Katibu Mkuu, Wizara ya
Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel amekutana na Ujumbe kutoka
nchini Saudi Arabia kwa lengo la kuweka mazingira mazuri ya kufanya biashara ya
nyama na nchi hiyo.
Prof. Ole Gabriel alikutana
na Ujumbe huo kutoka Saudi Arabia ulioongozwa na Mkaguzi, Mamlaka ya Dawa na Chakula, Saudi Arabia,
Ahmed Alhajouj jijini Dar es Salaam Agosti 7, 2021.
Kwa mujibu wa Prof. Gabriel
kabla ya kukutana nao, ujumbe huo ulipata fursa ya kukagua maeneo mbalimbali
yanayohusika na uchakataji wa mazao ya mifugo ikiwemo Machinjio, Maabara na
Shirika la Viwango Tanzania(TBS) ambapo kote wamejirisha na kutoa mapendekezo
kadhaa ya kuboresha ili biashara hiyo iweze kufanyika kwa viwango
vinavyohitajika na nchi hiyo.
Alisema kuwa Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ameielekeza Wizara hiyo
kutafuta masoko nje ya nchi hivyo Wizara inaendelea kufanya jitihada ikiwemo
hatua hiyo ya kutafuta soko katika nchi Saudi Arabia.
"Haya masoko ya nje ya
nchi ni mazuri kwa sababu yanatupatia fedha za kigeni lakini pia
yanawahakikishia wafugaji wetu soko la uhakika kwa mazao ya mifugo yao,"
alisema Prof. Ole Gabriel
Aidha, Prof. Gabriel alitoa
rai kwa Wafugaji nchini kuchukulia hatua hiyo kama ni fursa kubwa na hivyo
wahakikishe wanaboresha ufugaji wao kuwa wa kisasa zaidi ili kukidhi soko hilo
la kimataifa.
"Serikali ni rahisi
kutafuta masoko lakini je, mifugo iliyopo inakidhi soko hilo? hivyo niwaombe
wafugaji na Wafanyabiashara watumie fursa hii vizuri ili kuboresha uchumi wao
na wa Taifa pia," aliongeza Prof. Ole Gabriel
Alisema Sekta ya Mifugo kwa
sasa inachangia katika pato la Taifa kwa asilimia 7.4 lakini lengo la Wizara ni
kufikia asilimia 15 ifikapo mwaka 2025 na hilo linawezekana kama milango ya
masoko nje ya nchi ikianza kufunguka kwa
uhakika.
Prof. Ole Gabriel aliongeza
kuwa wao kama wizara watatoa ushirikiano kwa kila mdau anayechangia katika
mnyororo wa thamani wa mazao ya mifugo kuhakikisha kunakuwa na mazao bora kwa
ajili ya soko la ndani na la nje.
Naye, Msajili wa Bodi ya
Nyama, Dkt. Daniel Mushi alisema anaishukuru Serikali kwa jitihada mbalimbali
inazozifanya kwa kushirikiana na wadau kufungua masoko mengine nje ya nchi ili
kuuza nyama katika masoko yanayolipa bei nzuri.
Aliongeza kuwa ujio wa
ujumbe huo umewapa changamoto kwani kuna mambo wanapaswa kufanya ili nyama ya
Tanzania iweze kukubalika katika masoko ya nje.
Aliendelea kusema kuwa ili
waweze kufikia masoko hayo ni lazima kuboresha lishe ya mifugo ili wanyama waweze
kukua kwa haraka na ambao watakuwa na nyama nyingi yenye ubora.
Itakumbukwa hivi karibuni,
Rais Samia alikutana na Mtoto wa Mfalme wa Saudi Arabia ambapo miongoni mwa
maeneo yaliyoangaliwa ni pamoja na Sekta ya Mifugo na aliielekeza Wizara
kutafuta masoko nje ya nchi ikiwemo nchi ya Saudi Arabia.
Katibu
Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel (katikati-
mstari wa mbele) akiwa katika picha ya pamoja na Ujumbe kutoka nchi ya Saudi
Arabia uliokuja nchini kwa lengo la kuweka mazingira mazuri ya kufanya biashara
ya Nyama na Tanzania. Wa pili kutoka kulia ni Mkaguzi, Mamlaka ya Dawa na
Chakula, Saudia Arabia, Ahmed Alhajouj. Ujumbe huo ulikutana na Prof. Ole
Gabriel jijini Dar es Salaam leo Agosti 7, 2021. Wengine katika picha ni Maafisa
waliombatana na Mkaguzi huyo pamoja na
Viongozi mbalimbali kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni