Serikali imeombwa kusitisha uchinjaji na uuzaji wa ngozi na malighafi zitokanazo na punda katika machinjio ya Shinyanga na kuwachukulia hatua watu wote waliobainika kukiuka haki za wanyama.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Shirika la Ulinzi na Utetezi wa haki na Ustawi wa Wanyama Arusha (ASPA) Bw. Livingstone Masija leo Agosti 6, 2021 Jijini Dodoma mbele ya Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel baada ya ukaguzi uliofanyika juni 20 mwaka huu na kubaini ukiukwaji mkubwa wa haki za mnyama punda kwa kuwafanyiwa mateso makubwa.
Alisema, miongoni wa vitendo vinavyofanyika ni pamoja na kuwakosesha malisho kwa muda mrefu, kuchinja punda walio na mimba, kuchinja punda wakati wengine wanawaangalia na kuwapiga na vitu vizito kichwani pindi mashine zimeharibika na kukaa na majeraha bila ya kutibiwa.
“kwa sababu watu wako pale wameaminiwa na Serikali lakini namna ya utekelezaji wao wa majukumu ni shida, wameambiwa wasimamie punda wachinjwe 20 kwa siku lakini wao wako pale sijajua wanakuwa hawaoni au hawako kazini basi unakuta punda wanachinjwa zaidi ya walioambiwa wasimamie, tunaomba pia wachukuliwa hatua za kinidhamu” alisema Masija
Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel alisema kuwa serikali imepokea wasilisho hilo na italifanyia kazi haraka iwezekanavyo kwa mujibu wa sheria kwa sababu lengo la Wizara ni kuona kuwa wanyama kazi wanaendelea kulindwa.
Alisema mpaka juni 30, 2020 idadi ya punda ilikuwa ni 657,380 kwa hiyo endapo wangefata utaratibu wa kuchinja punda 20 kwa siku kama maelekezo ya Serikali yalivyo Punda hao wangeishi kwa miaka 50 kama wazaliaji.
“nimesema tuna taratibu zetu sasa za kisheria ambazo ndani ya Wizara tutazitumia ili kuhakikisha tunasonga mbele nanyi mtaendelea kupewa taarifa kupitia Ofisi ya Mkurugenzi wa huduma za Mifugo kwamba nini kinaendelea”. Alisema.
Aliongeza kuwa lengo la serikali si kufanya punda waishe bali kuongezeka lakini pia swala la punda kutoka nje ya nchi ni jambo lingine ambalo ni kosa kisheria kwa sababu serikali inapoteza mapato, kwa hiyo suala hilo litaangaliwa kwa umakini.
Naye Msajili wa Baraza la Veterinari Tanzania, Dkt. Bedan Masuruli amemshukuru Katibu Mkuu kwa kutenga muda wake na kuja kuwasikiliza wadau wa ustawi wa wanyama na wamekusikia vizuri na kwamba Wizara imelichukua.
Katibu Mkuu Wizara ya
Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel akiongea na wadau (hawapo
pichani) kwenye kikao cha mapendekezo ya usitishaji wa shughuli za uchinjaji
punda uuzaji wa ngozi na malighafi nyinginezo zinazotokana na punda leo Agosti
6, 2021 Jijini Dodoma.*
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo)
Prof. Elisante Ole Gabriel (kushoto), akiangalia video pamoja na wadau ya
namna haki za punda zinavyokiukwa kwenye kampuni ya Fang Huo Investment Co. Ltd
leo Agosti 6, 2021 Jijini Dodoma.
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo),
Prof. Elisante Ole Gabriel (Waliokaa katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na
wawakilishi kutoka Shirika la Ulinzi na Utetezi wa Haki na Ustawi wa Wanyama
Arusha (ASPA) pamoja na watumishi wa Wizara hiyo mara baada ya kikao cha
mapendekezo ya usitishaji wa shughuli za uchinjaji punda, uuzaji wa ngozi na
malighafi nyinginezo zinazotokana na punda katika machinjio ya Shinyanga leo
Agosti 6, 2021 Jijini Dodoma.*
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni