Nav bar

Jumamosi, 24 Julai 2021

NDAKI ATOA SOMO KWA VIONGOZI, WATENDAJI WA WIZARA YAKE.

·   Ulega asisitiza sheria ya mabondo na sera ya kopa mbuzi lipa mbuzi 


Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki amewataka viongozi  wa Wizara hiyo kufanya kazi bila woga na kuwatengenezea mazingira rafiki ya utendaji kazi watumishi walio chini yao.


Ndaki ameyasema hayo leo (19.07.2021) kwenye Ofisi za Wizara hiyo zilizopo mji wa Magufuli eneo la Mtumba jijini Dodoma wakati wa kikao baina yake na viongozi wa idara, vitengo na wakuu wa taasisi zote zilizopo chini ya wizara hiyo ambapo amewasisitiza kudumisha ushirikiano baina yao na watumishi waliopo chini yao.


“Niwaombe viongozi wote mliopo hapa, ondoeni hofu wakati wote wa utendaji kazi wenu kwa sababu mimi sipo upande wa mtu yoyote hapa hata nikikupa kazi ifanye bila kuhofia labda naweza kuwa nimekupa kama kipimo flani” Amesema Ndaki.


Aidha Ndaki amewataka viongozi hao kutowalinganisha watumishi waliopo chini yao wakati wa utekelezaji wa majukumu mbalimbali kwa kuwa   uwezo wa mtumishi mmoja hauwezi kufanana na uwezo wa mtumishi mwingine hata kama watakuwa kwenye kada moja.


“Hata wewe leo ungekuwa Waziri ungefanya kwa staili yako na usingefanana na mimi  au Mhe. Ulega hivyo acheni kuwalinganisha watumishi wenu na kumuona mmoja anafaa kuliko wengine na badala yake tafuta mbinu ya kumjengea uwezo ambayo itamfanya afanye kazi vile  inavyotakiwa” Amesisitiza Ndaki.


Akigusia kuhusu matumizi ya lugha sahihi wakati wa kukosoana kwenye mazingira ya kazi, Ndaki amewataka viongozi hao kutumia lugha nzuri wakati wa kuwaelekeza watumishi walio chini yao juu ya namna wanavyopaswa kutekeleza majukumu yao badala ya kutumia lugha za kashfa na dharau.


 “Unakuta kiongozi  anasema kabisa, yule huwa hawezi kufanya hizi kazi tena muda mwingine ukute mtumishi husika ndo ameajiriwa kufanya kazi hiyo, nawahakikishia viongozi mliopo hapa tukifanya hivyo hatutafika na utendaji kazi lazima utakuwa chini” Amesema Ndaki.


Ndaki amewataka viongozi na watendaji hao kuepuka kuwatengenezea hofu watumishi waliopo chini yao ambapo amewashauri kutumia njia ya utoaji huduma bora kwa watumishi hao ili kujipatia heshima wanayostahili.


“ Mimi ninaamini siwezi kuheshimika kwa kuogopwa eti kwa sababu ni Waziri, heshima yangu itatokana na huduma nayotoa kwenu mliopo chini yangu na ninatambua heshima inayotokana na woga inaweza kunikosesha mambo mengi sana kutoka huko chini”


Kwa upande wake Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amewapongeza viongozi hao kwa kazi kubwa wanayoifanya ambapo amewataka kuongeza nguvu zaidi ili kuendelea kutoa huduma stahiki kwa wananchi.


“Kwa mfano hili suala la kopa mbuzi lipa mbuzi, watu wengi wanalisubiri kwa hamu sana hivyo ninatoa rai kwenu mhakikishe mchakato wa kulifanikisha hili unakamilika mapema na wananchi waanze kunufaika na shughuli hiyo” Amesema Ulega.


Akigusia upande wa sekta ya Uvuvi, mbali na kuwapongeza viongozi hao kwa kazi nzuri ya kusimamia uendeshaji wa viwanda vya kuchakata samaki, Ulega amewataka watendaji wa sekta hiyo kusimamia sheria kuhusu suala la uchakataji wa mabondo ambayo yameonekana kuchakatwa na wananchi katika maeneo mbalimbali badala ya viwandani kama sheria inavyoelekeza.


“Lakini pia sasa hivi ni lazima tudhibiti huu mfumo wa kuuza samaki mzima kabla ya kumchakata kwa sababu kwa mtazamo wangu naona unatukosesha mapato mengi sana ambayo yangepatikana kutokana na mauzo ya mazao mbalimbali yanayotokana na samaki huyo” Amesisitiza Ulega.


Wakitoa neno la shukrani  kutokana na kikao hicho, Makatibu wakuu wa Wizara hiyo Prof. Elisante Ole Gabriel (Mifugo) na Dkt. Rashid Tamatamah (Uvuvi) wameahidi kutekeleza maelekezo yote yaliyotolewa na viongozi hao kwenye kikao hicho huku pia wakiwashukuru mawaziri hao kutokana na ushirikiano wanaowaonesha wakati wa utekelezaji wa majukumu yao.


Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki (kushoto) akisisitiza kuhusu ushirikiano kati ya viongozi na watumishi waliopo chini yao wakati wa kikao baina yake na Viongozi na watendaji wa idara, vitengo na taasisi zilizopo chini ya wizara yake kilichofanyika leo (19.07.2021) makao makuu ya Wizara hiyo yaliyopo mji wa Magufuli eneo la Mtumba jijini Dodoma, Kulia ni Naibu Waziri wa Wizara hiyo Abdallah Ulega.


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega (kulia) akimuonesha Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki mfano wa  namna Serikali inavyopata hasara kutokana na mauzo ya samaki mzima kabla hajachakatwa wakati wa kikao baina yao na Viongozi na watendaji wa idara, vitengo na taasisi zilizopo chini ya wizara ya Mifugo na Uvuvi kilichofanyika leo (19.07.2021) makao makuu ya Wizara hiyo yaliyopo mji wa Magufuli eneo la Mtumba jijini Dodoma.

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt.Rashid Tamatamah akifafanua namna sekta yake inavyosimamia utekelezaji wa majukumu yake wa kikao baina ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki, Naibu Waziri wa Wizara hiyo Abdallah Ulega na Viongozi, watendaji wa idara, vitengo na taasisi zilizopo chini ya wizara hiyo kilichofanyika leo (19.07.2021) makao makuu ya Wizara hiyo yaliyopo mji wa Magufuli eneo la Mtumba jijini Dodoma.


Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof.Elisante Ole Gabriel akieleza namna alivyoguswa na ujumbe uliotolewa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki wakati wa kikao baina ya Waziri huyo, Naibu Waziri wa Wizara hiyo Abdallah Ulega na Viongozi, watendaji wa idara, vitengo na taasisi zilizopo chini ya wizara hiyo kilichofanyika leo (19.07.2021) makao makuu ya Wizara hiyo yaliyopo mji wa Magufuli eneo la Mtumba jijini Dodoma.


Sehemu ya Viongozi watendaji wa idara, vitengo na taasisi zilizopo chini ya wizara ya Mifugo na Uvuvi wakimsikiliza Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki (hayupo pichani) wakati wa kikao baina yake na Viongozi, watendaji wa idara, vitengo na taasisi zilizopo chini ya Wizara hiyo kilichofanyika leo (19.07.2021) makao makuu ya Wizara hiyo yaliyopo mji wa Magufuli eneo la Mtumba jijini Dodoma.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni