI

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki ameiagiza Wakala ya Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo (LITA) kuendelea kutoa mafunzo ya muda mfupi kwa wafugaji ili wafuge kisasa.

 

Waziri Ndaki ameyasema hayo leo (28.10.2021) alipotembelea Kampasi ya Tengeru iliyopo mkoani Arusha kwa lengo la kufungua bweni la wasichana lenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 80 ambalo litasaidia kupunguza changamoto ya miundombinu iliyopo.

 

“Wafugaji bado wanahitaji kupatiwa elimu ya ufahamu ili waweze kuelewa faida na hasara za kuendelea na njia ya ufugaji wa asili na njia bora za ufugaji wa kisasa utakaoweza kuwaletea tija ambapo kwa kuwatumia wataalam tunaowafundisha na waliopo katika maeneo mbalimbali tutaweza kubadilisha fikra za wafugaji wetu,” alisema Waziri Ndaki

 

Pia LITA imetakiwa kusaidia kutatua changamoto ya malisho kwa wafugaji kwa kutoa elimu juu ya umiliki wa maeneo na upandaji malisho. Waziri Ndaki amesema kupitia mashamba yao ya malisho ambayo hutumika kuwafundishia wanafunzi, pia wanaweza kuyatumia mashamba hayo kama mashamba darasa ambapo wafugaji watapata fursa ya kwenda kujifunza.

 

Aidha, amewashauri Bodi na Viongozi wa LITA kuangalia namna ya kutoa elimu ambayo itawasaidia wahitimu wa vyuo hivyo kwenda kujiajiri wenyewe badala ya kutegemea kuajiriwa. Hili pia amewaeleza wanafunzi baada ya kufungua bweni la wasichana kuwa ni lazima wasome kwa nguvu wakilenga kujiajiri.

 

Waziri Ndaki ameipongeza Bodi na Uongozi mzima wa LITA kwa kazi nzuri wanayoifanya ikiwemo ya ujenzi wa miundombinu kama bweni la wasichana licha ya changamoto walizonazo. Pia amewaahidi kuwa wizara itaendelea kutenga fedha za maendeleo katika bajeti kwa ajili ya kuendelea kutatua changamoto walizonazo zikiwemo za miundombinu, mitambo na vifaa mbalimbali na kwamba wizara itaangalia namna ya kuwasaidia ili kutatua changamoto ya usafiri kwa kununua basi la chuo.

 

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya LITA, Prof. Malongo Mlozi amesema majukumu ya LITA ni kutoa mafunzo ya muda mrefu katika ngazi ya Stashahada na Astashahada, kutoa huduma za ushauri na mafunzo ya muda mfupi kwa wafugaji, maafisa ugani pamoja na wadau wengine katika sekta, kufanya tafiti na huduma za ushauri ili kujitathmini na kuboresha mafunzo yanayotolewa na kuzalisha na kutunza aina mbalimbali za mifugo na malisho bora kwa ajili ya mafunzo na kuhudumia jamii ya watanzania.

 

Mtendaji Mkuu wa Wakalaya ya Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo, Dkt. Pius Mwambene amesema wakala imepata mafanikio mbalimbali ikiwemo ongezeko la udahili kutoka 798 mwaka 2012/13 hadi wanafunzi 3,592 mwaka 2020/21, ongezeko la ufikiaji wafugaji kutoka 267 mwaka 2012/13 hadi 2,104 mwaka 2020/21. Pamoja na mafanikio hayo bado wakala inakabiliwa na changamoto nyingi zikiwemo za miundombinu, upungufu wa walimu na watumishi wengine, uhaba wa fedha za maendeleo, usafiri, mitambo, lakini pia baadhi ya wanafunzi wasaidiwe kupata fursa ya mikopo.


Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki akifungua bweni la wasichana lenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 80 katika Chuo cha LITA Kampasi ya Tengeru mkoani Arusha ambapo amewataka wanafunzi hao kutunza miundombinu hiyo vizuri. (28.10.2021)

Mkuu wa Wilaya ya Arumeru mkoani Arusha, Mhe. Mhandisi. Richard H. Ruyango (kushoto) akitoa taarifa fupi ya Wilaya kwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki wakati alipofika ofisini kwake kwa ajili ya kusaini kitabu cha wageni. (28.10.2021)

Mwenyekiti wa Bodi ya LITA, Prof. Malongo Mlozi (kushoto aliyesimama) akitoa taarifa fupi ya utekelezaji wa majukumu ya bodi kwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki wakati alipotembelea Chuo cha LITA Kampasi ya Tengeru mkoani Arusha kwa lengo la kufungua bweni la wasichana lenye uwezo wa kubeba wanafunzi 80. Prof. Mlozi amesema moja ya jukumu walilokuwa nalo ni kuhakikisha kuna kuwa na ongezeko la wanafunzi hivyo kufunguliwa kwa bweni hilo kutasaidia sana. Taarifa hiyo imesomwa katika ofisi ya meneja Kampasi ya Tengeru mkoani Arusha. (28.10.2021)

Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo (LITA), Dkt. Pius Mwambene akitoa taarifa ya Wakala hiyo kwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki wakati alipotembelea Chuo cha LITA Kampasi ya Tengeru mkoani Arusha kwa ajili ya kuzindua bweni la wasichana. Dkt. Mwambene amesema licha ya mafanikio wanayoyapata bado wakala inakabiliwa na changamoto kubwa ya upungufu wa miundombinu, mitambo, upungufu wa walimu na watumishi wengine, uhaba wa fedha za maendeleo, usafiri, mitambo, lakini pia baadhi ya wanafunzi wasaidiwe kupata fursa ya mikopo. (28.10.2021)

Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti, Mafunzo na Huduma za Ugani (WMUV), Dkt. Angello Mwilawa akitoa maelezo kuhusu aina ya malisho ya mifugo yaliyopandwa katika shamba la chuo kwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki wakati alipotembelea moja ya shamba la malisho katika Chuo cha LITA Kampasi ya Tengeru. (28.10.2021)

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki akipanda mti nje ya bweni la wasichana kwenye Chuo cha LITA Kampasi ya Tengeru mara baada ya kulifungua. (28.10.2021)

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki akizungumza na wanafunzi wa Chuo cha LITA Kampasi ya Tengeru mara baada ya kufungua bweni la wasichana ambapo amewasihi kusoma kwa bidii huku wakilenga zaidi kwenda kujiajiri mara baada ya kuhitimu masomo yao. (28.10.2021)

Alhamisi, 28 Oktoba 2021

NDAKI: TUMIENI UTAALAM WENU KUWAELIMISHA WAFUGAJI NA WAVUVI

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki amewataka wataalamu wa mifugo na uvuvi kutoa elimu ya kitaalam kwa wafugaji na wavuvi ili waweze kufuga kwa tija.

 

Waziri Ndaki aliyasema hayo leo (27.10.2021) wakati akifungua Mkutano wa 44 wa Wataalam wa Uzalishaji Mifugo Tanzania (TSAP) wenye kauli mbiu ya Uzalishaji Endelevu wa Mifugo na Samaki wakati wa janga la UVIKO 19 uliofanyika kwenye ukumbi wa Olasiti Garden Hotel jijini Arusha.

 

Kutokana na janga la UVIKO 19, wataalam wametakiwa kuongeza kasi katika utoaji elimu kwa wafugaji na wavuvi ili kuwapa mbinu bora zitakazowasaidia kuongeza uzalishaji na kuweza kukidhi soko la nyama na samaki ambalo kwa sasa linazidi kukua kutokana na kufunguka kwa masoko ya nje ya nchi kutokana na jitihada kubwa zinazofanywa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan za kufungua fursa za masoko ya mifugo na samaki nchi za nje haswa kwenye masoko ya Uarabuni, Ulaya na China.

 

Pia amewasihi wataalam walioshiriki mkutano huo kuishauri serikali haswa Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuhusu namna bora ya kuongeza uzalishaji na kupunguza migogoro ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi. Waziri Ndaki amesema kuwa Wizara itaendeleza jitihada za kuhakikisha kuna kuwa na mazingira bora ya kufuga, kusindika na kufanya biashara ya mazao ya mifugo na uvuvi.

 

Lakini pia Waziri Ndaki amewasisitiza wafugaji kuendelea kununua maeneo kihalali kwa ajili ya shughuli za ufugaji na kuhakikisha wanayapima na kuyamiliki ili waondokane na migogoro. Vilevile amewasisitiza kuendelea kupanda malisho katika maeneo watakayoyamiliki ili kuondokana na tatizo la malisho kwa mifugo.

 

Naye Mwenyekiti wa Chama hicho cha TSAP, Dkt. Daniel Komwihangilo alisema lengo la chama hicho ni kuhimiza maendeleo katika sayansi ya uzalishaji na uendelezaji wa mifugo hapa nchini, kutoa fursa kwa wadau wote wa tasnia ya mifugo kukutana ili kubadilishana mawazo na uzoefu, na kushirikiana na wataalam na wanachama wa waliopo katika vyama vya taaluma chini katika sekta ya mifugo na uvuvi ili kuendeleza sekta hizo. Chama hicho kwa sasa kina wanachama zaidi ya 300 ambao wapo hai kutoka katika sekta mbalimbali.

 

Aidha, amemuomba Waziri kuangalia uwezekano wa kuunda chombo maalum cha kutambua na kuisimamia kada hiyo kisheria. Vilevile amemshukuru Waziri kwa ushirikiano anaoutoa katika kusimamia sekta ya mifugo na uvuvi na kwamba wao kama chama wataendelea kutoa ushirikiano kwa serikali katika kuhakikisha uzalishaji unaongezeka.


Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki akifungua Mkutano wa 44 wa Wataalam wa Uzalishaji Mifugo Tanzania ambapo amewataka wataalam hao kutumia utaalamu wao kuwaelimisha wafugaji na wavuvi ili waweze kufuga kisasa. Mkutano huo umefanyika katika ukumbi wa Olasiti Garden Hotel Jijini Arusha. (27.10.2021)

Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti, Mafunzo na Huduma za Ugani, Dkt. Angello Mwilawa akiwasalimia wajumbe wa Mkutano wa 44 wa Wataalam wa Uzalishaji Mifugo Tanzania ambapo pia alisema mkutano huo unawasaidia wataalam kutoka maeneo tofauti kubadilishana uzoefu. Mkutano huo umefanyika katika ukumbi wa Olasiti Garden Hotel Jijini Arusha. (27.10.2021)

Mwenyekiti wa Chama cha Wataalam wa Uzalishaji wa Mifugo Tanzania, Dkt. Daniel Komwihangilo akitoa maelezo mafupi kuhusu chama hicho kwenye Mkutano wa 44 wa chama hicho ambapo amesema moja ya malengo yake ni kuhimiza maendeleo katika sayansi ya uzalishaji na uendelezaji wa mifugo hapa nchini. Mkutano huo umefanyika katika ukumbi wa Olasiti Garden Hotel Jijini Arusha. (27.10.2021)

Msajili wa Bodi ya Maziwa nchini ambaye pia ni Katibu Msaidizi wa TSAP, Dkt. George Msalya akiwatambulisha wajumbe walioshiriki Mkutano wa 44 wa Wataalam wa Uzalishaji Mifugo Tanzania kwa mgeni rasmi Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki. Mkutano huo umefanyika katika ukumbi wa Olasiti Garden Hotel Jijini Arusha. (27.10.2021)

Wajumbe wa Mkutano wa 44 wa Wataalam wa Uzalishaji Mifugo Tanzania wakifuatilia mada zilizokuwa zikiwasilishwa katika mkutano huo uliofanyika kwenye ukumbi wa Olasiti Garden Hotel Jijini Arusha. (27.10.2021)

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (kulia) akipokea zawadi ya maziwa kutoka kwa wawakilishi wa Kampuni za Kilimanjaro Fresh na Asas Dairies Ltd mara baada ya kumaliza kufungua Mkutano wa 44 wa Wataalam wa Uzalishaji Mifugo Tanzania uliofanyika katika ukumbi wa Olasiti Garden Hotel Jijini Arusha. (27.10.2021)

Picha ya Pamoja ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (wanne kutoka kushoto waliokaa) na Wajumbe wa Mkutano wa 44 wa Wataalam wa Uzalishaji Mifugo Tanzania mara baada ya kumalizika kwa ufunguzi wa mkutano uliofanyika kwenye ukumbi wa Olasiti Garden Hotel Jijini Arusha. (27.10.2021)




Jumanne, 26 Oktoba 2021

WAZIRI NDAKI ANG’AKA UKUSANYAJI MDOGO WA MADUHULI*

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (Mb) amewaagiza watendaji wakuu wa wizara kuhakikisha makusanyo ya maduhuli yanafikia malengo ya bajeti ya mwaka wa fedha 2021/22 baada ya kupokea taarifa ya makusanyo ya robo mwaka ya bajeti hiyo ambayo hakuridhika nayo ukilinganisha na bajeti iliyopita.

Akizungumza leo (26.10.2021) katika kikao cha kupokea taarifa ya ukusanyaji wa maduhuli ya robo mwaka kwa bajeti ya wizara ya mwaka wa fedha 2021/22 Sekta ya Mifugo jijini Dodoma, Waziri Ndaki amesema utaratibu wa ukusanyaji maduhuli uko wazi lakini kuna shida ya namna ya ukusanyaji pamoja na fedha nyingine kutojulikana zinapopelekwa baada ya kukusanywa.

Ameongeza kuwa amesikitishwa na baadhi ya minada ya mifugo, kutofikia malengo yaliyowekwa katika robo ya mwaka ya bajeti kati ya Mwezi Julai hadi Septemba mwaka huu na kumlazimu kutoa uamuzi wa kuwaondoa baadhi ya wasimamizi wa minada kwenye nafasi zao na wengine kuwaweka katika kipindi cha uangalizi ili kufuatilia utendaji kazi wao katika ukusanyaji wa maduhuli.

“Picha hii tunayoiona hapa inaonyesha tatizo ni kubwa namna ya kukusanya pesa katika ngazi ya chini kwenye vituo vyetu na siyo makao makuu, sababu zinazotajwa na watu wanaokusanya ni zile zile miaka yote na bado tulikusanya, kwa nini kipindi hiki makusanyo yashuke?” amehoji Mhe. Ndaki

Kufuatia ukusanyaji wa kiwango cha chini wa maduhuli katika kipindi cha robo mwaka ya bajeti kwa mwaka wa fedha 2021/22 Sekta ya Mifugo, Waziri Ndaki ameagiza kufikia tarehe 28 mwezi huu kuwe kumeundwa timu ya ufuatiliaji wa makusanyo ya maduhuli.

Ameongeza kuwa timu hiyo ambayo anataka akutane nayo kabla ya utekelezaji wa majukumu yake, inapaswa kufanya kazi kwa weledi na kutoa taarifa za ukweli bila kupendelea wala kumuonea mtu na kuhakikisha inapita katika minada yote ya mifugo na halmashauri zote nchini kufuatilia utekelezaji wa ukusanyaji wa maduhuli.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (Mb) amesema amekuwa akikerwa na utoroshaji wa rasilimali za mifugo nchini kwenda nje ya nchi na uingizaji wa mazao ya mifugo kinyume na utaratibu ambapo wanaweza kuwa wanaingiza mazao mbalimbali kwa kuwa hawalipi kodi na kuathiri uzalishaji ndani ya nchi mambo ambayo hayavumiliki.

Amesema vitendo hivyo vimekuwa vikiathiri kwa kiasi kikubwa ukusanyaji wa mapato ya mifugo na mazao yake hali inayoifanya serikali kukosa mapato.

Naye Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia mifugo Bw. Amosy Zephania akizungumza kando ya kikao hicho amesema maazimio yaliyotolewa katika kikao hicho ni kupitia na kufanya tathmini ya kila kituo cha kukusanyia mapato na kupima utekelezaji wa ukusanyaji, kuimarisha timu ya kufuatilia maduhuli sehemu zote katika sekta ya mifugo pamoja na halmashauri kurejesha fedha kutokana na makusanyo kwa ajili ya kuingizwa katika mfuko mkuu wa serikali.

Kikao kingine cha taarifa ya ukusanyaji wa maduhuli kwa bajeti ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi Sekta ya Mifugo mwaka wa fedha 2020/2021 kinatarajiwa kufanyika mwezi januari mwaka 2022 au muda wowote kama ambavyo itaelekezwa na Uongozi wa Wizara. Utaratibu huu wa kukutana kila robo mwaka ni maelekezo ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (Mb)


Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (Mb) akizungumza wakati wa kupokea taarifa ya ukusanyaji wa maduhuli ya robo mwaka kwa bajeti ya wizara ya mwaka wa fedha 2021/22 Sekta ya Mifugo jijini Dodoma, ambapo Waziri Ndaki amesema utaratibu wa ukusanyaji maduhuli uko wazi lakini kuna shida ya namna ya ukusanyaji pamoja na fedha nyingine kutojulikana zinapopelekwa baada ya kukusanywa. (26.10.2021) 

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (Mb) akizungumzia kukerwa na utoroshaji wa rasilimali za mifugo nchini kwenda nje ya nchi na uingizaji wa mazao ya mifugo kinyume na utaratibu ambapo wanaweza kuwa wanaingiza mazao mbalimbali kwa kuwa hawalipi kodi na kuathiri uzalishaji ndani ya nchi mambo ambayo hayavumiliki. Amezungumza hayo wakati wa kikao cha kupokea taarifa ya ukusanyaji wa maduhuli ya robo mwaka kwa bajeti ya wizara ya mwaka wa fedha 2021/22 Sekta ya Mifugo jijini Dodoma. (26.10.2021) 

Baadhi ya washiriki wa kikao cha kupokea taarifa ya ukusanyaji wa maduhuli ya robo mwaka kwa bajeti ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi Sekta ya Mifugo kwa mwaka wa fedha 2021/22 Sekta ya Mifugo jijini Dodoma, wakifuatilia mwenendo wa kikao hicho kilichoongozwa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (Mb). (26.10.2021) 


Ijumaa, 22 Oktoba 2021

WAZIRI NDAKI ATAKA KUWEKWA VIPAUMBELE ZAIDI KATIKA TASNIA YA MAZIWA

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki amesema ni muhimu uwekezaji uwekewe kipaumbele katika sekta za uzalishaji zikiwemo za mifugo na uvuvi ili nchi iweze kuuza maziwa nje ya nchi.

Akizungumza (21.10.2021) jijini Dodoma wakati wa uwasilishaji wa taarifa ya utendaji kazi wa Bodi ya Maziwa nchini kwa kamati ya Kudumu ya Bunge, Kilimo, Mifugo na Uvuvi amesema matatizo mengi yanaweza kutatuliwa katika tasnia ya maziwa na uzalishaji wa tasnia hiyo ili kukuza wigo wa upatikanji wa kutosha wa maziwa katika ngazi ya uzalishaji.

“Suala hili la uwekezaji linapokuwa dogo linatuathiri katika maeneo mengi, kwa kweli unahitajika uwekezaji wa kutosha katika tasnia ya maziwa ili kuongeza uzalishaji na kuweza kuuza maziwa nje ya nchi.” Amesema Mhe. ndaki

Aidha amesema serikali imekuwa ikihimiza wafugaji kuwa katika vyama vya ushirika kama nyenzo ya kuweza kuwafikia wafugaji kwa uhakika ili kuzalisha na kukusanya maziwa katika mfumo rasmi kwa ajili ya kutumika katika viwanda vya kuchakata maziwa nchini.

Kwa upande wake Msajili wa Bodi ya Maziwa nchini Dkt. George Msalya amesema asilimia 80 ya maziwa yanayozalishwa hapa nchini hayapo katika mfumo rasmi hivyo inahitajika jitihada zaidi ili yawe kwenye mfumo huo kwa ajili ya kujulikana ubora wake kabla ya kutumika kwenye viwanda vya kuchakata maziwa nchini.

Amefafanua kuwa bado tasnia ya maziwa katika mchango wa taifa ni mdogo licha ya kwamba bodi imekuwa ikiendelea na jitihada mbalimbali za kuhakikisha unywaji wa maziwa unaongezeka nchini.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge, Kilimo, Mifugo na Maji Mhe. Dkt. Christine Ishengoma amesema ni muhimu kwa wafugaji kwa sasa kubadili fikra zao na kufuga kisasa kwa kuwa na ng’ombe wachache wenye uwezo wa kutoa maziwa mengi.

Amebainisha kuwa ni vyema kuwepo na mikakati ikiwemo ya takwimu ili kufahamu kiasi sahihi cha maziwa kinachozalishwa nchini kutoka kwa ng’ombe wa asili na walioboreshwa.


Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (Mb), akifafanua jambo na kujibu maswali mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge, Kilimo, Mifugo na Maji wakati wa uwasilishaji wa taarifa ya utendaji kazi wa Bodi ya Maziwa nchini jijini Dodoma, ambapo Mhe. Ndaki amesema ni muhimu uwekezaji uwekewe kipaumbele katika sekta za uzalishaji zikiwemo za mifugo na uvuvi ili nchi iweze kuuza maziwa nje ya nchi. (21.10.2021) 


Msajili wa Bodi ya Maziwa nchini Dkt. George Msalya akiwasilisha taarifa ya utendaji kazi wa bodi hiyo mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge, Kilimo, Mifugo na Maji jijini Dodoma na kufafanua kuwa asilimia 80 ya maziwa yanayozalishwa hapa nchini hayapo katika mfumo rasmi hivyo inahitajika jitihada zaidi ili yawe kwenye mfumo huo kwa ajili ya kujulikana ubora wake kabla ya kutumika kwenye viwanda vya kuchakata maziwa nchini. (21.10.2021) 

 

 

UHITAJI WA NYAMA WAONGEZEKA, YABAINIKA SEKTA KUKUA

Serikali imesema malalamiko yaliyojitokeza hivi karibuni ya kupanda kwa bei ya nyama nchini yanaashiria ukuaji wa sekta hiyo ambapo wafugaji wameshauriwa kuwa muda huu ni mzuri kwa wao kuvuna na kuuza mifugo yao.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (Mb) amebainisha hayo leo (20.10.2021) jijini Dodoma, mbele ya wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge, Kilimo, Mifugo na Maji wakati wa uwasilishaji wa taarifa ya utendaji kazi wa Bodi ya Nyama nchini mbele ya kamati hiyo.

Mhe. Ulega amesema kipindi cha nyuma wafugaji walikuwa wakilalamika kutopata masoko ya mifugo yao ila katika kipindi cha sasa uhitaji wa mifugo katika viwanda vya kuchakata nyama nchini umekuwa mkubwa pamoja na hitaji la nyama katika soko la ndani.

“Sekta ambayo ulikuwa hauwezi kuisikia inasemwa, lakini leo inakuwa mjadala hivyo ni wakati mzuri sana kwa wafugaji kuvuna na kuuza mifugo yao.” Amesema Mhe. Ulega

Amesema serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan imetengeneza uhitaji wa nyama baada ya kufungua biashara ya kuuza nyama nje ya nchi hivyo uhitaji wa mifugo kwenye viwanda vya kuchakata hapa nchini umeongezeka.

Kwa upande wake Msajili wa Bodi ya Nyama nchini Dkt. Daniel Mushi ameiambia kamati hiyo kuwa uhaba wa nyama uliojitokeza hivi karibuni na kusababisha bei ya nyama kupanda ni fursa ya kufuga kibiashara na kunenepesha mifugo hiyo.

Amesema kwa sasa sera ya serikali ni kuhamasisha uwepo wa vikundi kwa ajili ya unenepeshaji wa mifugo ili kupatikana kwa mifugo bora kulingana na hitaji la soko la sasa hususan kwenye viwanda vya kuchakata nyama nchini.

Ameongeza kuwa hivi karibuni Tanzania kupitia viwanda vilivyopo nchini itaanza kupeleka nyama katika soko la Saudi Arabia na kwamba hitaji la soko hilo ni Tani Laki Sita kwa mwaka hali ambayo itachangia kwa kiasi kikubwa kukuza sekta ya mifugo nchini.

Kuhusu ugonjwa wa midomo na miguu (FMD) ambao unaathiri mifugo na kusababisha Tanzania kushindwa kupeleka nyama katika baadhi ya nchi za nje kulingana na masharti yaliyopo kwenye nchi hizo, akimwakilisha Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo, Msajili wa Baraza la Veterinari Tanzania (RVCT) Dkt. Bedan Masuruli amesema ugonjwa huo umekuwa ukiathiri kwa kiasi kikubwa biashara ya nje na kwamba umekuwa ukisababishwa na uwepo wa wanyama pori.

Amesema ni vigumu kudhibiti ugonjwa huo kwa kuwa Tanzania ina kirusi cha ugonjwa huo ambacho hakipo kwenye chanjo ambazo zinaingizwa nchini kutoka nchi za nje kwa ajili ya kudhibiti ugonjwa huo na kwamba kuna virusi aina saba vya ugonjwa huo.

Amefafanua baadhi ya viwanda ambavyo vimepewa vibali vya kusafirisha nyama kwenda ya nchi vinataratibu ya kuweka mifugo karantini kabla ya kuchinjwa ili kujiridhisha mifugo hiyo kutokuwa na ugonjwa wa midomo na miguu ambao hauathiri binadamu.

Akizungumza wakati akihitimisha kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge, Kilimo, Mifugo na Maji Mwenyekiti wa kamati hiyo Mhe. Dkt. Christine Ishengoma baada ya kamati kusomewa taarifa ya utendaji kazi wa Bodi ya Nyama nchini, ameishauri Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuendelea kuisimamia vyema sekta ya mifugo ili iweze kuongeza mapato kwa kuuza mifugo na mazao yake ndani na nje ya nchi.

Pia, amesema ni vyema elimu iendelee kutolewa kwa ajili ya uzalishaji wenye tija kwenye masoko na uvunaji wa mifugo kusudi uzalishaji uwe wenye tija na kwamba mifugo ipo mingi wafugaji hawapaswi kutokuvuna mifugo yao hali ambayo inasababisha pia viwanda vya kuchakata nyama kutopata malighafi ya kutosha.


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (Mb), (aliyesimama) akifafanua jambo na kujibu maswali mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge, Kilimo, Mifugo na Maji wakati wa uwasilishaji wa taarifa ya utendaji kazi wa Bodi ya Nyama nchini jijini Dodoma, ambapo Mhe. Ulega amesema malalamiko yaliyojitokeza hivi karibuni ya kupanda kwa bei ya nyama nchini yanaashiria ukuaji wa sekta hiyo ambapo wafugaji wameshauriwa kuwa huu ni muda mzuri kwa wao kuvuna na kuuza mifugo yao. (20.10.2021) 

 


Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge, Kilimo, Mifugo na Maji Mhe. Dkt. Christine Ishengoma akifafanua jambo wakati wa kuhitimisha kikao kilichopokea taarifa ya utendaji kazi wa Bodi ya Nyama nchini jijini Dodoma, na kuishauri Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuendelea kuisimamia vyema sekta ya mifugo nchini ili iweze kutoa uzalishaji wenye tija. (20.10.2021) 

 

ULEGA: TUMEJIPANGA KUINUA BIASHARA YA DAGAA WA KIGOMA

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amesema Serikali ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imejipanga kuhakikisha Dagaa wa Kigoma wanakuwa ni zao la kimkakati kibiashara litakalokwenda kuvutia uwekezaji na kusisimua uchumi wa mtu mmoja mmoja na nchi kwa ujumla.

Ulega aliyasema hayo wakati akiongea na Wadau wa Uvuvi alipofanya kikao nao katika Mwalo wa Katonga uliopo Mkoani Kigoma Oktoba 17, 2021.

Alisema kuwa serikali imejipanga kufanya zao la dagaa wa Kigoma kuwa la kimkakati kwa sababu biashara ya dagaa inahusisha watu wengi katika jamii, hivyo kuiimarisha biashara hiyo ni kuwaimarisha wananchi kiuchumi.

"Sisi Serikali tunataka kuinua biashara ya dagaa wa Kigoma, tunataka wavuvi wainuke kiuchumi, na tumejipanga kuondoa vikwazo vyote vinavyowasumbua na tutalitangaza vyema zao hili ili kuvutia uwekezaji zaidi hapa Kigoma," alisema Ulega

Pia, Naibu Waziri Ulega aliwataka Viongozi wa Mkoa huo kuanza mikakati na kampeni maalum kwa ajili ya  kutangaza ubora wa dagaa wa Kigoma ili kuvutia uwekezaji wa viwanda vidogovidogo na vikubwa kwa ajili ya kuchakata dagaa hao.

Aliendelea kusema kuwa zao hilo la dagaa likitangazwa vizuri, wawekezaji na Taasisi za kibenki wote watakwenda kuwekeza  na ndio itakuwa mwisho wa dagaa wa Kigoma kutupwa tupwa hovyo kwa sababu ya kukosa soko.

Aidha, aliongeza kwa kusema kuwa uvunaji wa dagaa hao uendane sambamba na utunzaji wa mazalia ya samaki ili upatikanaji wa rasilimali hiyo uwe wa uhakika wakati wote.

"Ndugu zangu, mkakati huu wa kuinua biashara ya zao la dagaa hautafanikiwa kama malighafi haitakuwepo, ili viwanda viweze kuanzishwa ni lazima malighafi ipatikane ya kutosha," alisistiza Ulega

Alisema Serikali imejipanga kuwawezesha wavuvi vifaa mbalimbali vitakavyowasaidia kuvuna dagaa kwa uhakika na kuwakausha kwa kutumia vichanja vya kisasa ili kupunguza upotevu wa dagaa na kuongeza ubora wake.

Naye, Diwani wa Kata ya Bangwe, Hamisi Besete alisema Serikali kwa Sasa inapoteza mapato mengi kwa sababu Mwalo wa Katonga haujajengwa hivyo kuwafanya wafanyabiashara wa Samaki na Dagaa kukosa sehemu ya kuuzia.

"Mhe. Naibu Waziri, Mwalo wa Katonga ni mkubwa sana hapa Kigoma, tunaomba mtujengee mwalo huu ili Serikali iweze kukusanya mapato ya kutosha hapa kutokana na biashara ya mazao ya Uvuvi, sasa hivi mapato yanapotea kwa sababu Wafanyabiashara hawana sehemu rasmi ya kuuzia samaki wao," alisema Besete

Mbunge wa Kigoma Mjini, Kilumbe Ngenda nae alisema kuwa kwa sababu sasa nchi inaelekea katika uchumi wa buluu ambao unataka kuongezeka kwa kasi ya uzalishaji katika Bahari na Maziwa ili kukuza uchumi wa nchi, Serikali ione uwezekano wa kupunguza baadhi ya masharti ili wananchi wengi waweze kuingia katika uchumi wa buluu.


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega (kulia) akimpa maelekezo Afisa Mfawidhi, Usimamizi wa Rasilimali za Uvuvi Kanda Kuu ya Tanganyika, Juma Makongoro wakati wa Mkutano na Wavuvi wanaofanya shughuli zao katika Mwalo wa Katonga uliopo Mkoani Kigoma Oktoba 17, 2021. 

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega akieleza ubora wa dagaa wa Kigoma alipotembelea Mwalo wa Katonga uliopo Mkoani Kigoma kuangalia namna Wavuvi wanavyokausha dagaa hao katika vichanja. 


 

WAVUVI WAHIMIZWA KUTUNZA MAZALIA YA SAMAKI KUINUA UZALISHAJI

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amewataka wavuvi wanaofanya shughuli zao Wilayani Uvinza, Mkoani Kigoma kutunza mazalia ya Samaki ili waweze kuzaliana na kuongezeka jambo ambalo litasaidia kuongeza uzalishaji na kukuza uchumi wa buluu nchini.

Ulega alitoa wito huo wakati akiongea na wavuvi wa Vijiji vya Buhingu  na Igalula alipofanya ziara  ya kukagua shughuli za uvuvi zinazofanyika Mkoani humo Oktoba 16, 2021.

Alisema ni muhimu kutunza mazalia hayo kwani ndio kiwanda cha kuzalisha malighafi huku akiwakumbusha wananchi kuwa kwa kufanya hivyo kutapelekea samaki kuongezeka na hivyo watakuwa na uhakika wa kupata lishe bora na kukuza kipato chao.

"Wananchi ungeni mkono jitihada za Serikali na wadau wengine wa maendeleo katika kuhakikisha mazingira ya mazalia ya Samaki yanatunzwa vizuri, mkifanya hivyo mazao mengi yatapatikana na uchumi wenu hapa utainuka," alisema Ulega

Aliendelea kusema kuwa uchumi wa wananchi hao ukiinuka kupitia biashara nzuri ya samaki watakayoifanya wataweza kutoka katika uvuvi wanaofanya sasa wa kuwinda na kufanya uvuvi wa kisasa kwa sababu watakuwa na uwezo wa kupata vifaa bora vya kuwarahisishia shughuli zao hizo.

Aidha, aliupongeza Mradi wa Tuungane ambao kwa kushirikisha na Serikali wanahamasisha jamii kutunza maeneo ya mazalia samaki Wilayani Uvinza na tayari wametenga maeneo ya hifadhi katika Vijiji mbalimbali.

"Niwaombe muendelee kutanua wigo wa utunzaji wa mazalia, ongezeni mipaka ya kutunza, tunzeni na baada ya muda mvune samaki, huu ndio uchumi wa buluu anaouhamasisha Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan," aliongeza 

Waziri Ulega aliwataka wananchi wanaoishi katika Vijiji hivyo vilivyopo kandokando ya Ziwa Tanganyika kuhakikisha wanajipanga kuyalinda maeneo hayo ili waharibifu wasiweze kuingia katika maeneo hayo kuvuna samaki kiholela.

"Hakikisheni harakati zenu hizi hazirudi nyuma, muwe walinzi wa maeneo haya, Serikali ipo pamoja na nyinyi," alisistiza

Katika kuunga mkono jitihada hizo, Naibu Waziri Ulega alitoa ahadi ya kuwapatia Injini za Boti 2 kwa kikundi cha Ushirika cha Wavuvi cha Katumbi kilichopo katika  Kijiji cha Buhingu na  kingine kimoja kitakachopatikana katika Kijiji cha Igalula ili waweze kuzitumia kufanya shughuli zao za uvuvi ikiwemo kutunza mazalia ya Samaki.

Naye, Kaimu Mkurugenzi, Mradi wa Tuungane, Peter Limbu alisema kuwa kupitia mradi huo wanaweza kuunda mazalia ya samaki 10 kwenye Vijiji 10 ambayo jamii katika vijijini hivyo wanashiriki kuhifadhi na maeneo hayo yamechukua jumla ya Ekari Elfu Thelathini na Nne (34000).

"Zoezi hili la kutambua maeneo ya mazalia ya samaki tulishirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) na walitusaidia kubainisha maeneo hayo ambayo sasa tumeyahifadhi," alisema Limbu.



Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega (kushoto) akikata utepe kuashiria uzinduzi wa jengo jipya lililojengwa kupitia ufadhili wa Mradi wa Tuungane kwa ajili ya kutumika na kikundi shirikishi cha ulinzi na usimamizi wa rasilimali za uvuvi katika ziwa Tanganyika (BMU) kilichopo katika Kata ya Igalula, Wilayani Uvinza, Mkoani Kigoma Oktoba 16, 2021. Kulia ni Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Uvinza, Ester Mahawe. 

MIFUGO NA UVUVI WASHINDI WA PILI MAADHIMISHO YA SIKU YA CHAKULA DUNIANI.

Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeibuka mshindi wa pili kwenye matokeo ya jumla ya Maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya chakula Duniani kwa mwaka huu yaliyotangazwa wakati wa kilele cha Maadhimisho hayo leo (17.10.2021) mkoani Kilimajaro.

Wizara imeshika nafasi hiyo kufuatia kuongoza kwenye kipengele cha Taasisi iliyoonesha ubunifu wa kuchakata mazao yake kwenye mabanda ya maonesho kwa taasisi zote zilizoshiriki kwenye maadhimisho hayo ambapo nafasi ya kwanza imechukuliwa na banda la Umoja wa mataifa.

Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa zawadi ya kombe na cheti kufuatia ushindi huo, Mkurugenzi Msaidizi huduma za Ugani (Mifugo) Dkt. Kejeri Gillah amesema kuwa ushindi huo umetokana na umoja na mshikamano uliopo baina ya Wizara, Taasisi na wadau waliopo chini yao ambapo amesisitiza kudumisha ushirikiano huo wakati wote.

“Tulikuwa na wadau wa tasnia ya maziwa, nyama, ufugaji wa kuku na wale wanaojihusisha na ufugaji wa samaki na ulinzi wa rasilimali za uvuvi kwa ujumla, hawa wote walikuwa wakionesha ubunifu wa namna gani wanahakikisha mlaji anapata lishe yenye mazao yote yanayotokana na sekta za mifugo na uvuvi na kwa kweli watu wamefurahia huduma zetu mara zote walipofika hapa” Amesema Dkt. Gillah.

“Niendelee kuwasisitiza wananchi waendelee kula vyakula ambavyo vina asili ya nyama kwa sababu vimethibitika kutoa protini namba moja ambayo inaimarisha afya ya mwili na akili ya mlaji na waongeze kiwango cha unywaji wa maziwa ili wawe na nguvu na uwezo wao wa kufikiria uongezeke pia” Amesisitiza Dkt. Gillah.

Kwa upande wake mmoja wadau walioonesha ubunifu katika banda la Wizara hiyo ambaye ni Mkurugenzi wa Kiwanda cha Maziwa cha Nronga kilichopo Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, Bi. Hellen Usiri ameishukuru Wizara ya Mifugo na Uvuvi na Bodi ya Maziwa nchini (TDB) kwa ushirikiano mkubwa wanaowapa wakati wote wanapowahitaji.

“Niiombe Wizara iendelee kuweka msisitizo kwenye huu mpango wa unywaji maziwa shuleni kwa sababu utasaidia sana kuinua kiwango cha ufaulu hapa nchini kwa sababu tayari tumeshaona matokeo yake kwenye shule ambazo zimeshaanza kutekeleza mpango huu” Amesema Usiri.

Awali akisoma hotuba ya kufunga Maadhimisho hayo kwa mwaka huu, Mgeni rasmi ambaye pia ni Waziri wa Kilimo, Prof. Adolph Mkenda amesema kuwa  Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia taasisi yake ya Wakala ya Maabara ya Veterinari nchini (TVLA) imeweza kuzalisha dozi milioni 63 za chanjo  kwa ajili ya kuikinga mifugo dhidi ya magonjwa ya mdondo, kimeta, chambavu, Homa ya mapafu ya ng’ombe na Ugonjwa wa kutupa mimba ambapo pia ameongeza kuwa Taasisi hiyo inaendelea kufanya utafiti ili kuzalisha chanjo za magonjwa mengine yanayoathiri mifugo hapa nchini.

“Kwa upande wa Sekta ya Uvuvi, Wizara hiyo ina mpango wa kufanya ujenzi wa mitambo ya barafu, kutengeneza chanja za kukaushia dagaa,ununuzi  wa vifaa vya kukaushia samaki vinavyotumia mwanga wa jua na ujenzi wa soko kubwa la samaki la Kipumbwi wilayani Pangani mkoani Tanga” Amesema Prof. Mkenda.

Maadhimisho ya kitaifa ya Siku ya Chakula Duniani kwa mwaka huu yalianza Oktoba 10 hadi leo ambapo wananchi wa Mkoa wa Kilimanjaro wamepata fursa ya kujifunza teknolojia mbalimbali za uchakati wa mazao mbalimbali ya sekta za kilimo, mifugo na Uvuvi huku pia wakipata elimu inayohusu lishe bora.



Mgeni Rasmi wa kilele cha Maadhimisho ya kitaifa ya Siku ya Chakula Duniani ambaye pia ni Waziri wa Kilimo, Prof. Adolph Mkenda (kulia) akimkabidhi zawadi ya kombe, Afisa Utumishi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Scholastica Mdoe baada ya Wizara hiyo kuibuka mshindi wa jumla wa nafasi ya  pili kwenye kipengele cha Taasisi zilizoonesha ubunifu wa teknolojia mbalimbali wakati wote wa Maadhimisho hayo yaliyohitimishwa (17.10.2021)  Mkoani Kilimanjaro.

WAVUVI WATAKIWA KUWA WALINZI WA MAZINGIRA YA BAHARI KUKABILIANA NA ASIDI

Wavuvi na watumiaji wengine wa baharini wametakiwa kuwa walinzi wa mazingira ili kukabiliana na uchafuzi wa hewa ya ukaa inayoikabili dunia kutokana na kuwepo kwa asidi nyingi baharini.

Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) Dkt. Ishmael Kimirei, amesema hayo (15.10.2021) wakati wa uzinduzi wa mitambo itakatayotumika kupata taarifa ya hali ya hewa katika Bahari ya Hindi kwenye mwambao wa Tanzania.

“Ripoti zinaonesha Bahari ya Hindi inaongezeka joto kwa kasi zaidi kuliko bahari zote duniani na joto limeongezeka kwa asilimia 0.88, na hii ni ripoti ya mwaka jana. Tukiondoa mifumo ya ikolojia inayosababisha dunia iwe baridi itasababisha kesho kuwa ngumu zaidi,” amefafanua Dkt. Kimirei.

Kwa upande wake Afisa Utafiti wa TAFIRI, Dkt. Baraka Sekadende alisema mbali na mradi huo wa kuangalia asidi baharini, TAFIRI imeanza kupima ongezeko la vurutubisho maji ili kuwa na samaki wenye afya ambapo kutaongeza tija kwenye mazao ya samaki na kunufaisha wavuvi

Aidha, Mwenyekiti wa Kikundi cha Ulinzi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi (BMU) katika Mwalo wa Kunduchi jijini Dar es Salaam, Bw. Zedi Mwinyi Zedi aliipongeza serikali kwa mradi huo na kuahidi kuwa wataulinda maana una manufaa zaidi kwenye shughuli zao za uvuvi, hasa kupata taarifa za uvuvi wanapokuwa baharini.

Dunia inakabiliwa na uchafuzi wa mazingira kutokana na hewa ya ukaa kunakopelekea mataifa mbalimbali kutafuta njia za kukabiliana na hali hiyo ikiwepo kupanda miti na usafi wa mazingira kwa ujumla.

Mtambo huo uliofungwa na TAFIRI unathamani ya zaidi ya Shilingi Milioni 25 za kitanzania na utakuwa unakusanya taarifa kwa njia ya kidigitali kila siku na kuziwasilisha katika kituo kikuu cha utafiti TAFIRI kwa kutumia program maalum.




Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) Dkt. Ishmael Kimirei (Kulia) akifunga mitambo maalum kwa ajili ya kukusanyia taarifa ya mabadiliko ya mazingira katika Bahari ya Hindi katika mwambao wa bahari hiyo jijini Dar es Salaam. (15.10.2021) 


Alhamisi, 21 Oktoba 2021

NARCO YAJENGA MSINGI KUTATUA MIGOGORO YA WAFUGAJI

Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) imefanikiwa kukodisha maeneo kwa ajili ya wafugaji kufuga mifugo yao hali iliyochangia kupunguza migogoro baina ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi, huku ikiahidi kuendelea kushirikiana na wawekezaji wanaotaka kuwekeza katika ranchi hizo.

Akizungumza (13.10.2021) wakati wa kikao cha mwisho cha bodi ya wakurugenzi ya NARCO, mwenyekiti wa bodi hiyo Bw. Paul Kimiti amesema bodi hiyo ambayo imemaliza muda wake baada ya kukaa madarakani kwa miaka mitatu imeweza kwa kiasi kikubwa kusimamia na kuhakikisha wafugaji nchini ambao wana mifugo mingi wanapatiwa maeneo kwa mikataba katika ranchi hizo ili waweze kufuga mifugo yao na kukuza sekta ya mifugo nchini.

“Tumegawa maeneo ya ranchi takriban asilimia 75 na kubakiza asilimia 25 kwa kuwa wafugaji nchini wamekuwa na mifugo mingi na wanahitaji maeneo kwa ajili ya kufuga mifugo yao.” Amesema Bw. Kimiti

Aidha alisema katika kipindi cha miaka mitatu bodi ya wakurugenzi ya NARCO imeweza kuhakikisha maeneo ya ranchi za taifa yanawekewa mipaka ili kuzuia uvamizi wa maeneo hayo na kwamba zoezi hilo linaendelea katika maeneo mengine ambayo bado hayajawekewa alama hizo.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa NARCO Prof. Peter Msoffe alisema bodi ya wakurugenzi ya NARCO ambayo imemaliza muda wake imeweka misingi sahihi katika kufuatilia ukubwa wa maeneo ya ranchi, madeni na mashauri mbalimbali ambayo kwa kiasi kikubwa yameiwezesha NARCO kupata mafanikio zaidi.

Aliongeza kuwa bodi imekuwa ikitoa maelekezo kwa NARCO kuhakikisha inakaa na wawekezaji ambao wamepatiwa vitalu katika ranchi za NARCO na kuona namna ya kuboresha mikataba ili iweze kuzinufaisha pande zote mbili lengo ni kuhakikisha wafugaji wanapata fursa ya kupatiwa vitalu ili kufuga mifugo yao na kulima malisho ya mifugo.

Kwa upande wao baadhi ya wakurugenzi wa bodi ya wakurugenzi ya NARCO ambayo imemaliza muda wake walisema kampuni hiyo imeweza kutatua kwa kiasi kikubwa migogoro baina ya wafugaji na watumiaje wengine wa ardhi kwa kuamua kukodisha vitalu kwenye ranchi za NARCO ili wafugaji waweze kufuga mifugo yao.

Waliongeza kuwa NARCO imekuwa ikifuga mifugo bora ambapo wananchi wanakaribishwa kwenda kununua mifugo hiyo ikiwemo ng’ombe na mbuzi ili kuwa na aina bora ya mifugo inayozalishwa katika ranchi hizo.

Pia wamewaalika wawekezaji kuwekeza katika ranchi za NARCO kwa ajili ya kulima malisho, kujenga majosho na miundombinu mbalimbali ili mifugo inayozalishwa katika ranchi hizo kuongezewa thamani.


Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi ya Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) Bw. Paul Kimiti akifafanua jambo kwa wakurugenzi wa bodi hiyo iliyokaa madarakani kwa miaka mitatu namna ilivyoweza kukodisha maeneo kwa ajili ya wafugaji kufuga mifugo yao hali iliyochangia kupunguza migogoro baina ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi. Kikao hicho kimefanyika katika makao makuu ya NARCO jijini Dodoma. (13.10.2021) 


 

KIWANGO CHA UZALISHAJI MAZAO YA MIFUGO NA UVUVI KIMEONGEZEKA-DKT. TAMATAMAH

Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia kwa katibu Mkuu wa Wizara hiyo anayeshughulikia sekta ya Uvuvi Dkt. Rashid Tamatamah imesema kuwa kiwango cha uzalishaji wa mazao ya mifugo na uvuvi na matumizi yake kimeongezeka ukilinganisha na kile kilichokuwepo  mwaka 2020.

Dkt. Tamatamah ameyasema hayo leo (12.10.2021) wakati akisoma taarifa ya Wizara hiyo kwenye sherehe za ufunguzi wa maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani ambazo kitaifa zimefanyika mkoani Kilimanjaro kwenye Uwanja wa shule ya Msingi Nelson Mandela uliopo eneo la Pasua Manispaa ya Moshi.

“Kiwango cha uzalishaji wa samaki kupitia maji ya asili kwa mwaka 2021 kimefikia takribani tani 372,000 huku uzalishaji wa mazao hayo kwa tasnia ya ufugaji wa samaki  ukifikia takribani tani 20,355  na wastani wa kiwango cha ulaji wa samaki hao kimeongezeka kutoka kilo 8.2 hadi kilo 8.5 kwa mtu kwa mwaka ” Amesema Dkt. Tamatamah.

Akizungumzia kwa upande wa sekta ya Mifugo, Dkt. Tamatamah amesema kuwa kiwango cha uzalishaji wa nyama kimeongezeka hadi tani  738,166  ukilinganisha na  tani 701679 zilizozalishwa mwaka uliopita na kiwango cha uzalishaji wa maziwa kimefikia lita bilioni 3.4 ikilinganishwa na lita bilioni 3.1 zilizozalishwa mwaka uliopita.

Dkt. Tamatamah amebainisha kuwa kuongezeka kwa kiwango hicho cha uzalishaji wa mazao ya mifugo na uvuvi kumetokana na dhamira ya serikali katika kuhakikisha wananchi wanaondokana na uhaba wa chakula na lishe bora hapa nchini.

“Aidha maadhimisho haya ya Siku ya Chakula nchini huwa ni moja ya chachu za kuongeza uzalishaji wa mazao haya ya mifugo na uvuvi kwa sababu hutukumbusha kuwatendea haki wananchi kwa kuhakikisha chakula cha kutosha na chenye ubora kinapatikana na kinalindwa ili kisiharibike kabla au baada ya kuvunwa ili kimfikie mlaji kikiwa salama” Ameongeza Dkt. Tamatamah.

Hata hivyo Dkt. Tamatamah amewasihi wananchi kuendelea kutumia vyakula vinavyotokana na mazao ya mifugo na Uvuvi kwa wingi ili kufikia viwango vilivyowekwa na Shirika la Umoja wa mataifa la Chakula na Kilimo (FAO) ambalo husisitiza  kila mtu kula wastani wa kilo 20.3 za samaki, kilo 50 za nyama na lita 200 za maziwa kwa mwaka.

Maadhimisho ya Siku ya chakula Duniani huadhimishwa kila mwaka kwa lengo la kumkumbusha mwananchi kuzingatia lishe bora wakati wote ili kuondokana na changamoto ya tatizo la  udumavu na kuhakikisha jamii inakuwa na afya bora wakati wote.


Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Dkt. Rashid Tamatamah (kushoto) akimuonesha Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Stephen Kagaigai ukubwa wa samaki wanaoweza kupatikana endapo vitendo vya uvuvi haramu vitadhibitiwa muda mfupi baada ya Kagaigai kufika kwenye banda la maonesho la Mifugo na Uvuvi leo (12.10.2021) ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya kitaifa ya Siku ya Chakula Duniani yanayoendelea kwenye uwanja wa Nelson Mandela, Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro.

 

Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Uzalishaji na Masoko (Wizara ya Mifugo na Uvuvi), Stephen Michael (kulia) akimfafanulia Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Dkt. Rashid Tamatamah kuhusu kuongezeka kwa uzalishaji wa Nyama na Maziwa muda mfupi baada ya Dkt. tamatamah kufika kwenye banda la Kampuni ya Ranchi ya taifa (NARCO) leo (12.10.2021) ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya kitaifa ya Siku ya Chakula Duniani yanayoendelea kwenye uwanja wa Nelson Mandela, Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro, Katikati yao ni Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti, Mafunzo na Ugani Dkt. angelo Mwilawa.