Wizara ya Mifugo na Uvuvi leo imewasilisha taarifa zake za utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo kwa mwaka wa fedha uliopo (2020/2021) na mikakati iliyojiwekea katika utekelezaji wa miradi kwa mwaka ujao wa fedha (2021/2022) mbele ya kamati ya kudumu ya bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kwenye moja ya kumbi za bunge jijini Dodoma.
Sekta ya Mifugo ndio ilikuwa ya kwanza
kuwasilisha taarifa yake ambapo Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof.
Elisante Ole Gabriel alibainisha kuwa sekta yake iliidhinishiwa kiasi cha
Shilingi bilioni 5 kwa mwaka wa fedha wa fedha uliopo likiwa ni ongezeko la
takribani asilimia 60 ukilinganisha na mwaka wa fedha uliopita (2019/2020)
ambapo sekta hiyo ilitengewa kiasi cha shilingi 3.
“Mhe. Mwenyekiti fedha hiyo ndo
tumeitumia kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwa ni pamoja na ujenzi
wa majosho 20 yaliyojengwa katika Halmashauri mbalimbali za wilaya, kujenga
kliniki na maabara 10 za mifugo ambazo zitagharimu shilingi milioni 700 na
tayari mchakato wa kuhamisha fedha umeshaanza” Amesema Prof. Ole Gabriel.
Prof. Ole Gabriel ameieleza kamati kuwa
uwepo wa kliniki na maabara za mifugo utawasaidia wafugaji kupata huduma bora
za afya ya mifugo kwenye maeneo yao na kuondokana na hali iliyopo hivi sasa
ambapo wafugaji wanalazimika kusafiri umbali mrefu kupata huduma hiyo huku pia
akielezea namna Sekta hiyo ilivyofanikiwa kujenga mabwawa ya kisasa ya
kunyweshea mifugo ya Kimokouwa lililopo wilayani Longido, Narakauo lililopo
wilayani Simanjiro na Chamakweza lililopo wilayani Chalinze. .
“Lakini pia Mhe. Mwenyekiti tunaendelea
na Ujenzi wa Kiwanda cha kuzalisha chanjo pale Kibaha ambacho mpaka sasa ujenzi
wake umefikia asilimia 90 na fedha iliyotumika ni shilingi milioni 213 kati ya
shilingi milioni 600 zilizotengwa na tayari vifaa vya maabara vimeshanunuliwa”
Ameongeza Prof. Ole Gabriel.
Nao baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo
walipata fursa ya kuchangia mambo mbalimbali yaliyopo kwenye taarifa hiyo
ambapo Mbunge wa Viti Maalum (Manyara) Mhe. Yustina Rahhi aliishauri sekta hiyo
kuongeza wigo wa upatikanaji wa maafisa ugani hasa kwenye mamlaka za Serikali
za Mitaa ambako ndipo wanapopatikana wafugaji wengi ushauri ambao Prof. Ole
Gabriel aliupokea na kuahidi kuendelea kushirikiana na Ofisi ya Rais-Tawala za
Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) ili kukabiliana na changamoto hiyo.
Kwa upande wa taarifa ya sekta ya uvuvi
iliyowasilishwa mbele ya kamati hiyo, Jumla ya shilingi bilioni 13 zilitengwa
ambazo zinajumuisha shilingi bilioni 6 zinazotokana na fedha za ndani na
shilingi bilioni 7 zinazotokana na fedha za nje.
Akiwasilisha taarifa hiyo Mkurugenzi wa
Sera na Mipango (Uvuvi) Dkt. Andrew Komba amesema kuwa sekta hiyo mpaka sasa
imetekeleza miradi mbalimbali ikiwa ni pamoja na Ujenzi na ukarabati wa mialo
13 ya kisasa ya kupokelea samaki,
kuboresha masoko matatu ya samaki na
vituo vitano vya ukuzaji viumbe maji.
“Mhe. Mwenyekiti, Ujenzi wa bandari ya
Uvuvi upo katika hatua za awali za upembuzi yakinifu lakini pia baada ya
Serikali kuamua kutobinafsisha shirika la TAFICO tayari Serikali imeshaanza
ukarabati wa miundombinu ya Shirika hilo” Amesema Dkt. Komba.
Aidha Dkt. Komba ameiambia kamati kuwa
Sekta yake ilipokea fedha za mradi wa
Usimamizi Shirikishi wa Uvuvi kusini mwa bahari ya Hindi (Swiofish) ambapo
fedha zilizotengwa kwa ajili ya kutekeleza mradi huo (bilioni 6) zimetekeleza
mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na ujenzi wa nyumba 3 za wafanyakazi mkoani
Tanga na ujenzi wa maabara ya kisasa ya Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi nchini
(TAFIRI) iliyopo Kunduchi jijini Dar-es-salaam.
“Mhe. Mwenyekiti, hata hivyo kutokana
na changamoto ya kutokuwepo kwa vituo vya kutosha vya ukuzaji viumbe maji,
tumeanza mchakato wa ujenzi wa kituo kikubwa cha Ukuzaji viumbe maji pale
Kunduchi ambapo jumla ya shilingi bilioni 1.6 zimetengwa kwa ajili ya kazi hiyo
na kwa sasa ipo kwenye hatua ya upembuzi yakinifu na tayari Wakala wa Majengo
nchini (TBA) wameshaanza kazi ya kusanifu miundombinu ya kituo hicho kisha wao ndio watasimamia ujenzi huo”
Amesema Dkt. Komba.
Akihitimisha taarifa zilizowasilishwa
na sekta zote mbili (Mifugo na Uvuvi), Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Pauline
Gekul mbali na kuishukuru kamati hiyo kwa maoni na mchango walioutoa wakati wa
uwasilishwaji, ameahidi kufanyia kazi changamoto zote zilizowasilishwa na
wajumbe wa kamati ambapo aliwaomba kuendelea kutoa ushirikiano wa kutosha
kwenye Wizara yake ili iendelee kuboresha sekta hizo hapa nchini.
“Hivi karibuni Mhe. Waziri aliagiza
wapangaji waliokodisha vitalu afu hawavitumii wanyang’anywe vitalu hivyo ili
wapewe wafugaji wengine wenye mahitaji navyo na huu ndo msimamo wa Wizara kwa
sasa kwa hiyo waheshimiwa wajumbe wa kamati, ninawahakikishia Wizara yetu
itaendelea kuboresha maeneo mbalimbali ambayo awali yalikuwa ni changamoto kwa
wafugaji au wavuvi” Amehitimisha Mhe. Gekul.
Naibu Waziri wa Mifugo na
Uvuvi Mhe. Pauline Gekul akifafanua moja ya hoja zilizowasilishwa na wajumbe wa
kamati ya kudumu ya Kilimo, Mifugo na Maji muda mfupi baada ya kuwasilishwa kwa
taarifa ya Wizara yake kuhusu utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo kwa
mwaka wa huu fedha (2020/2021) leo (09.03.2021) katika moja ya kumbi za bunge
jijini Dodoma.
Katibu Mkuu Wizara ya
Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel akiwasilisha taarifa ya
miradi ya maendeleo iliyotekelezwa na sekta yake kwa mwaka huu wa fedha
(2020/2021) mbele ya kamati ya Kudumu ya bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji leo
(09.03.2021) kwenye moja ya kumbi za bunge jijini Dodoma.
Mkurugenzi wa Sera na
Mipango (Uvuvi) Dkt. Andrew Komba akiwasilisha taarifa ya miradi ya maendeleo
iliyotekelezwa na sekta yake kwa mwaka huu wa fedha (2020/2021) mbele ya kamati
ya Kudumu ya bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji leo (09.03.2021) kwenye moja ya
kumbi za bunge jijini Dodoma.
Baadhi ya Watendaji wa
Sekta ya Uvuvi wakifuatilia michango inayotolewa na wajumbe wa kamati ya kudumu
ya bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji muda mfupi baada ya Sekta za Mifugo na Uvuvi
kuwasilisha taarifa kuhusu utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo kwa
mwaka wa huu fedha (2020/2021) leo (09.03.2021) katika moja ya kumbi za bunge
jijini Dodoma.
Baadhi ya Watendaji wa Sekta ya Mifugo wakifuatilia michango inayotolewa na wajumbe wa kamati ya kudumu ya bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji muda mfupi baada ya Sekta za Mifugo na Uvuvi kuwasilisha taarifa kuhusu utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo kwa mwaka wa huu fedha (2020/2021) leo (09.03.2021) katika moja ya kumbi za bunge jijini Dodoma.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni