Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki amewataka wataalamu wa mifugo na uvuvi kutoa elimu ya kitaalam kwa wafugaji na wavuvi ili waweze kufuga kwa tija.
Waziri Ndaki aliyasema hayo
leo (27.10.2021) wakati akifungua Mkutano wa 44 wa Wataalam wa Uzalishaji Mifugo
Tanzania (TSAP) wenye kauli mbiu ya Uzalishaji Endelevu wa Mifugo na Samaki
wakati wa janga la UVIKO 19 uliofanyika kwenye ukumbi wa Olasiti Garden
Hotel jijini Arusha.
Kutokana na janga la UVIKO
19, wataalam wametakiwa kuongeza kasi katika utoaji elimu kwa wafugaji na wavuvi
ili kuwapa mbinu bora zitakazowasaidia kuongeza uzalishaji na kuweza kukidhi soko
la nyama na samaki ambalo kwa sasa linazidi kukua kutokana na kufunguka kwa
masoko ya nje ya nchi kutokana na jitihada kubwa zinazofanywa na Mhe. Rais
Samia Suluhu Hassan za kufungua fursa za masoko ya mifugo na samaki nchi za nje
haswa kwenye masoko ya Uarabuni, Ulaya na China.
Pia amewasihi wataalam
walioshiriki mkutano huo kuishauri serikali haswa Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuhusu
namna bora ya kuongeza uzalishaji na kupunguza migogoro ya wafugaji na
watumiaji wengine wa ardhi. Waziri Ndaki amesema kuwa Wizara itaendeleza jitihada
za kuhakikisha kuna kuwa na mazingira bora ya kufuga, kusindika na kufanya
biashara ya mazao ya mifugo na uvuvi.
Lakini pia Waziri Ndaki amewasisitiza
wafugaji kuendelea kununua maeneo kihalali kwa ajili ya shughuli za ufugaji na
kuhakikisha wanayapima na kuyamiliki ili waondokane na migogoro. Vilevile
amewasisitiza kuendelea kupanda malisho katika maeneo watakayoyamiliki ili kuondokana
na tatizo la malisho kwa mifugo.
Naye Mwenyekiti wa Chama
hicho cha TSAP, Dkt. Daniel Komwihangilo alisema lengo la chama hicho ni kuhimiza
maendeleo katika sayansi ya uzalishaji na uendelezaji wa mifugo hapa nchini,
kutoa fursa kwa wadau wote wa tasnia ya mifugo kukutana ili kubadilishana
mawazo na uzoefu, na kushirikiana na wataalam na wanachama wa waliopo katika
vyama vya taaluma chini katika sekta ya mifugo na uvuvi ili kuendeleza sekta
hizo. Chama hicho kwa sasa kina wanachama zaidi ya 300 ambao wapo hai kutoka
katika sekta mbalimbali.
Aidha, amemuomba Waziri kuangalia uwezekano wa kuunda chombo maalum cha kutambua na kuisimamia kada hiyo kisheria. Vilevile amemshukuru Waziri kwa ushirikiano anaoutoa katika kusimamia sekta ya mifugo na uvuvi na kwamba wao kama chama wataendelea kutoa ushirikiano kwa serikali katika kuhakikisha uzalishaji unaongezeka.
Mkurugenzi wa Idara ya
Utafiti, Mafunzo na Huduma za Ugani, Dkt. Angello Mwilawa akiwasalimia wajumbe
wa Mkutano wa 44 wa Wataalam wa Uzalishaji Mifugo Tanzania ambapo pia alisema mkutano
huo unawasaidia wataalam kutoka maeneo tofauti kubadilishana uzoefu. Mkutano huo
umefanyika katika ukumbi wa Olasiti Garden Hotel Jijini Arusha. (27.10.2021)
Mwenyekiti wa Chama cha
Wataalam wa Uzalishaji wa Mifugo Tanzania, Dkt. Daniel Komwihangilo akitoa
maelezo mafupi kuhusu chama hicho kwenye Mkutano wa 44 wa chama hicho ambapo
amesema moja ya malengo yake ni kuhimiza maendeleo katika sayansi ya uzalishaji
na uendelezaji wa mifugo hapa nchini. Mkutano huo umefanyika katika ukumbi wa
Olasiti Garden Hotel Jijini Arusha. (27.10.2021)
Msajili wa Bodi ya Maziwa
nchini ambaye pia ni Katibu Msaidizi wa TSAP, Dkt. George Msalya akiwatambulisha
wajumbe walioshiriki Mkutano wa 44 wa Wataalam wa Uzalishaji Mifugo Tanzania
kwa mgeni rasmi Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki. Mkutano huo
umefanyika katika ukumbi wa Olasiti Garden Hotel Jijini Arusha. (27.10.2021)
Wajumbe wa Mkutano wa 44 wa Wataalam
wa Uzalishaji Mifugo Tanzania wakifuatilia mada zilizokuwa zikiwasilishwa
katika mkutano huo uliofanyika kwenye ukumbi wa Olasiti Garden Hotel Jijini
Arusha. (27.10.2021)
Waziri wa Mifugo na Uvuvi,
Mhe. Mashimba Ndaki (kulia) akipokea zawadi ya maziwa kutoka kwa wawakilishi wa
Kampuni za Kilimanjaro Fresh na Asas Dairies Ltd mara baada ya kumaliza
kufungua Mkutano wa 44 wa Wataalam wa Uzalishaji Mifugo Tanzania uliofanyika
katika ukumbi wa Olasiti Garden Hotel Jijini Arusha. (27.10.2021)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni