Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amesema Serikali ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imejipanga kuhakikisha Dagaa wa Kigoma wanakuwa ni zao la kimkakati kibiashara litakalokwenda kuvutia uwekezaji na kusisimua uchumi wa mtu mmoja mmoja na nchi kwa ujumla.
Ulega aliyasema hayo wakati akiongea na Wadau wa Uvuvi alipofanya kikao nao katika Mwalo wa Katonga uliopo Mkoani Kigoma Oktoba 17, 2021.
Alisema kuwa serikali imejipanga kufanya zao la dagaa wa Kigoma kuwa la kimkakati kwa sababu biashara ya dagaa inahusisha watu wengi katika jamii, hivyo kuiimarisha biashara hiyo ni kuwaimarisha wananchi kiuchumi.
"Sisi Serikali tunataka kuinua biashara ya dagaa wa Kigoma, tunataka wavuvi wainuke kiuchumi, na tumejipanga kuondoa vikwazo vyote vinavyowasumbua na tutalitangaza vyema zao hili ili kuvutia uwekezaji zaidi hapa Kigoma," alisema Ulega
Pia, Naibu Waziri Ulega aliwataka Viongozi wa Mkoa huo kuanza mikakati na kampeni maalum kwa ajili ya kutangaza ubora wa dagaa wa Kigoma ili kuvutia uwekezaji wa viwanda vidogovidogo na vikubwa kwa ajili ya kuchakata dagaa hao.
Aliendelea kusema kuwa zao hilo la dagaa likitangazwa vizuri, wawekezaji na Taasisi za kibenki wote watakwenda kuwekeza na ndio itakuwa mwisho wa dagaa wa Kigoma kutupwa tupwa hovyo kwa sababu ya kukosa soko.
Aidha, aliongeza kwa kusema kuwa uvunaji wa dagaa hao uendane sambamba na utunzaji wa mazalia ya samaki ili upatikanaji wa rasilimali hiyo uwe wa uhakika wakati wote.
"Ndugu zangu, mkakati huu wa kuinua biashara ya zao la dagaa hautafanikiwa kama malighafi haitakuwepo, ili viwanda viweze kuanzishwa ni lazima malighafi ipatikane ya kutosha," alisistiza Ulega
Alisema Serikali imejipanga kuwawezesha wavuvi vifaa mbalimbali vitakavyowasaidia kuvuna dagaa kwa uhakika na kuwakausha kwa kutumia vichanja vya kisasa ili kupunguza upotevu wa dagaa na kuongeza ubora wake.
Naye, Diwani wa Kata ya Bangwe, Hamisi Besete alisema Serikali kwa Sasa inapoteza mapato mengi kwa sababu Mwalo wa Katonga haujajengwa hivyo kuwafanya wafanyabiashara wa Samaki na Dagaa kukosa sehemu ya kuuzia.
"Mhe. Naibu Waziri, Mwalo wa Katonga ni mkubwa sana hapa Kigoma, tunaomba mtujengee mwalo huu ili Serikali iweze kukusanya mapato ya kutosha hapa kutokana na biashara ya mazao ya Uvuvi, sasa hivi mapato yanapotea kwa sababu Wafanyabiashara hawana sehemu rasmi ya kuuzia samaki wao," alisema Besete
Mbunge wa Kigoma Mjini, Kilumbe Ngenda nae alisema kuwa kwa sababu sasa nchi inaelekea katika uchumi wa buluu ambao unataka kuongezeka kwa kasi ya uzalishaji katika Bahari na Maziwa ili kukuza uchumi wa nchi, Serikali ione uwezekano wa kupunguza baadhi ya masharti ili wananchi wengi waweze kuingia katika uchumi wa buluu.
Naibu Waziri wa Mifugo na
Uvuvi, Abdallah Ulega (kulia) akimpa maelekezo Afisa Mfawidhi, Usimamizi wa
Rasilimali za Uvuvi Kanda Kuu ya Tanganyika, Juma Makongoro wakati wa Mkutano
na Wavuvi wanaofanya shughuli zao katika Mwalo wa Katonga uliopo Mkoani Kigoma
Oktoba 17, 2021.
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega akieleza ubora
wa dagaa wa Kigoma alipotembelea Mwalo wa Katonga uliopo Mkoani Kigoma
kuangalia namna Wavuvi wanavyokausha dagaa hao katika vichanja.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni