Ziara ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Mashauri Ndaki mkoani Kagera imekuwa dawa ya utatuzi wa migogoro ya ardhi kati ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi.
Waziri Ndaki amefanya ziara ya siku nne mkoani Kagera kwa
lengo la kutatua migogoro ya ardhi iliyokuwepo katika maeneo yanayomilikiwa na
Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) katika Ranchi za Mabale wilayani Misenyi,
Kagoma na Mwesa wilayani Muleba mkoani Kagera.
Akizungumza na uongozi wa mkoa wa Kagera ambapo pia alikuwepo
Katibu Mkuu anayesimamia sekta ya mifugo baada ya kumaliza ziara yake, Waziri
Ndaki alisema kuwa ziara hiyo imekuwa muhimu na yenye mafanikio makubwa kwake
na kwa sekta ya mifugo kwani uwepo wa migogoro husababisha kupungua kwa kasi ya
ukuaji wa sekta ya mifugo.
Katika ranchi hizo kulikuwa na wananchi ambao walikuwa
wanakaa kwa muda mrefu na kufanya shughuli zao za maendeleo katika maeneo hayo.
Hivyo kutokana na hilo kulikuwepo na migogoro kati ya wananchi hao na wawekezaji
waliopewa vitalu kwa ajili kufugia mifugo.
Baada ya malalamiko hayo ya muda mrefu kati ya wananchi na
wawekezaji, Waziri Ndaki aliwaeleza wananchi hao kuwa Mhe. Rais Samia Hassan
ameridhia wabaki katika maeneo hayo na kuendelea kufanya shughuli zao za
maendeleo. Pia aliwaeleza wananchi na wawekezaji kuwa serikali itayapima upya
maeneo hayo na kuweka alama za mipaka ili migogoro hii isijirudie.
Vilevile wananchi katika maeneo hayo walielezwa kuwa upimaji
na mipaka ikishawekwa lazima kila mmoja aifuate na kuiheshimu. Pia kwa wale
ambao wamejitenga mmoja mmoja wanatakiwa kuanza kuhama na kutafuta maeneo
kwenye vijiji.
Waziri Ndaki pia aliwaeleza wawekezaji kuwa upimaji huu
utakaofanyika katika maeneo ya ranchi hauta waathiri katika shughuli zao za
ufugaji. Serikali inawahitaji wawekezaji katika kuhakikisha sekta ya Mifugo
inakua. Lakini pia amewasisitiza wawekezaji kuwa vitalu watakavyopewa ni lazima
wahakikishe wanavitumia kwa malengo yaliyokusudiwa kwa kuhakikisha wanafuga
mifugo bora.
Katika ranchi ya Mwisa II ambayo nayo ilikuwa na mgogoro
mkubwa Waziri Ndaki alisema tayari wizara imeshaweka makubaliano na uongozi wa
Mkoa wa Kagera pamoja na Wilaya ya Muleba ili kuhakikisha utatuzi wa mgogoro
uliopo pale unatatuliwa.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Meja Jenarali Charles Mbuge amesema
kuwa ulinzi na usalama ni kipaumbele namba moja kwenye mkoa hivyo uwepo wa
migogoro husababisha uvunjifu wa amani. Hivyo utatuzi wa migogoro uliofanyika
utasaidia sana maeneo hayo kuwa na amani na kuwafanya wananchi na wawekezaji
kuendeleza shughuli zao za maendeleo. Kwa upande wake ameahidi kuwa atasimamia
utekelezaji wa makubaliano yote yaliyofikiwa katika utatuzi wa migogoro hiyo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Mbunge wa Muleba Kaskazini,
Mhe. Charles Mwijage na Mbunge wa Muleba Kusini, Mhe. Oscar Kikoyo walisema
kuwa migogoro hiyo imechukua muda mrefu kutatuliwa lakini wamemshukuru Mhe.
Rais Samia Hassan kwa kuridhia wananchi hao kubaki katika maeneo hayo
yanayomilikiwa NARCO. Vilevile wamemshukuru Waziri Ndaki na viongozi na
wataalam katika Wizara Mifugo kwa jitihada waliochukua ili kuhakikisha wanamaliza
migogoro hiyo.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayesimamia
sekta ya mifugo, Prof. Elisante Ole Gabriel alisema kuwa lengo la wizara ni
kuhakikisha sekta ya mifugo inakua na inaongeza kipato kwa wafugaji na taifa
kwa ujumla. Pia alisema kwa upande wa wizara atahakikisha makubaliano yote
yaliyofikiwa yanakwenda kutekelezwa.
Utatuzi wa wa migogoro hiyo katika Mkoa wa Kagera umeleta
faraja kubwa kwa wananchi ambao walikuwa wanakaa katika maeneo ya ranchi za
Taifa. Lakini pia kwa wawekezaji waliopatiwa vitalu kwani baada ya utatuzi huo
sasa pande zote mbili watafanya shughuli zao za kiuchumi kwa amani.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (Mb) akizungumza na viongozi na wataalam kutoka wizarani upande wa sekta ya Mifugo, sekretarieti ya mkoa wa Kagera, Wilaya ya Muleba na Wabunge wa Muleba baada ya kumaliza ziara yake ya siku nne mkoani Kagera kwa lengo la kutatua migogoro iliyokuwepo kwenye maeneo yanayomilikiwa na Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO). Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Meja Jenarali Charles Mbuge na kulia ni Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Elisante Ole Gabriel. (13.07.2021)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni