Na. Edward Kondela
Serikali imemtaka mkandarasi anayejenga
bwawa la Kijiji cha Chamakweza kilichopo Wilaya ya Chalinze Mkoani Pwani,
kukamilisha bwawa hilo kwa wakati pamoja na kuzingatia ubora ili liweze kuwa na
tija kwa jamii ya wafugaji.
Akizungumza (16.04.2021) mara baada ya
kufanya ziara ya kikazi ya siku moja kujionea ujenzi wa bwawa hilo, Katibu Mkuu
Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel
amesema endapo kukitokea dosari yoyote katika bwawa hilo wakati wa kipindi cha
mwakwa mmoja wa uangalizi mkandarasi atapaswa kugharamia hasara zote pamoja na
kuchukuliwa hatua za kisheria.
“Tungetamani hili jambo lifike ukomo
ili tupokee huu mradi, na umalize haraka kwa wakati na kingine ubora kwa kuwa
usipofanya hivyo kile kipindi cha uangalizi cha mwaka mmoja kama kuna kilichoharibika
kwanza utalipa fidia, nitakutoza na riba ya kuharibu.” Amesema Prof. Gabriel
Ameongeza kuwa bwawa hilo ambalo lipo
katika Jimbo la Chalinze ambapo anaisha Rais mstaafu wa awamu ya nne Mhe. Dkt.
Jakaya Mrisho Kikwete linajengwa kwa heshima kubwa kwa kuwa rais mstaafu
amekuwa na mapenzi makubwa na wafugaji hivyo ni vyema kuenzi mchango wake
katika uongozi wa nchi hii na kuwataka viongozi wa Kijiji cha Chamakweza
kujenga utaratibu wa kuthamini mchango wa viongozi na kuwashukuru wakati bado
wakiwa hai.
Kwa upande wake mkandarasi anayejenga
bwawa la Chamakweza Bw. Peter Kasera kutoka Kampuni ya Westmont Tanzania
Limited, amesema ujenzi wa bwawa hilo ambao unagharimu Shilingi Milioni 670
umefikia zaidi ya asilimia 90 na kwamba kazi wanayoendelea nayo ni kuweka mawe,
kumalizia kuta na upande wa uzio tayari vifaa vyote vimekamilika kwa ajili ya
ujenzi.
Amebainisha kuwa mradi huo umeshindwa
kukamilika kwa wakati kutokana na changamoto za kifedha, mvua na mambo ya
kitaifa hivyo kuhitaji muda kidogo ili kukamlisha sehemu ya kazi iliyobaki
kabla ya kuukabidhi mradi huo.
Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha
Chamakweza Bw. Mika Ole Kashimba ametaka kufanyika kwa baadhi ya maboresho
katika ujenzi wa bwawa hilo hususan kwa kuliongezea kina ili liweze kukusanya
maji mengi ambayo yataweza kukaa kwa muda mrefu.
Ameongeza kuwa kuna nyakatia kuta za bwawa zimekuwa zikivunjika kutokana na wingi wa maji yanayoingia kwenye bwawa hali inayolifanya bwawa kushindwa kuhimili kutunza kiasi cha maji kinachoingia.
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel akifafanua jambo kwa mmoja wa wafugaji katika Kijiji cha Chamakweza kilichopo Wilaya ya Chalinze Mkoani Pwani, alipotembelea ujenzi wa bwawa la kijiji hicho kwa ajili ya matumizi ya mifugo na shughuli nyingine za kibinadamu. (16.04.2021)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni