Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki ameagiza eneo la shamba la uzalishaji mifugo lililopo wilayani Misungwi mkoani Mwanza kulindwa na Suma JKT, Polisi pamoja na kujengewa fensi (uzio) ili kuimarisha ulinzi na usalama wa eneo hilo.
Hii ni baada ya Waziri huyo
kufanya ziara jana ya kutembelea shamba la Mabuki pamoja na taasisi zilizomo
ndani yake ambapo alielezwa kuwepo kwa uchungaji haramu na uchomaji moto pamoja
na tishio la usalama kwa wanafunzi na watumishi katika shamaba hilo.
Ndaki amesema,eneo hilo ni
kubwa na lipo wazi kwa hali hiyo siyo
salama kila mtu anaweza kuingia na kufanya jambo lolote hivyo waangalie
uwezekano wa kuweka fensi ili mtu atakaye bomoa na kuingia itakuwa rahisi
kumdhibiti.
Amesema,eneo hilo linapaswa
kulindwa na Suma JKT,hivyo alimuagiza Mkurugenzi wa Utafiti ,Mafunzo na Ugani
kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi
Dkt.Angello Mwilawa pamoja na uongozi wa kituo hicho kukaa pamoja na kuangalia
ni walinzi wa ngapi wanahitajika kwa ajili ya ulinzi wa shamba hilo.
Pia amesema katika suala la
kuwalipa Suma JKT ni lazima taasisi hizo na wizara kukaa Pamoja kuangalia namna
ambayo watakuwa wanawalipa ili kusiwe na sababu yoyote itayositisha ulinzi huo
pindi utakapoanza.
Aidha, katika kuimarisha
zaidi ulinzi wa eneo hilo amemuomba Mkuu wa Wilaya ya Misungwi awapatie Askari
Polisi ambao watakuwa wanafanya kazi kwa kushirikiana na SUMA JKT lengo likiwa
ni kuhakikisha eneo hilo linakuwa salama.
"Hatuwezi kuangalia wanafunzi
na watumishi wapo hatarini,halfu sisi tunanyoosha mikono na kusema Mungu
tusaidie na vitendo vya waangalizi wa ng'ombe,wanafunzi na watumishi kupigwa
siyo sawa hivyo,tutafute pesa popote fensi ijengwe kama mwanzo,eneo hili
lilindwe na Suma JKT na Polisi ili wavamizi wajue kuwa linalindwa,"
amesema Ndaki.
Awali Kaimu Meneja wa Wakala
wa Mafunzo ya Mifugo (LITA) kampasi ya Mabuki Joel Ngogo,akisoma taarifa kwa
Waziri huyo, amesema Juni 9,2020 wanafunzi wao wakiwa shambani kukata fito za kujengea uzio wa ng'ombe
walivamiwa,walipigwa na jaribio la kutaka kubakwa mwanafunzi mmoja wa kike ambaye aliokolewa na watu waliopita
eneo hilo.
Ngogo amesema, Aprili 23, mwaka
huu matukio ya wanafunzi kuvamiwa na kupigwa kwa kombeo wakiwa eneo la kantini (mgahawa)
wakipata chakula yalirudiwa na wavamizi wanaodhaniwa kutumwa na wafugaji ambao
mifugo yao ilikamatwa na uongozi wa shamba hilo.
Amesema katika kutatua
changamoto hiyo alimuomba Waziri kusaidia kuoata ulinzi thabiti kwa kutumia
makampuni ya ulinzi kwa kushirikiana na jeshi la Polisi.
Kwa upande wake Meneja wa
shamba la uzalishaji mifugo Mabuki Lini Andey Mwalla,amesema wamekuwa
wakikabiliwa na changamoto ya uchungaji haramu wa mifugo ya wananchi kutoka
sehemu mbalimbali.
Hali hiyo imekuwa ikivuruga
malengo yaliyokusudiwa na serikali na kusababisha athari ikiwemo kueneza
magonjwa ya virusi na yaenezwayo na kupe hivyo kusababisha vifo vingi vya
mifugo vitokanavyo na magonjwa kama ndigana kali na mengineyo.
Pia amesema,suala la uchomaji
moto hususani kipindi cha kiangazi kinachofanywa na watu ambao bado
hawajawabaini kutokana na mbinu wanazotumia wahusika limekuwa likisababisha
uharibifu wa mazingira na hivyo mifugo kukosa malisho.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki akizungumza na wanafunzi wa LITA Mabuki wakati alipowatembelea kwa lengo la kuona maendeleo yao ya kielimu ambapo amewataka wasome kwa bidii ili waje wajiajiri na sio kutegemea ajira kutoka serikalini. (14.07.2021)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni