Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki leo (15.07.2021) amekataa nyongeza ya ruzuku kwenye shughuli za uvuvi ambapo amesema kuwa hatua hiyo itawawekea mazingira magumu wavuvi waliopo hapa nchini kutokana na kutokuwa na miundombinu ya kisasa ya kufanya shughuli hizo hasa katika eneo la bahari kuu ikilinganishwa na makampuni yanayotoka nje ya nchi.
Ndaki ameyasema hayo alipokuwa akiwasilisha taarifa ya wizara yake kwenye mkutano wa kamati ya majadiliano ya biashara (TNC) ngazi ya mawaziri ambao ulikuwa ukijadili mkataba wa kuondoa ruzuku katika shughuli za uvuvi ambapo amesema kuwa kwa hivi sasa Tanzania bado haijapiga hatua kubwa kwenye uvuvi wa bahari kuu hivyo ongezeko hilo la ruzuku litatoa fursa nzuri zaidi kwa makampuni ya uvuvi ya yaliyopo kwenye nchi zilizoendelea.
“Kwanza sisi bado hatujaanza kutoa ruzuku kwa wavuvi wetu lakini pia makampuni haya kutoka nje yakipata ruzuku hiyo yatakwenda kuvua mahali popote kwenye samaki na kwa kuwa wao wana nyenzo za kisasa watafanya hadi uvuvi unaopitiliza “overfishing” jambo ambalo litawakosesha samaki wavuvi wetu” Amesema Ndaki.
Ndaki ameongeza kuwa kwa hivi sasa nchi inahitaji nafasi ya kutosha ya kuwawezesha wavuvi waliopo hapa nchini mazingira mazuri yatakayowasaidia kufanya shughuli zao kwa ufanisi hasa kwenye ukanda wa bahari kuu.
“Tunahitaji kuweka mazingira madhubuti na kujidhatiti kisera na sasa tupo kwenye mchakato wa ununuzi wa meli za uvuvi ambazo kwa kiasi kikubwa zitaweza kutusaidia kutekeleza shughuli za uvuvi kwenye ukanda wa bahari kuu” Amesisitiza Ndaki.
Jumla ya Mawaziri na watendaji wa nchi wanachama 164 wa kamati ya majadiliano ya biashara (TNC) wameshiriki mkutano huo ambao ulifanyika kwa njia ya mtandao na kuratibiwa na Shirika la biashara duniani (WTO) kutoka nchini Uswisi.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki akifuatilia mkutano wa kamati ya majadiliano ya biashara (TNC) uliofanyika kwa njia ya mtandao leo (15.07.2021) na kujumuisha viongozi wa sekta za Mifugo na Uvuvi, Viwanda na biashara kutoka nchi 164, balozi wa Tanzania nchini Uswisi na watendaji wa sekta hizo kutoka kwenye mataifa shiriki ya mkutano huo, lengo la mkutano huo lilikuwa ni kujadili Mkataba wa kuondoa ruzuku kwenye shughuli za uvuvi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni