Serikali imepiga marufuku matumizi ya vyakula vilivyopoteza ubora wa kutumiwa na binadamu na kutumiwa kama vyakula vya mifugo kabla ya kuthibitishwa kwanza na wataalam wa maabara ya mifugo.
Hayo yamesemwa leo na Mkurugenzi wa Idara ya Uendelezaji Maeneo ya Malisho na Rasilimali
za Vyakula vya Mifugo (WMUV), Dkt. Asimwe Rwiguza ikiwa ni sehemu ya
kuhitimisha mafunzo ya siku mbili ya wakaguzi wa vyakula vya mifugo kutoka
mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Singida na yaliyofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza.
"Kumekuwa na mazoea ya
vyakula ambavyo vimeshapoteza ubora wa matumizi ya binadamu kutumika kama
vyakula vya mifugo hivyo ninapenda kutumia fursa hii kutoa wito kwa wafugaji,
wazalishaji na taasisi mbalimbali zinazojihusisha na uzalishaji wa vyakula vya
binadamu kuwa ni marufuku kutumia vyakula hivyo bila Wizara yenye dhamana kuwa
na taarifa na kujiridhisha kitaalam kama chakula hicho kinafaa au la,"
Amesisitiza Dkt. Rwiguza.
Aidha, Dkt. Rwiguza
amebainisha madhara yanayoweza kumpata mtu ambaye atatumia mazao ya mfugo
uliokula vyakula hivyo kuwa ni pamoja na kupatwa na magonjwa mbalimbali kama
vile Kansa.
Kwa upande wake Mkurugenzi
Msaidizi wa Idara ya Uendelezaji Maeneo ya Malisho na Rasilimali za Vyakula vya
Mifugo, Bw. Roggers Shengoto amesema kuwa mafunzo hayo yamekuwa na manufaa
makubwa kwasababu zaidi ya asilimia 90 ya wataalam walioalikwa walishiriki.
"Pia kupitia mafunzo
haya tumegundua kuwa bado kuna haja ya Halmashauri za vijiji kutenga maeneo ya
malisho ya mifugo na pia wazalishaji na wauzaji wa vyakula vya mifugo bado
hawazingatii sheria na kanuni za kufanya shughuli hizo, hivyo tuna imani
wataalam hawa wataenda kuleta mabadiliko katika maeneo yote yenye changamoto
kwa wafugaji" Ameongeza Shengoto.
Nao baadhi ya washiriki wa
mafunzo hayo wamesema kuwa wamenufaika na yote waliyofundishwa ambapo wameahidi
kuyafanyia kazi na kubadilisha utendaji wao pindi wakirejea kwenye vituo vyao
vya kazi.
"Kwa mfano, zamani
nilikuwa naenda kwa mdau kama Mkaguzi na nilikuwa natumia lugha ya mamlaka
lakini kupitia mafunzo haya nimefundishwa kumfuata mdau kama rafiki na
kuzungumza naye kwa lugha ya kawaida" Amesema mmoja wa washiriki Veronica
Ngoso.
Takribani wakaguzi 129 nchi
nzima wanatarajiwa kupatiwa mafunzo hayo ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa
kufuata taratibu, sheria na kanuni.
Mkurugenzi wa Idara ya Uendelezaji
Maeneo ya Malisho na Rasilimali za Vyakula vya Mifugo (WMUV), Dkt. Asimwe
Rwiguza (kulia) akifafanua jambo mbele ya wataalam wa ukaguzi wa malisho na
rasilimali za vyakula vya mifugo muda mfupi baada ya kufika kwenye kiwanda cha
kusindika chakula cha mifugo kinachojulikana kama "Musoma Animal
Feed" kilichopo mkoani Mwanza. (13.11.2020)
Meneja wa Kiwanda cha "Musoma Animal Feed", Bi. Maajabu Musa (mwenye kilemba cheusi) akitoa maelekezo ya namna chakula cha mifugo kinavyotengenezwa kiwandani hapo mbele ya timu ya wataalam kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi na wakaguzi wa vyakula vya mifugo kutoka mikoa ya Mwanza, Arusha, Shinyanga na Arusha wakati walipotembelea kiwanda hicho kilichopo mkoani Mwanza. (13.11.2020)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni