NARCO YAELEKEZWA KUIPATIA KITALU KAMPUNI YA CHOBO
Waziri wa Mifugo na Uvuvi,
Mashimba Ndaki ameielekeza Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) kuipatia Kampuni
ya Chobo Kitalu Mbadala katika eneo la Mradi wa Mwisa II lililopo Wilayani
Muleba, Mkoani Kagera baada ya kuchelewa kuendeleza Kitalu cha awali alichopewa
katika Ranchi ya Mabale na kupelekea wawekezaji wengine kutumia eneo hilo.
Ndaki alitoa agizo hilo
alipokutana na mwekezaji huyo jijini Dodoma Julai 27, 2021 na kukubaliana kuwa
Wizara itampatia eneo lingine katika mradi wa Mwisa II ili aweze kuendeleza
uwekezaji katika sekta ya mifugo.
Kufuatia makubaliano hayo,
Waziri Ndaki ameielekeza NARCO kushughulikia jambo hilo kwa haraka ili
mwekezaji huyo aweze kuendelea na shughuli zake za uwekezaji nchini.
“Kama nilivyosema sisi tuko
tayari kushirikiana na Chobo pamoja na wawekezaji wengine kwa lengo la kuongeza
tija kwenye sekta ya mifugo ili kutimiza malengo ya Tanzania ya Viwanda,”
alisema Ndaki
Naye, Mkurugenzi wa Kampuni
ya Chobo, John Chobo pamoja na kumshukuru Waziri kwa hatua hiyo, alisema kuwa
uamuzi huo utasaidia kiwanda chake kupata malighafi iliyobora kutoka kwa mifugo
watakayoiwekeza katika eneo hilo na anaamini kwa ushirikiano wanaopata kutoka
kwa NARCO na Wizara wataweza kuzalisha bidhaa bora itakayoweza kushindana
katika Soko la Kimataifa.
Aliongeza kuwa kiwanda chake
cha kuchakata nyama ni kikubwa na kina uwezo wa kuchinja ng’ombe 600 na mbuzi
1500 kwa masaa nane, hivyo kupitia uwekezaji huo kampuni yake itaweza
kutengeneza mnyororo wa thamani utakaoweza kufaidisha maelfu ya Watanzania.
Julai 9, 2021 Waziri Ndaki
alipokuwa katika ziara Mkoani Kagera alimtaka mwekezaji huyo kukubali kuachia
Kitalu cha Mabale ili kuepusha mgogoro uliopo baina yake na wawekezaji wengine
ambao wanatumia eneo hilo alilokabidhiwa awali na kumuahidi kuwa pindi atakapokuwa
tayari kuwekeza Wizara itampatia eneo lingine ambalo litakuwa zuri zaidi kwa
uwekezaji wake.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki (kulia) akifurahia jambo na Mkurugenzi wa Kampuni ya Chobo, John Chobo (kulia) wakati akiagana nae baada ya kumaliza kikao chao kilichofanyika jijini Dodoma Julai 27, 2021. Katikati ni Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki (kulia) akiongea na Mkurugenzi wa Kampuni ya Chobo, John Chobo (kushoto) muda mfupi baada ya kumaliza kikao chake kilichoshirikisha Mkurugenzi huyo wa Kampuni ya Chobo, Viongozi wa Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) na wadau wengine kilichofanyika jijini Dodoma Julai 27, 2021. Katika kikao hicho Waziri Ndaki aliielekeza Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) kuipatia Kampuni hiyo Kitalu katika eneo la Mradi wa Mwisa II lililopo Wilayani Muleba, Mkoani Kagera ili iweze kuendeleza shughuli za uwekezaji katika sekta ya mifugo kwa lengo la kuiwezesha nchi kufikia uchumi wa Viwanda.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni