Nav bar

Jumatano, 28 Julai 2021

SERIKALI KUENDELEA KUSHIRIKIANA NA AAT

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki amewaeleza viongozi wa Chama cha Ukuzaji Viumbe Maji Tanzania (AAT) kuendelea kushirikiana na serikali ili kuongeza uzalishaji wa viumbe hao.

 

Waziri Ndaki ameyasema hayo leo (27.07.2021) ofisini kwake jijini Dodoma wakati alipotembelewa na viongozi wa AAT waliokuwa na lengo la kujitambulisha na kumuelezea mpango mkakati wao wa miaka mitano pamoja na namna walivyojipanga kushirikiana na serikali katika kufanikisha malengo yaliyowekwa na wizara.

 

Wizara inayo malengo ya kuongeza uzalishaji katika eneo la ukuzaji viumbe maji ili kuhakikisha uzalishaji huu una kuwa sawa na ule wa maji ya asili. Kwa kufanya hivi uzalishaji wa samaki hapa nchini utakuwa umeongezeka na hivyo kusaidia kukuza uchumi kupitia sekta ya uvuvi.

 

Aidha, amewaeleza viongozi hao kuwa wizara itaendelea kushirikiana na AAT katika kazi wanayoifanya kwa kuwa malengo ya serikali ni kushirikiana na sekta binafsi katika kukuza uchumi kupitia sekta ya uvuvi, huku akiwapongeza kwa jitihada mbalimbali ambazo tayari wameshazifanya katika kukuza uzalishaji wa viumbe maji hapa nchini.

 

Naye mwenyekiti wa Chama cha Ukuzaji Viumbe Maji Tanzania, Dkt. Charles Mahika amemshukuru waziri kwa utayari wake katika kuwapokea pamoja na kuwaahidi kuwapa ushirikiano katika jitihada wanazozifanya.


Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki akiwa kwenye picha ya pamoja na Mwenyekiti wa Chama cha Ukuzaji Viumbe Maji Tanzania, Dkt. Charles Mahika (wa pili kutoka kulia), Mkurugenzi wa Idara ya Ukuzaji Viumbe Maji (WMUV), Dkt. Nazael Madala (kulia) na Katibu wa Chama cha Ukuzaji Viumbe Maji, Bw. Geophrey Rucho mara baada ya kumaliza mazungumzo yao ambapo Waziri Ndaki amewapongeza kwa kazi wanayoifanya na kuwa ahidi kuwa wizara itaendelea kuwapa ushirikiano. (27.07.2021)

NARCO YAELEKEZWA KUIPATIA KITALU KAMPUNI YA CHOBO

NARCO YAELEKEZWA KUIPATIA KITALU KAMPUNI YA CHOBO

 

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki ameielekeza Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) kuipatia Kampuni ya Chobo Kitalu Mbadala katika eneo la Mradi wa Mwisa II lililopo Wilayani Muleba, Mkoani Kagera baada ya kuchelewa kuendeleza Kitalu cha awali alichopewa katika Ranchi ya Mabale na kupelekea wawekezaji wengine kutumia eneo hilo.

 

Ndaki alitoa agizo hilo alipokutana na mwekezaji huyo jijini Dodoma Julai 27, 2021 na kukubaliana kuwa Wizara itampatia eneo lingine katika mradi wa Mwisa II ili aweze kuendeleza uwekezaji katika sekta ya mifugo.

 

Kufuatia makubaliano hayo, Waziri Ndaki ameielekeza NARCO kushughulikia jambo hilo kwa haraka ili mwekezaji huyo aweze kuendelea na shughuli zake za uwekezaji nchini.

 

“Kama nilivyosema sisi tuko tayari kushirikiana na Chobo pamoja na wawekezaji wengine kwa lengo la kuongeza tija kwenye sekta ya mifugo ili kutimiza malengo ya Tanzania ya Viwanda,” alisema Ndaki

 

Naye, Mkurugenzi wa Kampuni ya Chobo, John Chobo pamoja na kumshukuru Waziri kwa hatua hiyo, alisema kuwa uamuzi huo utasaidia kiwanda chake kupata malighafi iliyobora kutoka kwa mifugo watakayoiwekeza katika eneo hilo na anaamini kwa ushirikiano wanaopata kutoka kwa NARCO na Wizara wataweza kuzalisha bidhaa bora itakayoweza kushindana katika Soko la Kimataifa.

 

Aliongeza kuwa kiwanda chake cha kuchakata nyama ni kikubwa na kina uwezo wa kuchinja ng’ombe 600 na mbuzi 1500 kwa masaa nane, hivyo kupitia uwekezaji huo kampuni yake itaweza kutengeneza mnyororo wa thamani utakaoweza kufaidisha maelfu ya Watanzania.

 

Julai 9, 2021 Waziri Ndaki alipokuwa katika ziara Mkoani Kagera alimtaka mwekezaji huyo kukubali kuachia Kitalu cha Mabale ili kuepusha mgogoro uliopo baina yake na wawekezaji wengine ambao wanatumia eneo hilo alilokabidhiwa awali na kumuahidi kuwa pindi atakapokuwa tayari kuwekeza Wizara itampatia eneo lingine ambalo litakuwa zuri zaidi kwa uwekezaji wake.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki (kulia) akifurahia jambo na Mkurugenzi wa Kampuni ya Chobo, John Chobo (kulia) wakati akiagana nae baada ya kumaliza kikao chao kilichofanyika jijini Dodoma Julai 27, 2021. Katikati ni Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki (kulia) akiongea na Mkurugenzi wa Kampuni ya Chobo, John Chobo (kushoto) muda mfupi baada ya kumaliza kikao chake  kilichoshirikisha Mkurugenzi huyo wa Kampuni ya Chobo, Viongozi wa Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) na  wadau wengine kilichofanyika jijini Dodoma Julai 27, 2021. Katika kikao hicho Waziri Ndaki aliielekeza Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) kuipatia  Kampuni hiyo Kitalu katika eneo la Mradi wa Mwisa II lililopo Wilayani Muleba, Mkoani Kagera ili iweze kuendeleza shughuli za uwekezaji katika sekta ya mifugo kwa lengo la kuiwezesha nchi kufikia uchumi wa Viwanda.


Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki (katikati mstari wa mbele) akiwa katika picha ya pamoja na Mkurugenzi wa Kampuni ya Chobo, John Chobo (kulia kwake) baada ya kumaliza kikao chao  jijini Dodoma Julai 27, 2021. Kushoto kwake ni Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel. Wengine ni Maafisa kutoka Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO).

Jumamosi, 24 Julai 2021

WATENDAJI SEKTA ZA MIFUGO NA UVUVI WAWEKWA KITIMOTO

Na Mbaraka Kambona,


Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki amewataka Watendaji wanaofanya kazi ya ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali katika Minada, Mialo na Vituo vya Ukaguzi kufanya kazi hiyo kwa uaminifu na uadilifu huku akionya kuwa hawataweza kuendelea kuwa na Mtendaji atakayejihusisha na vitendo vinavyosababisha upotevu wa mapato ya Serikali.


Waziri Ndaki aliyasema hayo katika kikao cha Tathmini ya Ukusanyaji wa Maduhuli ya Serikali kwa mwaka uliopita na kuweka malengo mapya ya ukusanyaji mapato kwa mwaka 2021/ 2022 kilichofanyika jijini Dodoma Julai 23, 2021.


Akiongea na Watendaji hao aliwaeleza bayana kuwa ili waweze kufikia malengo ya kukusanya Shilingi Bilioni 90 walizojiwekea kukusanya kwa mwaka huu wa fedha ni lazima wafanye kazi hiyo kwa uaminifu na uadilifu kinyume na hapo hawatafanikiwa kufikia malengo.


"Katika kipindi ambacho nimekuwa hapa Wizarani nimepata taarifa nyingi kuhusu baadhi yenu kujihusisha na vitendo vya upotevu wa mapato, acheni kufanya hivyo kwa sababu tukikugundua hatutaweza kuendelea na wewe," alisema Ndaki


Aliongeza kuwa kumekuwa na vitendo vingi vya upotevu wa maduhuli ya Serikali ambavyo  vimekuwa vikifanywa na baadhi ya maafisa  wasiokuwa waaminifu na  kupelekea serikali kutopata mapato yanayostahili.


Waziri Ndaki aliendelea kusema kuwa Mhe. Rais, Samia Suluhu Hassan amewaahidi Watanzania mambo mengi mazuri na  ili mambo hayo yaweze kutekelezeka yanahitaji pesa, na miongoni mwa pesa zinazotegemewa na Serikali ni pamoja na zile zinazokusanywa kutoka kwenye minada, mialo na vituo vya ukaguzi.


Aliendelea kubainisha kuwa kwa mwaka huu atafuatilia kwa karibu utendaji kazi wa watendaji hao na amepanga kukutana nao kila robo mwaka ili kupima utendaji kazi wa kila mmoja ili kuona kama yale malengo yaliyowekwa yanafikiwa.


"Nitaendelea kuwatembelea katika vituo vyenu vya kazi, nitakuja kwa taarifa na wakati mwingine bila taarifa na nikifika nitataka kujua mmefikia wapi kuhusu ukusanyaji wa maduhuli," alisisitiza Ndaki


Aidha, Waziri Ndaki aliwaelekeza Watendaji hao kupelekea taarifa ya minada isiyo rasmi ili aitambue na kuifuta  kwa sababu imekuwa ni kikwazo kwa minada inayotambulika kisheria.


 Pia aliwasisitiza Watendaji hao kuendelea kufanya kazi ya Serikali kwa haki ikiwa ni pamoja na kuzuia uvuvi haramu na utoroshaji wa mifugo kwani vitendo hivyo vimekuwa ni sehemu ya upotevu wa mapato ya Serikali.




Kaimu Mkurugenzi, Uzalishaji na Masoko (Mifugo), Steven Michael akifafanua jambo katika kikao cha Tathmini ya Ukusanyaji wa Maduhuli kwa mwaka uliopita na kuweka malengo ya ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali kwa mwaka mpya wa fedha 2021/ 2022 kilichofanyika jijini Dodoma Julai 23, 2021.


Afisa Mfawidhi Msimamizi wa Rasilimali za Uvuvi Kanda Kuu ya Tanganyika, Juma Makongoro akitoa maoni yake katika kikao cha Tathmini ya Ukusanyaji wa Maduhuli kwa mwaka uliopita na kuweka malengo ya ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali kwa mwaka mpya wa fedha 2021/2022 kilichofanyika jijini Dodoma Julai 23, 2021.


Afisa Tehama, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Baltazari Kibola akitoa ufafanuzi kuhusu mifumo ya kielekroniki ya kukusanyia maduhuli ikiboreshwa vizuri inavyoweza kusaidia kutatua changamoto ya upotevu wa maduhuli ya Serikali katika kikao cha Tathmini ya Ukusanyaji wa Maduhuli kwa mwaka uliopita na kuweka malengo ya ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali kwa mwaka mpya wa fedha 2021/2022.


Mhasibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Richard Mayongela akiwasilisha taarifa ya makusanyo ya maduhuli ya mwaka uliopita na mipango ya ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali kwa mwaka mpya wa fedha 2021/2022 kwenye kikao cha Tathmini ya Ukusanyaji wa Maduhuli ya Serikali kwa mwaka fedha uliopita na kuweka mipango ya ukusanyaji wa maduhuli kwa mwaka mpya wa fedha 2021/2022 kilichofanyika jijini Dodoma Julai 23, 2021.


Mhasibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Veronica Kishala akiwasilisha taarifa ya makusanyo ya maduhuli kwa mwaka wa fedha uliopita na mipango ya ukusanyaji wa maduhuli Serikali kwa mwaka mpya wa fedha 2021/2022 katika kikao cha Tathmini ya Ukusanyaji wa Maduhuli ya Serikali na kuweka mipango ya ukusanyaji kwa mwaka mpya wa fedha 2021/ 2022 kilichofanyika jijini Dodoma Julai 23, 2021.


Pichani ni sehemu ya Watendaji wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi walioshiriki Kikao cha Tathmini ya Ukusanyaji wa Maduhuli kwa mwaka wa fedha uliopita na kuweka malengo ya ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali kwa mwaka mpya  wa fedha 2021/2022 kilichofanyika jijini Dodoma Julai 23, 2021.


Wahasibu Wakuu wa Sekta za Mifugo na Uvuvi wakifuatilia matukio yanayoendelea kufanyika katika Kikao cha Tathmini ya Ukusanyaji wa Maduhuli kwa mwaka wa fedha uliopita na kuweka malengo ya ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali kwa mwaka mpya wa fedha 2021/ 2022. Kulia ni Richard Mayongela (Uvuvi) na kushoto ni Veronica Kishala (Mifugo).


Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki (katikati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya Watendaji wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi waliohudhuria Kikao cha Tathmini ya Ukusanyaji wa Maduhuli kwa Mwaka wa fedha uliopita na kuweka malengo ya ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali kwa mwaka mpya wa fedha 2021/2022 uliofanyika jijini Dodoma Julai 23, 2021. Kulia waliokaa ni Kaimu Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Emmanuel Bulayi na Kushoto ni Kaimu Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Amos Zephania.



Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki (katikati) akimueleza jambo Kaimu Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Amos Zephania (kushoto) muda mfupi baada ya kumaliza Kikao cha Tathmini ya Ukusanyaji wa Maduhuli kwa mwaka uliopita na kuweka malengo ya ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali kwa mwaka mpya wa fedha 2021/ 2022. Kulia ni Kaimu Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Emmanuel Bulayi.

TAARIFA KWA UMMA KUHUSU VIFO VYA SAMAKI ENEO LA FUKWE YA BAHARI YA HINDI MKOANI DAR ES SALAAM

 




NDAKI ATOA SOMO KWA VIONGOZI, WATENDAJI WA WIZARA YAKE.

·   Ulega asisitiza sheria ya mabondo na sera ya kopa mbuzi lipa mbuzi 


Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki amewataka viongozi  wa Wizara hiyo kufanya kazi bila woga na kuwatengenezea mazingira rafiki ya utendaji kazi watumishi walio chini yao.


Ndaki ameyasema hayo leo (19.07.2021) kwenye Ofisi za Wizara hiyo zilizopo mji wa Magufuli eneo la Mtumba jijini Dodoma wakati wa kikao baina yake na viongozi wa idara, vitengo na wakuu wa taasisi zote zilizopo chini ya wizara hiyo ambapo amewasisitiza kudumisha ushirikiano baina yao na watumishi waliopo chini yao.


“Niwaombe viongozi wote mliopo hapa, ondoeni hofu wakati wote wa utendaji kazi wenu kwa sababu mimi sipo upande wa mtu yoyote hapa hata nikikupa kazi ifanye bila kuhofia labda naweza kuwa nimekupa kama kipimo flani” Amesema Ndaki.


Aidha Ndaki amewataka viongozi hao kutowalinganisha watumishi waliopo chini yao wakati wa utekelezaji wa majukumu mbalimbali kwa kuwa   uwezo wa mtumishi mmoja hauwezi kufanana na uwezo wa mtumishi mwingine hata kama watakuwa kwenye kada moja.


“Hata wewe leo ungekuwa Waziri ungefanya kwa staili yako na usingefanana na mimi  au Mhe. Ulega hivyo acheni kuwalinganisha watumishi wenu na kumuona mmoja anafaa kuliko wengine na badala yake tafuta mbinu ya kumjengea uwezo ambayo itamfanya afanye kazi vile  inavyotakiwa” Amesisitiza Ndaki.


Akigusia kuhusu matumizi ya lugha sahihi wakati wa kukosoana kwenye mazingira ya kazi, Ndaki amewataka viongozi hao kutumia lugha nzuri wakati wa kuwaelekeza watumishi walio chini yao juu ya namna wanavyopaswa kutekeleza majukumu yao badala ya kutumia lugha za kashfa na dharau.


 “Unakuta kiongozi  anasema kabisa, yule huwa hawezi kufanya hizi kazi tena muda mwingine ukute mtumishi husika ndo ameajiriwa kufanya kazi hiyo, nawahakikishia viongozi mliopo hapa tukifanya hivyo hatutafika na utendaji kazi lazima utakuwa chini” Amesema Ndaki.


Ndaki amewataka viongozi na watendaji hao kuepuka kuwatengenezea hofu watumishi waliopo chini yao ambapo amewashauri kutumia njia ya utoaji huduma bora kwa watumishi hao ili kujipatia heshima wanayostahili.


“ Mimi ninaamini siwezi kuheshimika kwa kuogopwa eti kwa sababu ni Waziri, heshima yangu itatokana na huduma nayotoa kwenu mliopo chini yangu na ninatambua heshima inayotokana na woga inaweza kunikosesha mambo mengi sana kutoka huko chini”


Kwa upande wake Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amewapongeza viongozi hao kwa kazi kubwa wanayoifanya ambapo amewataka kuongeza nguvu zaidi ili kuendelea kutoa huduma stahiki kwa wananchi.


“Kwa mfano hili suala la kopa mbuzi lipa mbuzi, watu wengi wanalisubiri kwa hamu sana hivyo ninatoa rai kwenu mhakikishe mchakato wa kulifanikisha hili unakamilika mapema na wananchi waanze kunufaika na shughuli hiyo” Amesema Ulega.


Akigusia upande wa sekta ya Uvuvi, mbali na kuwapongeza viongozi hao kwa kazi nzuri ya kusimamia uendeshaji wa viwanda vya kuchakata samaki, Ulega amewataka watendaji wa sekta hiyo kusimamia sheria kuhusu suala la uchakataji wa mabondo ambayo yameonekana kuchakatwa na wananchi katika maeneo mbalimbali badala ya viwandani kama sheria inavyoelekeza.


“Lakini pia sasa hivi ni lazima tudhibiti huu mfumo wa kuuza samaki mzima kabla ya kumchakata kwa sababu kwa mtazamo wangu naona unatukosesha mapato mengi sana ambayo yangepatikana kutokana na mauzo ya mazao mbalimbali yanayotokana na samaki huyo” Amesisitiza Ulega.


Wakitoa neno la shukrani  kutokana na kikao hicho, Makatibu wakuu wa Wizara hiyo Prof. Elisante Ole Gabriel (Mifugo) na Dkt. Rashid Tamatamah (Uvuvi) wameahidi kutekeleza maelekezo yote yaliyotolewa na viongozi hao kwenye kikao hicho huku pia wakiwashukuru mawaziri hao kutokana na ushirikiano wanaowaonesha wakati wa utekelezaji wa majukumu yao.


Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki (kushoto) akisisitiza kuhusu ushirikiano kati ya viongozi na watumishi waliopo chini yao wakati wa kikao baina yake na Viongozi na watendaji wa idara, vitengo na taasisi zilizopo chini ya wizara yake kilichofanyika leo (19.07.2021) makao makuu ya Wizara hiyo yaliyopo mji wa Magufuli eneo la Mtumba jijini Dodoma, Kulia ni Naibu Waziri wa Wizara hiyo Abdallah Ulega.


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega (kulia) akimuonesha Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki mfano wa  namna Serikali inavyopata hasara kutokana na mauzo ya samaki mzima kabla hajachakatwa wakati wa kikao baina yao na Viongozi na watendaji wa idara, vitengo na taasisi zilizopo chini ya wizara ya Mifugo na Uvuvi kilichofanyika leo (19.07.2021) makao makuu ya Wizara hiyo yaliyopo mji wa Magufuli eneo la Mtumba jijini Dodoma.

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt.Rashid Tamatamah akifafanua namna sekta yake inavyosimamia utekelezaji wa majukumu yake wa kikao baina ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki, Naibu Waziri wa Wizara hiyo Abdallah Ulega na Viongozi, watendaji wa idara, vitengo na taasisi zilizopo chini ya wizara hiyo kilichofanyika leo (19.07.2021) makao makuu ya Wizara hiyo yaliyopo mji wa Magufuli eneo la Mtumba jijini Dodoma.


Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof.Elisante Ole Gabriel akieleza namna alivyoguswa na ujumbe uliotolewa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki wakati wa kikao baina ya Waziri huyo, Naibu Waziri wa Wizara hiyo Abdallah Ulega na Viongozi, watendaji wa idara, vitengo na taasisi zilizopo chini ya wizara hiyo kilichofanyika leo (19.07.2021) makao makuu ya Wizara hiyo yaliyopo mji wa Magufuli eneo la Mtumba jijini Dodoma.


Sehemu ya Viongozi watendaji wa idara, vitengo na taasisi zilizopo chini ya wizara ya Mifugo na Uvuvi wakimsikiliza Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki (hayupo pichani) wakati wa kikao baina yake na Viongozi, watendaji wa idara, vitengo na taasisi zilizopo chini ya Wizara hiyo kilichofanyika leo (19.07.2021) makao makuu ya Wizara hiyo yaliyopo mji wa Magufuli eneo la Mtumba jijini Dodoma.

MKAKATI WA KOPA MBUZI LIPA MBUZI KUANZA, CHANJO ZA MIFUGO ZATAKIWA VIJIJINI

Na. Edward Kondela


Serikali imesema Ranchi ya mifugo ya Mkata iliyopo Wilaya ya Kilosa Mkoani Morogoro itakuwa sehemu ya kuzalisha mbuzi kwa wingi kwa ajili ya mkakati wa kopa mbuzi lipa mbuzi ambao unatarajia kuanza hivi karibuni lengo likiwa ni kuwa na mbuzi wa kutosha kwa ajili ya soko la nje ya nchi.


Akizungumza na uongozi wa ranchi na Wilaya ya Kilosa, wakati wa ziara ya kikazi ya siku moja katika Ranchi ya Mkata, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdalllah Ulega amesema ni muhimu kuangalia namna bora ya kufanya ufugaji wa kibiashara katika ranchi hiyo.


Amesema serikali imechagua Ranchi ya Mkata kuwa kituo cha kuzalisha mbuzi kwa wingi ambacho watakuwa wanasambaza katika maeneo mbalimbali nchini.


"Tutakayempa tutataka tujue yupo wapi na ana mbuzi wangapi ili tuwatambue na tuwaingize katika mfumo wetu wa takwimu za kibiashara ili iwapo tunapata mteja wa kilo 50 kwa mwezi kweli tuwe na uhakika wa kupata kilo hizo 50 kwa mwezi.” Amesema Mhe. Ulega


Kutokana na mkakati huo wa kopa mbuzi lipa mbuzi mahitaji ya mbuzi yatakuja kuwa makubwa nchini hivyo ameitaka ranchi hiyo kuzalisha mbuzi kwa wingi ili kuweza kutosheleza soko la ndani na nje ya nchi.


Aidha Mhe. Ulega amesema wafugaji wa mbuzi wafuge kibiashara ili kuweza kutimiza vigezo na masharti ya wateja wa kimataifa kama nchini hizo na kutolea mfano wa nchi za uarabuni ambazo wanataka mbuzi wenye uzito wa kilo kati ya 8 hadi 10 ambao hawajakomaa sana.


Kwa upande wake Meneja wa Ranchi ya Mkata Bw. Oscar Magete amesema ranchi ilianzishwa  na serikali kwa madhumuni ya kuendeleza na kueneza ufugaji bora wa mbuzi, kondoo na ng'ombe ambapo ranchi hiyo kwa sasa ina mbuzi 609 kondoo 116 na ng'ombe 47.


Katika hatua nyingine Naibu Waziri Ulega ametembelea kiwanda cha kuzalisha chanjo cha Nobel Vaccine Bioscience (NOVABI) kilichopo Mkoani Morogoro kinachozalisha chanjo aina ya Tatu Moja kwa ajili ya ya mdondo, ndui ya kuku na mafua ambayo yanaathiri mfumo wa upumuaji na yamekuwa chanzo kikuu cha vifo vya kuku na kuwatia hasara wafugaji.


Akiwa kiwandani hapo Naibu Waziri Ulega ameelekeza chanjo hiyo ya kipekee isambazwe maeneo mbalimbali nchini hususan vijijini ambapo kuna wafugaji wengi wa kuku wa kienyeji ili waweze kuipa mifugo yao chanjo kuondokana na hasara ambayo wamekuwa wakipata ya kuku kufa kutokana na magonjwa hayo.


Ameongeza kuwa ni vyema uongozi wa wizara kuhakikisha chanjo mbalimbali zinazozalishwa ndani na nje ya nchi zinawafikia walengwa hususan waliopo vijijini ili waweze kufuga kibiashara na waweze kunufaika kupitia mifugo yao.

Naibu waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega akionesha namna chanjo ya Tatu Moja inayozalishwa na kampuni ya Nobel Vaccine Bioscience (NOVABI) inavyotumika kwa ajili ya kudhibiti magonjwa ya mdondo, ndui na mafua ya kuku kupitia njia ya kwenye macho ya mifugo hiyo. (14.07.2021)


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (Mb), (kushoto) akipewa maelezo na mmoja wa wanasanyansi wanaotengeneza chanjo ya Tatu Moja Prof. Phillemon Wambura namna chanjo hiyo inayodhibiti magonjwa ya mdondo, ndui na mafua ya kuku isivyoweza kughushiwa kwa namna yoyote ile kwa kuwa imewekewa rangi maalum ya kubaini endapo ikiwa imeghushiwa. (14.07.2021)


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega akiwa amebeba moja ya aina ya mbuzi wanaozalishwa kwenye Ranchi ya Mkata iliyopo Wilaya ya Kilosa Mkoani Morogororo mara baada ya kufanya ziara ya kikazi ya siku moja katika ranchi hiyo na kuagiza ranchi hiyo kuendeleza uzalishaji wa mbuzi kwa ajili ya kufuga kibiashara. (14.07.2021)


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (Mb) akitoa maelekezo kwa uongozi wa Ranchi ya Mkata iliyopo Wilaya ya Kilosa Mkoani Morogoro, kuhakikisha wanazalisha mbuzi wengi zaidi kwa ajili ya mkakati wa kopa mbuzi lipa mbuzi ili wananchi wengi zaidi waweze kuingia katika ufugaji wa kisasa na kibiashara. (14.07.2021)


TANZANIA YAKATAA NYONGEZA YA RUZUKU KWENYE UVUVI

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki leo (15.07.2021) amekataa nyongeza ya ruzuku kwenye shughuli za uvuvi ambapo amesema kuwa hatua hiyo itawawekea mazingira magumu wavuvi waliopo hapa nchini kutokana na kutokuwa na miundombinu ya kisasa ya kufanya shughuli hizo hasa katika eneo la bahari kuu ikilinganishwa na makampuni yanayotoka nje ya nchi.


Ndaki ameyasema hayo alipokuwa akiwasilisha taarifa ya wizara yake  kwenye mkutano wa kamati ya majadiliano ya biashara (TNC) ngazi ya mawaziri ambao ulikuwa ukijadili mkataba wa  kuondoa  ruzuku  katika shughuli za uvuvi ambapo amesema kuwa kwa hivi sasa Tanzania bado haijapiga hatua kubwa kwenye uvuvi wa bahari kuu hivyo ongezeko hilo la ruzuku litatoa fursa nzuri zaidi kwa makampuni ya uvuvi ya yaliyopo kwenye nchi zilizoendelea.


“Kwanza sisi bado hatujaanza kutoa ruzuku kwa wavuvi wetu lakini pia makampuni haya kutoka nje yakipata ruzuku hiyo yatakwenda kuvua mahali popote kwenye samaki na kwa kuwa wao wana nyenzo za kisasa watafanya hadi uvuvi unaopitiliza “overfishing” jambo ambalo litawakosesha samaki wavuvi wetu” Amesema Ndaki.


Ndaki ameongeza kuwa kwa hivi sasa nchi inahitaji nafasi ya kutosha ya kuwawezesha wavuvi waliopo hapa nchini mazingira mazuri yatakayowasaidia kufanya shughuli zao kwa ufanisi hasa  kwenye ukanda wa bahari kuu.


“Tunahitaji kuweka mazingira madhubuti na kujidhatiti kisera na sasa tupo kwenye mchakato wa ununuzi wa meli za uvuvi ambazo kwa kiasi kikubwa zitaweza kutusaidia kutekeleza shughuli za uvuvi kwenye ukanda wa bahari kuu” Amesisitiza Ndaki.


Jumla ya Mawaziri  na watendaji wa nchi wanachama 164 wa kamati ya majadiliano ya biashara (TNC) wameshiriki mkutano huo ambao ulifanyika kwa njia ya mtandao na kuratibiwa na Shirika la biashara duniani (WTO) kutoka nchini Uswisi.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki akifuatilia mkutano wa kamati ya majadiliano ya biashara (TNC) uliofanyika kwa njia ya mtandao leo (15.07.2021)  na kujumuisha viongozi wa sekta za Mifugo na Uvuvi, Viwanda na biashara kutoka nchi 164, balozi wa Tanzania nchini Uswisi  na watendaji wa sekta hizo kutoka kwenye mataifa shiriki ya mkutano huo, lengo la mkutano huo lilikuwa ni kujadili Mkataba wa kuondoa ruzuku kwenye shughuli za uvuvi.

MAZUNGUMZO YA UBORESHAJI WA TAFITI KATIKA USIMAMIZI WA RASILIMALI ZA UVUVI

Kaimu Mkurugenzi Idara ya Uvuvi Bw. Stephen Lukanga  amesisitiza uvuvi endelevu ili kuleta faida za kiuchumi kwa Taifa na kwa Wananchi walio Katika mnyororo wa thamani.


Lukanga amesema hayo leo 15.07.2021 kwa niaba ya Mkurugenzi wa Idara ya Uvuvi wakati wa ufunguzi wa warsha ya Mazungumzo juu ya matumizi ya Utafiti Katika kufanya maamuzi ya Usimamizi wa Rasilimali za Uvuvi (science- management Dilogue) uliofanyika Katika Ukumbi wa Mkapa Jijini Dodoma.


Amesema Serikali kupitia Idara za Maendeleo ya Uvuvi imekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kuwa Uvuvi Katika Bahari ya Hindi unakuwa endelevu na wa manufaa zaidi .


Bw. Lukanga alieleza kuwa , Serikali ilisaini Barua ya makubalianao na Shirika la Kilimo na Chakula la Umoja wa Mataifa chini ya mpango wa EAF - Nansen kutekeleza Mradi mdogo wa Utekelezaji wa mpango wa Usimamizi wa Samaki wanaopatikana Katika tabaka la juu la maji Katika Ukanda wa Bahari ya hindi.


“Lengo la Mradi ni kusaidia Utekelezaji wa mpango wa Usimamizi wa samaki wanaopatikana katika Tabaka la juu ya maji ulioandaliwa mwaka 2010 mpaka 2013 na Serikali kwa kushirikiana na FAO ili kuimarisha uendelevu wa rasilimali ya samaki wadogo na Dagaa, amesema Lukanga.


Aliendelea kuwa mradi una lengo wa kuimarisha uwezo wa Wizara na wadau wake Katika kutekeleza mpango wa kusimamia samaki kwa kuzingatia mzunguko wa Usimamizi wa Uvuvi Fisheries Management Cycle (CFM) kwa kuzingatia mfumo wa Ikolojia na Mazingira ( Ecosystem Approach to Fisheries Management)


“Niwaombe tushiriki kikamilifu ili kuona namna ambayo tunaweza tukafanya Uvuvi huu kuwa endelevu na kuleta faida za kiuchumi kwa Taifa lakini pia kwa Wananchi walio katika mnyororo wa thamani , amesema Lukanga.


Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Nchini (TAFIRI)  Dkt. Ismael Kimirei amesema, kazi kubwa ya Taasisi hiyo ni kukuza, kuratibu na kufanya Utafiti ambapo anaamini majadiliano hayo yamelenga , kujenga na kuboresha Tafiti Katika kusimamia Rasilimali za Uvuvi.


Mkurugenzi Msaidizi Kitengo cha Udhibiti Ubora mazao ya Uvuvi na masoko Bw. Stephen Lukanga  akifungua warsha kwa niaba ya Mkurugenzi wa Idara ya Uvuvi inayolenga Mazungumzo juu ya matumizi ya Utafiti Katika kufanya maamuzi ya Usimamizi wa Rasilimali za Uvuvu (Science - management Dilogue) leo tarehe 15.07.2021 katika ukumbi wa Mkapa, Jijini Dodoma , kushoto ni Mkurugenzi Mkuu TAFIRI Dkt. Ismael Kimirei na kulia ni Mkurugenzi Msaidizi Kitengo cha Uendelezaji wa Rasilimali za Uvuvi Bi. Merisia Mparazo.

Baadhi ya Watendaji Wakuu wa Taasisi, Wakala, Wakurugenzi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi , Watafiti kutoka TAFIRI na Wawakilishi kutoka WWF, TuNA Alliance wakisikiliza kwa makini hotuba kutoka kwa Kaimu Mkurugenzi Idara ya Uvuvi Bw. Stephen Lukanga kwa niaba ya Mkurugenzi wa Idara ya Uvuvi leo 15.07.2021 katika Ukumbi wa Mkapa, Dodoma.


Afisa Uvuvi Mwandamizi Kitengo cha Uendelezaji wa Rasilimali za Uvuvi Bi. Upendo Hamidu akizungumzia juu ya uboreshaji wa tafiti Katika kufanya maamuzi ya Usimamizi wa Rasilimali za Uvuvi leo 15.07.2021 Ukumbi wa Mkapa, Dodoma.


Picha ya pamoja ni Kaimu Mkurugenzi Idara ya Uvuvi Bw. Stephen Lukanga kwa niaba ya Mkurugenzi wa Idara ya Uvuvi  (Katikati mwenye shirt nyekundu na koti jeusi ) akiwa na Baadhi ya Watendaji Wakuu wa Taasisi, Wakala, Wakurugenzi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi , Watafiti kutoka TAFIRI, Wawakilishi kutoka WWF na TuNA Alliance leo 15.07.2021 katika ufunguzi wa warsha ya Mazungumzo juu ya matumizi ya utafiti katika kufanya maamuzi ya Usimamizi na Rasilimali za Uvuvi, Jiji Dodoma.

ULEGA ATAKA SEKTA YA MIFUGO KUJIENDESHA KIBIASHARA

Na. Edward Kondela


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega ameagiza shamba la malisho ya mifugo lililopo Vikuge Wilaya ya Kibaha Mkoani Pwani, kujiendesha kibiashara na kusambaza mbegu za malisho kutoka nchini China ijulikanayo kama JUNCAO maeneo mbalimbali nchini kwa kuwa ina sifa ya kustahimili sehemu yenye ukame ili wafugaji wapande malisho hayo.


Wakati akihitimisha ziara ya kikazi ya siku mbili mkoani humo (13.07.2021) Naibu Waziri Ulega, amesema hayo wakati alipotembelea na kukagua maendeleo ya shamba hilo na kumuagiza Katibu Mkuu anayeshugulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel kuhakikisha aina mpya ya malisho hayo inasambazwa na kusimamia vyema ili mradi huo uweze kuwa na tija kwa taifa hususan kwa wafugaji vijijini.


Mhe. Ulega amesema mbegu za malisho ya JUNCAO zisambazwe kuanzia ngazi ya mikoa wilaya hadi vijiji lengo likiwa kudhibiti mifugo na wafugaji kuhamahama kutafuta malisho.


Amefafanua kuwa hataki kuona mambo yanayoanzishwa kwa ajili ya kunufaisha wananchi yanaishia njiani kwani ni vizuri kukawa na mwendelezo wa teknolojia hiyo ya kilimo hicho kipya cha malisho ya mifugo hata kusambazwa kwa wafugaji hadi vijijini.


Amesema lengo la serikali ni kuhakikisha mbegu za malisho hayo zinaenea hadi vijijini kwa wafugaji akitaja hususan mikoa yenye ukame kama Dodoma, Singida, Manyara, Shinyanga na iwapo zitasambazwa vizuri  itapunguza tatizo la wafugaji na mifugo yao kuhama hama kutafuta malisho ya mifugo yao.


"Kinachosababisha wafugaji kuzunguka na kuhama hama ni kutafuta chakula cha malisho na maji kwa ajili ya mifugo yao hivyo kama wafugaji watafikishiwa mahali walipo itawasaidia wafugaji kuwa na uhakika wa malisho." amesema Mhe. Ulega.


“Mbegu hizi nataka zifike kwa haraka na kwa gharama nafuu ambayo kila mfugaji ataweza kununua aweze kuhudumia mifugo yake.” amesema Mhe. Ulega


Akizungumzia changamoto wanazokutana nazo katika uendeshaji wa shamba la Vikuge Meneja wa shamba hilo Bw. Reuben Ngailo  amesema kukosekana kwa vifaa na nguvu kazi katika mipango yao ya kusafisha shamba na kupanua uzalishaji.


Amesema pia eneo hilo la shamba lina visiki vingi ili kuving'oa inagharimu kiasi kikubwa cha fedha jambo ambalo husababisha kuendesha uzalishaji wa malisho katika eneo dogo.


Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Chalinze Mhe. Ridhiwani Kikwete akiwa ameambatana na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega ameomba malisho yanayozalishwa shambani hapo kuwanufaisha wakazi wa Mkoa wa Pwani.


Mhe. Kikwete amesema shamba hilo lipo Mkoa wa Pwani na mkoa huo una migogoro mingi ya wakulima na wafugaji kwa ajili ya kutafuta malisho na maji, hivyo ombi lake ni mbegu hizo zisambazwe haraka kwa wafugaji wa mkoa huo.


Katika hatua nyingine Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega amekabidhi lambo la kunyweshea mifugo maji la Chamakweza lililopo Wilaya ya Chalinze Mkoani Pwani na kuiagiza Halmashauri ya Manispaa ya Chalinze kuunda kamati kwa ajili ya kusimamia lambo hilo lililokarabatiwa na serikali kwa gharama ya zaidi ya Shilingi Milioni 600 kwa ajili ya matumizi ya mifugo na binadamu.


Mhe. Ulega amesema ni wakati sasa wafugaji kutumia vyema lambo hilo kwa ajili ya kuboresha mifugo yao ambayo imekuwa ikikosa maji ya kunywa na kuwataka kubadilika na kuanza kufuga kibiashara kwa kuwa na mifugo ambayo wanakuwa wanavuna kila baada ya muda kwa kuuza kwenye viwanda vya kuchakata nyama badala ya kuwa na mazoea ya kuwa na mifugo mingi ambayo haina tija kwao.


Amefafanua kuwa lengo la serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ni kuona mfugaji ananufaika kupitia mifugo yake kwa kufanya biashara na hatimaye kuongeza pato la taifa na mfugaji mwenyewe.


Naibu Waziri Ulega tayari amemaliza ziara ya kikazi ya siku mbili Mkoani Pwani.


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (Mb) aliyechuchumaa akimpa maelezo Mbunge wa Jimbo la Chalinze Mhe. Ridhiwani Kikwete juu ya sifa za malisho ya mifugo yajulikanayo kama JUNCAO kutokea nchini China ambayo yamepandwa katika shamba la malisho ya mifugo lililopo Vikuge katika Wilaya ya Kibaha Mkoani Pwani, ambapo Mhe. Ulega ametaka mbegu za malisho hayo zisambazwa kote nchini hususan vijijini. (13.07.2021)


Meneja wa shamba la malisho ya mifugo lililopo Vikuge katika Wilaya ya Kibaha Mkoani Pwani, Bw. Reuben Ngailo (mwenye fulana nyekundu), akitoa maelezo kwa Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega, Mbunge wa Jimbo la Chalinze Mhe. Ridhiwani Kikwete na Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo kutoka wizarani Prof. Hezron Nonga juu ya aina mbalimbali za mbegu za malisho wakati wa ziara ya kikazi ya siku mbili ya Naibu Waziri Ulega Mkoani Pwani. (13.07.2021)


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (mwenye koti jeusi), akiangalia birika la kunyweshea mifugo maji wakati alipotembelea lambo kwa ajili ya matumizi ya mifugo na binadamu la Chamakweza lililopo Wilaya ya Chalinze Mkoani Pwani na kukabidhi rasmi lambo hilo kwa Halmashauri ya Manispaa ya Chalinze kwa ajili ya matumizi ya wafugaji. (13.07.2021)


Muonekano wa sehemu ya lambo kwa ajili ya matumizi ya mifugo na binadamu ambalo Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (Mb) amelikabidhi kwa Halmashauri ya Manispaa ya Chalinze baada ya kukarabatiwa na serikali kwa zaidi ya Shilingi Milioni 600 na kuagiza kuundwa kwa kamati ya kusimamia lambo hilo. (13.07.2021)



NDAKI AAGIZA ULINZI KUWEKWA KWENYE SHAMBA LA UZALISHAJI MIFUGO - MABUKI

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki ameagiza eneo la shamba la uzalishaji mifugo lililopo wilayani Misungwi mkoani Mwanza kulindwa na Suma JKT, Polisi pamoja na kujengewa fensi (uzio) ili kuimarisha ulinzi na usalama wa eneo hilo.

 

Hii ni baada ya Waziri huyo kufanya ziara jana ya kutembelea shamba la Mabuki pamoja na taasisi zilizomo ndani yake ambapo alielezwa kuwepo kwa uchungaji haramu na uchomaji moto pamoja na tishio la usalama kwa wanafunzi na watumishi katika shamaba hilo.

 

Ndaki amesema,eneo hilo ni kubwa na lipo wazi kwa hali hiyo  siyo salama kila mtu anaweza kuingia na kufanya jambo lolote hivyo waangalie uwezekano wa kuweka fensi ili mtu atakaye bomoa na kuingia itakuwa rahisi kumdhibiti.

 

Amesema,eneo hilo linapaswa kulindwa na Suma JKT,hivyo alimuagiza Mkurugenzi wa Utafiti ,Mafunzo na Ugani kutoka Wizara ya  Mifugo na Uvuvi Dkt.Angello Mwilawa pamoja na uongozi wa kituo hicho kukaa pamoja na kuangalia ni walinzi wa ngapi wanahitajika kwa ajili ya ulinzi wa shamba hilo.

 

Pia amesema katika suala la kuwalipa Suma JKT ni lazima taasisi hizo na wizara kukaa Pamoja kuangalia namna ambayo watakuwa wanawalipa ili kusiwe na sababu yoyote itayositisha ulinzi huo pindi utakapoanza.

 

Aidha, katika kuimarisha zaidi ulinzi wa eneo hilo amemuomba Mkuu wa Wilaya ya Misungwi awapatie Askari Polisi ambao watakuwa wanafanya kazi kwa kushirikiana na SUMA JKT lengo likiwa ni kuhakikisha eneo hilo linakuwa salama.

 

"Hatuwezi kuangalia wanafunzi na watumishi wapo hatarini,halfu sisi tunanyoosha mikono na kusema Mungu tusaidie na vitendo vya waangalizi wa ng'ombe,wanafunzi na watumishi kupigwa siyo sawa hivyo,tutafute pesa popote fensi ijengwe kama mwanzo,eneo hili lilindwe na Suma JKT na Polisi ili wavamizi wajue kuwa linalindwa," amesema Ndaki.

 

Awali Kaimu Meneja wa Wakala wa Mafunzo ya Mifugo (LITA) kampasi ya Mabuki Joel Ngogo,akisoma taarifa kwa Waziri huyo, amesema Juni 9,2020 wanafunzi wao wakiwa shambani  kukata fito za kujengea uzio wa ng'ombe walivamiwa,walipigwa na jaribio la kutaka kubakwa  mwanafunzi mmoja  wa kike ambaye aliokolewa na watu waliopita eneo hilo.

 

Ngogo amesema, Aprili 23, mwaka huu matukio ya wanafunzi kuvamiwa na kupigwa kwa kombeo wakiwa eneo la kantini (mgahawa) wakipata chakula yalirudiwa na wavamizi wanaodhaniwa kutumwa na wafugaji ambao mifugo yao ilikamatwa na uongozi wa shamba hilo.

 

Amesema katika kutatua changamoto hiyo alimuomba Waziri kusaidia kuoata ulinzi thabiti kwa kutumia makampuni ya ulinzi kwa kushirikiana na jeshi la Polisi.

 

Kwa upande wake Meneja wa shamba la uzalishaji mifugo Mabuki Lini Andey Mwalla,amesema wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya uchungaji haramu wa mifugo ya wananchi kutoka sehemu mbalimbali.

 

Hali hiyo imekuwa ikivuruga malengo yaliyokusudiwa na serikali na kusababisha athari ikiwemo kueneza magonjwa ya virusi na yaenezwayo na kupe hivyo kusababisha vifo vingi vya mifugo vitokanavyo na magonjwa kama ndigana kali na mengineyo.

 

Pia amesema,suala la uchomaji moto hususani kipindi cha kiangazi kinachofanywa na watu ambao bado hawajawabaini kutokana na mbinu wanazotumia wahusika limekuwa likisababisha uharibifu wa mazingira na hivyo mifugo kukosa malisho.



Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki akiwa amemshika nyati maji wakati alipotembelea  shamba la L.M.U. Mabuki lililopo wilayani Misungwi mkoani Mwanza kwa lengo la kuona maendeleo yake. (14.07.2021)


Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (Mb) akiwa kwenye picha ya pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Misungwi, Mhe. Veronica Kessy (wa nne kutoka kushoto), Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti, Mafunzo na Huduma za Ugani, Dkt. Angello Mwilawa (wa tatu kutoka kulia) na watumishi wa Shamba la L.M.U, LITA na TALIRI wote wa Mabuki wilayani Misungwi mkoa wa Mwanza wakati alipowatembelea kukagua maendeleo ya taasisi hizo ambapo amewataka kuwa na mipango ya kuweza kujiendesha wenyewe kwa faida badala ya kutegemea ruzuku kutoka serikali kuu, pia ameagiza kuwepo na ulinzi wa SUMA JKT. (14.07.2021)


Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki akizungumza na wanafunzi wa LITA Mabuki wakati alipowatembelea kwa lengo la kuona maendeleo yao ya kielimu ambapo amewataka wasome kwa bidii ili waje wajiajiri na sio kutegemea ajira kutoka serikalini. (14.07.2021)


 


SEKTA YA UVUVI KUFANYA MAPITIO YA BAADHI YA SHERIA NA KANUNI – MHE. NDAKI

Sekta ya Uvuvi imepanga kufanya mapitio ya baadhi ya sheria na kanuni za uvuvi ili ziweze kuendana na mazingira ya sasa.

 

Haya yamesemwa (13.07.2021) na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki wakati alipozungumza na wadau wa sekta ya uvuvi wa mkoa wa Kagera kwenye kikao kilichofanyika kwenye ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa.

 

Waziri Ndaki alisema kuwa kumekuwepo na malalamiko kutoka kwa wadau kuwa baadhi ya sheria na kanuni za uvuvi zimekuwa kikwazo katika utekelezaji wa shughuli zao. Hivyo wizara imeona ni muda muafaka kufanya mapitio ya baadhi ya sheria na kanuni hizo ili ziendane na mazingira ya sasa na kutokuwa kikwazo katika ufanyaji wa shughuli za uvuvi.

 

Lakini pamoja na mapitio hayo ya sheria na kanuni, wadau wa sekta ya uvuvi wametakiwa kuhakikisha wanafuata taratibu zote zilizopo katika utekelezaji wa shughuli zao za uvuvi na sio kusubiri mpaka wafuatiliwe. Aidha Waziri Ndaki aliwasihi wadau hao kuhakikisha wanashiriki kikamilifu kwenye udhibiti wa uvuvi haramu kwani bila kufanya hivyo samaki wataisha majini na wao itawalazimu kutafuta shughuli nyingine za kufanya.

 

Vilevile kwa upande wa wataalam wametakiwa kuendelea kuwaelimisha wavuvi kutumia mbinu bora za uvuvi ili waondokane na uvuvi haramu. Aidha, amewaonya wataalam kutojihusisha na vitendo vya uvuvi haramu kwani endapo watabainika watachukuliwa hatua. Pia amewataka wataalam kuendelea kuwaelimisha wavuvi kuhusu suala la ufugaji wa samaki kwenye vizimba.

 

Waziri Ndaki aliwaeleza wadau hao kuwa kazi wanayoifanya ya uvuvi ni halali na inatambulika kiserikali na serikali inategemea kupata mapato kutokana na shughuli za uvuvi hivyo wanatakiwa kuwa huru wakati wanapofanya shughuli zao na endapo wanakutana na changamoto ni vema wawe wanazifikisha kwenye mamlaka husika.

 

Pia amezishauri mamlaka za serikali za mitaa kutathmini upya tozo walizoziweka kwenye mazao ya uvuvi, biashara ya uvuvi au kwenye shughuli ya uvuvi kwani ni nyingi.

 

Wadau hao wa sekta ya uvuvi wa mkoa wa Kagera wamemshukuru waziri kwa kuitisha kikao hicho ambacho wameweza kutoa changamoto na maoni yao juu ya maendeleo ya sekta ya uvuvi kwani ni kitu ambacho hawajawai kutegemea kuja kukaa na waziri na kuwasikiliza.


Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (Mb) akizungumza na wadau wa sekta ya uvuvi wa mkoa wa Kagera (hawapo pichani) ambapo amewaeleza kuwa wizara itafanya mapitio ya sheria na kanuni za uvuvi ili ziweze kuendana na mazingira ya sasa. Kikao hicho kimefanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera. (13.07.2021)


Mmoja ya wadau wa sekta ya uvuvi mkoani Kagera, Bw. Pancras Mtungireli akitoa maoni yao kuhusu maendeleo ya sekta ya uvuvi kwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi (hayupo pichani) kwenye kikao cha wadau hao kilichofanyika kwenye ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera. (13.07.2021)


ZIARA YA NDAKI YAWA DAWA YA MIGOGORO MKOANI KAGERA

Ziara ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Mashauri Ndaki mkoani Kagera imekuwa dawa ya utatuzi wa migogoro ya ardhi kati ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi.

 

Waziri Ndaki amefanya ziara ya siku nne mkoani Kagera kwa lengo la kutatua migogoro ya ardhi iliyokuwepo katika maeneo yanayomilikiwa na Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) katika Ranchi za Mabale wilayani Misenyi, Kagoma na Mwesa wilayani Muleba mkoani Kagera.

 

Akizungumza na uongozi wa mkoa wa Kagera ambapo pia alikuwepo Katibu Mkuu anayesimamia sekta ya mifugo baada ya kumaliza ziara yake, Waziri Ndaki alisema kuwa ziara hiyo imekuwa muhimu na yenye mafanikio makubwa kwake na kwa sekta ya mifugo kwani uwepo wa migogoro husababisha kupungua kwa kasi ya ukuaji wa sekta ya mifugo.

 

Katika ranchi hizo kulikuwa na wananchi ambao walikuwa wanakaa kwa muda mrefu na kufanya shughuli zao za maendeleo katika maeneo hayo. Hivyo kutokana na hilo kulikuwepo na migogoro kati ya wananchi hao na wawekezaji waliopewa vitalu kwa ajili kufugia mifugo.

 

Baada ya malalamiko hayo ya muda mrefu kati ya wananchi na wawekezaji, Waziri Ndaki aliwaeleza wananchi hao kuwa Mhe. Rais Samia Hassan ameridhia wabaki katika maeneo hayo na kuendelea kufanya shughuli zao za maendeleo. Pia aliwaeleza wananchi na wawekezaji kuwa serikali itayapima upya maeneo hayo na kuweka alama za mipaka ili migogoro hii isijirudie.

 

Vilevile wananchi katika maeneo hayo walielezwa kuwa upimaji na mipaka ikishawekwa lazima kila mmoja aifuate na kuiheshimu. Pia kwa wale ambao wamejitenga mmoja mmoja wanatakiwa kuanza kuhama na kutafuta maeneo kwenye vijiji.

 

Waziri Ndaki pia aliwaeleza wawekezaji kuwa upimaji huu utakaofanyika katika maeneo ya ranchi hauta waathiri katika shughuli zao za ufugaji. Serikali inawahitaji wawekezaji katika kuhakikisha sekta ya Mifugo inakua. Lakini pia amewasisitiza wawekezaji kuwa vitalu watakavyopewa ni lazima wahakikishe wanavitumia kwa malengo yaliyokusudiwa kwa kuhakikisha wanafuga mifugo bora.

 

Katika ranchi ya Mwisa II ambayo nayo ilikuwa na mgogoro mkubwa Waziri Ndaki alisema tayari wizara imeshaweka makubaliano na uongozi wa Mkoa wa Kagera pamoja na Wilaya ya Muleba ili kuhakikisha utatuzi wa mgogoro uliopo pale unatatuliwa.

 

Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Meja Jenarali Charles Mbuge amesema kuwa ulinzi na usalama ni kipaumbele namba moja kwenye mkoa hivyo uwepo wa migogoro husababisha uvunjifu wa amani. Hivyo utatuzi wa migogoro uliofanyika utasaidia sana maeneo hayo kuwa na amani na kuwafanya wananchi na wawekezaji kuendeleza shughuli zao za maendeleo. Kwa upande wake ameahidi kuwa atasimamia utekelezaji wa makubaliano yote yaliyofikiwa katika utatuzi wa migogoro hiyo.

 

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Mbunge wa Muleba Kaskazini, Mhe. Charles Mwijage na Mbunge wa Muleba Kusini, Mhe. Oscar Kikoyo walisema kuwa migogoro hiyo imechukua muda mrefu kutatuliwa lakini wamemshukuru Mhe. Rais Samia Hassan kwa kuridhia wananchi hao kubaki katika maeneo hayo yanayomilikiwa NARCO. Vilevile wamemshukuru Waziri Ndaki na viongozi na wataalam katika Wizara Mifugo kwa jitihada waliochukua ili kuhakikisha wanamaliza migogoro hiyo.

 

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayesimamia sekta ya mifugo, Prof. Elisante Ole Gabriel alisema kuwa lengo la wizara ni kuhakikisha sekta ya mifugo inakua na inaongeza kipato kwa wafugaji na taifa kwa ujumla. Pia alisema kwa upande wa wizara atahakikisha makubaliano yote yaliyofikiwa yanakwenda kutekelezwa.

 

Utatuzi wa wa migogoro hiyo katika Mkoa wa Kagera umeleta faraja kubwa kwa wananchi ambao walikuwa wanakaa katika maeneo ya ranchi za Taifa. Lakini pia kwa wawekezaji waliopatiwa vitalu kwani baada ya utatuzi huo sasa pande zote mbili watafanya shughuli zao za kiuchumi kwa amani.


Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (Mb) akiwa kwenye picha ya pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Mhe. Meja Jenarali Charles Mbuge (wa tatu kutoka kushoto), Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel (wa pili kutoka kulia), Mkuu wa Wilaya ya Muleba, Mhe. Toba Nguvila (wa pili kutoka kushoto), Mbunge wa Jimbo la Muleba Kaskazini, Mhe. Charles Mwijage (kushoto) na Mbunge wa Jimbo la Muleba Kusini, Mhe. Dkt. Oscar Kikoyo na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Muleba, Bw. Emmanuel Sherembi wakiwa wameshikilia nakala za maazimio yaliyoafikiwa kuhusu utatuzi wa mgogoro wa ardhi kwenye Mradi wa Mwisa II uliopo wilayani Muleba. (13.07.2021)

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (Mb) akizungumza na viongozi na wataalam kutoka wizarani upande wa sekta ya Mifugo, sekretarieti ya mkoa wa Kagera, Wilaya ya Muleba na Wabunge wa Muleba baada ya kumaliza ziara yake ya siku nne mkoani Kagera kwa lengo la kutatua migogoro iliyokuwepo kwenye maeneo yanayomilikiwa na Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO). Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Meja Jenarali Charles Mbuge na kulia ni Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Elisante Ole Gabriel. (13.07.2021)


ULEGA ATAKA KUMALIZIKA KWA MIGOGORO NA CHANJO KUFIKISHWA VIJIJINI

Na. Edward Kondela


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (Mb) ameusisitiza uongozi wa Mkoa wa Pwani kutumia mkakati wa uvunaji wa mifugo kama mkakati wa kumaliza migogoro ya wafugaji na wakulima pamoja na kuondokana na tatizo la uhaba wa malighafi katika viwanda vya kuchakata nyama mkoani humo.


Naibu Waziri Ulega amesema hayo (12.07.2021) alipokutana na uongozi wa mkoa huo ukiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe. Abubakar Kunenge, wakati akitoa taarifa ya ziara yake ya kikazi ya siku mbili Mkoani Pwani na kufafanua kuwa ni vyema uongozi huo ukafanya tathmini ya kina kwa kuunda kamati maalum ili kutafuta suluhu ya migogoro ya ardhi baina ya wakulima na wafugaji mkoani humo.


Amesema viongozi ndani ya mikoa yote nchini ni vyema wakaunda kamati maalum za wataalamu kwenda wilayani hadi vijijini ili kutafuta ufumbuzi wa haraka na kudumu wa kumaliza migogoro ya wakulima na wafugaji, ukiwemo mkakati wa kuhakikisha wafugaji wanavuna mifugo yao kwa kuuza katika viwanda vya kuchakata nyama ili vipate malighafi na kuuza nyama ndani na nje ya nchi.


Mhe. Ulega amesema serikali inalichukulia suala hilo kwa uzito mkubwa kwa kutumia kamati maalum kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wizara ya Maji, Wizara ya Kilimo na Wizara ya Mifugo na Uvuvi.


Amesema wizara ilishatuma timu ya kushughulikia jambo hilo kwa ngazi ya taifa na imetoka na mapendekezo kadhaa kwa hatua zaidi.


Mhe. Ulega amesema Wizara ya Mifugo na Uvuvi inasisitiza mikoa kuunda kamati ya wataalam kubaini mambo kadhaa ili kuchukua hatua ili jambo hilo lisijitokeze katika maeneo mbalimbali nchini.


"Timu hizo zitabaini maeneo ya mifugo vamizi, wafugaji wakorofi ili waweze kuchukuliwa hatua kali sambamba na kubainisha mahitaji halisi ya miundombinu ya mifugo, kuwepo kwa taarifa kamili za mifugo ilipo pamoja na kuhamasisha kuwa na utamaduni wa kuuza mifugo kwenye viwanda vya kuchakata nyama ili vipate malighafi." amesema Mhe. Ulega.


Akizungumzia hali halisi ya hatua zilizochukuliwa na Mkoa wa Pwani kukabiliana na kero hiyo mkuu wa mkoa huo Mhe. Abubakar Kunenge amewataka wakazi wa Mkoa wa Pwani kutochukua sheria mkononi na kuviasa vyombo vya ulinzi na usalama kutenda haki wanapopata taarifa ya migogoro hiyo.


Mhe. Kunenge amefafanua kuwa mkoa huo tayari umeanza kufanya sensa ya mifugo katika wilaya zote na Wilaya ya Rufiji kwa sasa ipo hatua za mwisho kukabidhi mapendekezo yao.


Ameongeza kuwa taarifa hiyo ya sensa wamebaini kuna wafugaji wengi waliopo katika wilaya hiyo hawajasajiliwa na hawana taarifa zozote za wanakotoka wala wanakokwenda.


Katika hatua nyingine Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega akiwa katika Taasisi ya Chanjo Tanzania (TVI) iliyopo Wilaya ya Kibaha, Mkoani Pwani ameagiza uongozi huo pamoja na wizara wanaohusika na masuala ya chanjo kuhakikisha chanjo zinazozalishwa na taasisi hiyo zinawafikia wafugaji waliopo vijijini badala ya kuanza kufikiria kusambaza chanjo hizo nje ya nchi.


Mhe. Ulega amesema kuna mifugo mingi kama kuku, ng'ombe na mbuzi wanaokufa kwa kuwa wafugaji hawajui kama kuna chanjo zinazozalishwa hapa nchini ingawa kuna maeneo mengine chanjo hizo hazijafika kabisa.


Ametaka viongozi hao kuhakikisha chanjo zinafika maeneo mbalimbali nchini hususan maeneo ya vijijini ili wafugaji waweze kukinga mifugo yao dhidi ya magonjwa mbalimbali.


Mhe. Ulega ametembelea pia kiwanda cha kuzalisha chanjo za mifugo cha HESTER kilichopo Wilayani Kibaha na kujionea namna kiwanda hicho kikiwa tayari kuanza kuzalisha chanjo ambazo zitakuwa zikiuzwa ndani na nje ya nchi.


Akiwa kiwandani hapo ameendelea kusisitiza chanjo za mifugo kufikishwa maeneo mbalimbali nchini hususan ya vijijini ili mifugo iwe na afya bora na wafugaji waweze kunufaika kupitia ufugaji.


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (Mb) akizungumza mara baada ya kufika katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani kwa ajili ya kuanza rasmi ziara ya kikazi ya siku mbili mkoani humo ambapo ameusisitiza uongozi wa mkoa huo kuwa na mkakati wa kumaliza migororo ya wakulima na wafugaji ikiwemo njia ya kuhamasisha wafugaji kuvuna mifugo yao na kuuza viwandani ili viwanda hivyo vipate malighafi kwa ajili ya kuuza nyama ndani na nje ya nchi. (12.07.2021)


Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe. Abubakar Kunenge akibainisha mikakati ya mkoa katika kumaliza migogoro ya wakulima na wafugaji wakati Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega alipofika ofisini kwake kabla ya kuanza rasmi ziara ya kikazi ya siku mbili mkoani humo, ambapo Mhe. Kunenge amewataka wakazi wa mkoa huo kutochukua sheria mkononi na kuvielekeza vyombo vya ulinzi na usalama kutenda haki vinapopata taarifa juu ya migogoro hiyo. (12.07.2021)


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (Mb) akiangalia moja ya mitambo katika kiwanda cha kuzalisha chanjo za mifugo cha HESTER kilichopo Wilaya ya Kibaha Mkoani Pwani na kusisitiza chanjo zinazozalishwa nchini zinapaswa kufikishwa maeneo ya vijijini ili wafugaji wakinge mifugo yao dhidi ya magonjwa mbalimbali. (12.07.2021)


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega, (wa tatu kutoka kushoto) akioneshwa na Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) Dkt. Stella Bitanyi moja ya mitambo inayotumiwa na Taasisi ya Chanjo Tanzania (TVI) iliyopo Wilaya ya Kibaha, Mkoani Pwani. Wa kwanza kulia ni Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Hezron Nonga. (12.07.2021)


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (Mb) akioneshwa na Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) Dkt. Stella Bitanyi, sehemu ya eneo la Taasisi ya Chanjo Tanzania (TVI) iliyopo Wilaya ya Kibaha, Mkoani Pwani ambalo limevamiwa na baadhi ya wananchi na kujenga makazi. (12.07.2021)