Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. John Mongela amesifu juhudi zinazofanywa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi katika kuhakikisha wafugaji wake wanafanya shughuli hiyo kwa tija na kwa kuzingatia dhana ya ukuzaji wa uchumi wao.
Mhe. Mongela ameyasema hayo
leo (12.11.2020) baada ya kupokea timu ya wataalam wa Idara ya Uendelezaji
Malisho na Rasilimali za vyakula vya mifugo (Wizara ya Mifugo na Uvuvi) ambao
wamefika mkoani humo kwa ajili ya kutoa mafunzo ya siku mbili kwa wakaguzi wa
vyakula vya mifugo kuhusu ukaguzi wa maeneo ya malisho na rasilimali za vyakula
vya Mifugo
"Tunajitahidi sana
kukuza tasnia ya ufugaji lakini uwepo mafunzo kama haya unawafanya wafugaji
wetu wasiishie tu kufuga bali wafuge kwa tija na kukuza uchumi wao"
amesema Mhe. Mongela.
Mhe. Mongela ameishauri
Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuendelea na jitihada hizo za kujenga uwezo kwa
wafugaji ili kuwafanya kuwa wafugaji bora wenye uelewa na ujuzi wa ufugaji wa
kisasa badala ya ufugaji wa asili ambao haukuwa na tija kwa mfugaji pamoja na
kuwa na idadi kubwa ya mifugo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa
Idara ya Uendelezaji Malisho na Rasilimali za vyakula vya mifugo Dkt. Asimwe
Rwiguza amesema kuwa wakaguzi hao ni sehemu ya wakaguzi 129 walioteuliwa kutoka
kwenye Halmashauri na Sekretarieti za mikoa hapa nchini ambao baada ya kupatiwa
mafunzo hayo watawawezesha wafugaji waliopo kwenye maeneo yao elimu kuhusu
chakula bora cha mifugo ili waweze kuiboresha na kuongeza tija zaidi kwenye
tasnia hiyo.
"Semina hii ni muhimu
sana hivyo ninaomba tushirikiane na kwa sababu ninafahamu kuwa wote mna ujuzi
hivyo leo tupo hapa kwa ajili ya kuongezeana uwezo wa kuwahudumia vizuri
wafugaji wetu hasa ikizingatiwa kuwa takribani asilimia 70 ya mahitaji ya mfugo
ni chakula" Ameongeza Dkt. Rwiguza
Mafunzo hayo yaliyofunguliwa
na Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza Bw. Emmanuel ni ya awamu ya pili ambapo awamu
ya kwanza ilifanyika mkoani Morogoro na kuhusisha Mikoa ya Dar-es-Salaam,
Pwani, Morogoro, Tanga na Dodoma.
Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza, Ndg. Emanuel Tutuba (katikati waliokaa) akiwa kwenye picha ya pamoja na wakaguzi wa vyakula vya mifugo kutoka mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Singida na Arusha muda mfupi kabla ya wataalam hao kupatiwa mafunzo juu ya ukaguzi wa maeneo ya malisho na rasilimali za vyakula vya Mifugo yaliyofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa. Kulia kwake ni Mkurugenzi wa Idara ya Uendelezaji Maeneo ya Malisho na Rasilimali za Vyakula vya Mifugo (WMUV), Dkt. Asimwe Rwiguza na kushoto kwake ni Katibu Tawala Msaidizi – Sehemu ya Uchumi na Uzalishaji Ndg. Emil Kasagala. (12.11.2020)
Mkurugenzi wa Idara ya
Uendelezaji Maeneo ya Malisho na Rasilimali za Vyakula vya Mifugo, Dkt. Asimwe
Rwiguza (kulia) akimueleza Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. John Mongela (kushoto)
kuhusu Mafunzo ya siku mbiliWakaguzi wa Vyakula vya Mifugo yaliyofanyika katika
ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza. Katikati ni Katibu Tawala wa Mkoa, Ndg.
Emanuel Tutuba. (12.11.2020)
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe.
John Mongela (katikati) akifafanua juu ya namna mkoa huo unavyozipa kipaumbele
sekta za Mifugo na Uvuvi mbele ya timu ya wataalam wa Idara ya Uendelezaji Maeneo
ya Malisho na Rasilimali za Vyakula vya Mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi
waliofika Ofisini kwake kabla ya kuanza mafunzo kwa Wakaguzi wa Vyakula vya
Mifugo kutoka mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Singida na Arusha yaliyofanyika katika
ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza. (12.11.2020)
Sehemu ya Wakaguzi wa Vyakula
vya Mifugo kutoka mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Singida na Arusha wakifuatilia
kwa umakini mafunzo yanayoendelea kuhusu ukaguzi wa maeneo ya malisho na
rasilimali za vyakula vya Mifugo yaliyofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu
wa Mkoa wa Mwanza. Wawezeshaji wa mafunzo hayo ni timu ya wataalam kutoka Idara
ya Uendelezaji Maeneo ya Malisho na Rasilimali za vyakula vya mifugo (Wizara ya
Mifugo na Uvuvi). (12.11.2020)
Mkurugenzi Msaidizi Idara ya
Uendelezaji Maeneo ya Malisho na Rasilimali za Vyakula vya Mifugo (WMUV), Bw.
Roggers Shengoto akiwasilisha mada ya sheria na kanuni za Maeneo ya malisho na
rasilimali za vyakula vya mifugo wakati wa mafunzo kwa wakaguzi wa vyakula vya
mifugo yaliyofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa. (12.11.2020)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni