Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeiomba Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) kuwasaidia wavuvi katika mambo matatu ikiwemo kuwaondoa wavuvi kutoka kwenye uvuvi wa maji ya ndani na kuwapeleka kuvua kwenye maji ya Kitaifa kwa kutumia maboti ya kisasa badala ya mitumbwi na ngalawa.
Ombi hilo lilitolewa na
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Dkt. Rashid Tamatamah alipokuwa
akiongea na ujumbe kutoka Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) wakiongozwa na
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo, Bw. Frank Mugeta, alisema uvuvi wa samaki katika ukanda wa
bahari unaweza kuongezeka iwapo wataweza kuwasaidia wavuvi katika mambo
mbalimbali.
Pia, kuwaondoa wavuvi
wadogo wadogo kutoka kwenye uvuvi wa
maji ya ndani na kuwapeleka kuvua kwenye maji ya Kitaifa kwa kutumia maboti
ya kisasa badala ya mitumbwi na ngalawa ambazo wengi wao bado wanazitumia.
“Sasa Wizara ya Mifugo na
Uvuvi kwa kushirikiana na sekta binafsi imeanza kutekeleza baadhi ya mikakati
kuwawezesha wafugaji samaki wadogo kwenye maji ya asili kukabilina na changamoto
za uwekezaji mdogo katika maeneo yao
lakini hapo bado tuna changamoto,”alisema.
Alisema mafanikio katika
utekelezaji wa mikakati yanategemea kwa
kiasi kikubwa ushiriki wa Taasisi za
kifedha za ndani pamoja na nje.
Alisema Wizara imeanzisha dawati
la sekta binafsi ili kuratibu upatikanaji wa mikopo kwa vyama vya ushirika kwa
kuyafanyia marekebisho maandiko yao ili yakidhi matakwa ya Kibenki.
“Kufikia Februari 2021,
dawati limewezesha kupokelewa kwa maombi ya mikopo ya uvuvi katika Benki ya TADB yenye
thamani ya shilingi bilioni 51.4 lakini
kiasi kilichotolewa hadi sasa ni shilingi bilioni 1.2 kwa vyama vya ushirika
vitatu katika Wilaya ya Ukerewe, Buchosa
na Chato,”alisema.
Kwa upande wa Mkurugenzi
Mtendaji wa TADB, Bw. Mugeta amesema mara baada ya kikao hicho wataenda
kuangalia namna ya kuisaidia sekta hiyo ambayo inaajiri watanzania wengi.
Alisema wataisaidia sekta
hiyo kutokana na kufanyika kwa tafiti
nyingi ambazo zitawaongoza wao wasaidie sehemu zipi ili kuhakikisha Mtanzania
anaweza kujikwamua kimaisha.
“Niahidi wataalam wetu watakaa, hili ni eneo la kusapoti kwa nguvu zetu zote nimeteuliwa nina siku 10 bado nina nguvu hivyo tutapata majawabu ya haraka ili tuone tunaanzia wapi.Tunataka kuhakikisha sekta ya uvuvi inaajiri watu wengi nafikiri ni eneo ambalo tutaliangalia kwa kina zaidi,”alisema.
Awali akitoa wasilisho
kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Mkurugenzi wa Ukuzaji viumbe maji kutoka
Wizara hiyo, Dkt. Nazael Madalla alisema uvuvi ni miongoni mwa sekta
zinazoajiri watu wengi wa kipato cha chini ambapo moja kwa moja takribani
wavuvi na wakuzaji viumbe maji wapatao
225,435.
Alisema zaidi ya watanzania
milioni 4.5 wameendelea kupata kipato cha kila siku kutokana na shughuli
zinazohusiana na sekta ya uvuvi ikiwemo kuunda na kutengeneza boti, kuuza na
kushona nyavu kutengeneza na kuuza
barafu, biashara ya samaki na mazao yake.
Mkurugenzi huyo alisema
sekta hiyo inachangia katika lishe na usalama wa chakula ambapo takribani
asilimia 30 ya protein itokanayo na wanyama inachangiwa na samaki.
Alisema kwa upande wa
kipato na fedha za kigeni katika mwaka 2020-2021 tani 483,756.4 zilivunwa na
kuingiza kipato cha shilingi trilioni 2.42 kati ya mavuno hayo tani 41,319.00
na samaki hai wa mapambo 165,413 wenye thamani ya shilingi bilioni 18.91.
Mkurugenzi huyo amesema
sekta hiyo ni muhimu kwani inachangia
pato la Taifa kwa asilimia 1.7
Alisema kwa sasa kiasi cha
rasilimali za samaki kwenye maji ni
zaidi ya tani nne ambapo amedai kiasi kinachoweza kuvunwa bila kuathiri mazingira ni tani 750,000.
Katibu
Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah akieleza lengo
la kufanya kikao na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania
(TADB), Bw. Frank Mugeta (hayupo pichani) ikiwa ni pamoja na kuomba kuwasaidia wavuvi kupata
mikopo Ili kuweza kutatua changamoto zao katika masuala ya Uvuvi kwenye
ukumbi wa NBC Jijini Dodoma. Agosti 16, 2021.
Mkurugenzi
Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), Bw. Frank Mugeta
akielezea namna watakavyoweza kuiendeleza Sekta ya Uvuvi kwa kuwapatia wavuvi
mkopo Ili waweze kujiendesha kwenye shughuli zao za Uvuvi kwenye ukumbi wa
NBC Jijini Dodoma. Agosti 16, 2021.
Mkurugenzi
wa Ukuzaji viumbe maji kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt Nazael Madalla,
akiwasilisha mada wakati wa kikao na wajumbe kutoka Benki ya maendeleo ya
kilimo Tanzania (TADB) kwenye ukumbi wa NBC Jijini Dodoma. Agosti 16, 2021.
Katibu
Mkuu Sekta ya Uvuvi Dkt. Rashid Tamatama, (waliokaa kulia) akiwa kwenye picha ya pamoja mara baada ya kukutana na
wajumbe kutoka Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) lengo likiwa
ni kuwasaidia Wavuvi kukabiliana na
changamoto za uwekezaji mdogo katika maeneo yao pamoja kuvipatia vyama vya
ushirika vya uvuvi mikopo ili viweze kujiendesha kwenye ukumbi wa NBC Jijini
Dodoma.