Nav bar

Jumatano, 29 Aprili 2020

TUTAHAKIKISHA WAFUGAJI WOTE WANAFUGA KISASA NA KWA TIJA- DKT. MRUTTU
Kaimu Mkurugenzi wa Utafiti na Mafunzo, Dkt. Hassan Ally Mruttu  amewataka wafugaji mkoani Pwani  kufuga kisasa na kwa tija huku wakichukua tahadhari dhidi ya maambukizi ya virusi vya korona. 

Akiongea wakati wa Mafunzo elekezi na uhamasishaji  kwa ajili ya kupandisha ng'ombe kwa njia ya chupa (uhimilishaji) kwenye kijiji cha Mkwalia kitumbo kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga jana ( 22/04/2020) Dkt. Mruttu amesema lengo la Mafunzo hayo ni kutaka wafugaji kufuga kisasa na kupata Mifugo iliyo bora na mizuri ili kuwezesha wafugaji kufaidika na Mifugo yao.

"Ni jukumu la Wizara  kuhakikisha wafugaji wote nchini wanapata mbegu bora kwa njia ya uhimilishaji ili kupata Mifugo iliyo bora." Alisema Dr. Mrutu.

Aidha ametoa wito kwa wataalam wa Mifugo kuwa tayari wakati wowote kuwasaidia wafugaji pindi wanapotaka kupandikiziwa mbegu bora kwenye Mifugo yao.

Naye Mtafiti wa Mifugo, Bi. Neema Urassa kutoka taasisi ya utafiti wa Mifugo nchini (TALIRI) alielimisha wafugaji juu ya kufuga kibiashara kwa kukubali kuboresha Mifugo yao kwa lengo la kuongeza tija ya uzalishaji ng'ombe. 

Aliongeza kuwa Uzalishaji wa ng'mbe bora na bidhaa zake utachangia katika kukidhi mahitaji ya lishe bora ya kaya na  upatikanaji wa malighafi za viwanda. 

Aidha, alisisitiza kuhusu uongezaji thamani wa bidhaa na mazao ya ng'ombe na kuongeza kuwa utaratibu wa uvunaji ng'ombe kwa wakati utamfanya mfugaji kuona tija na thamani ya Mifugo katika kuchangia uchumi wa kaya na Taifa kwa ujumla.

" ili kukidhi mahitaji ya walaji na kupata soko lenye faida kubwa ni vyema kuzingatia masuala ya usafi unaokidhi viwango vya uzalishaji, usindikaji na ufungashaji wa mazao  na bidhaa zitokanazo na ng'ombe ikiwa ni pamoja na wanyama hai, maziwa, nyama, samli ngozi na samadi" alisema Bi. Urassa.

Kwa upande wake afisa Mifugo kutoka kituo cha Uhimilishaji Arusha NAIC  Bw. Juma Athumani alisema lengo kuu ya kukagua Mifugo ni kujua kama wana mimba, usalama wa vizazi vyao na kuwatenga wasio na mimba kwa ajili ya zoezi la uhimilishaji kwa njia ya chupa.

" Ni muhimu kwa mfugaji kuchagua mbegu anayotaka kwa Mifugo yake ikiwa ni pamoja na mbegu kwa ajili ya ngo'mbe wa nyama tuu na mbegu kwa ajili ya  maziwa na nyama." Amesema Bw. Juma Athumani.

Hata hivyo Mfugaji wa kijiji cha Mkwalia kitumbo wilayani Mkuranga mkoani Pwani Bw. Yakobo Onina aliishukuru Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kuona umuhimu wa kuwaletea elimu ya ufugaji kibiashara na Uhimilishaji wilayani hapo kwani wamehamasika kupandisha Mifugo yao kwa njia ya chupa na kuonyesha utayari wa kutumia njia hiyo na kuendelea kufuga kibiashara.Afisa Mfawidhi kituo cha Uhimilishaji Kanda ya Mashariki, Bw. Anzigari Balaka (katikati) akijibu maswali ya Bi.Imelda Kamunyu kuhusu Uhimilishaji mara baada kupima mimba na kuangalia usalama wa  vizazi vya mifugo kwa ajili ya maandalizi ya kufanya uhimilishaji kwa Mifugo itakayokuwa haina mimba na isiyo na shida ya kizazi kwenye kaya ya  Bw. Yakobo Onina kijiji cha Mkwalia kitumbo wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani. (22/04/2020) Wafugaji wa kijiji cha Mkwalia kitumbo wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani wakimsikiliza kwa makini Kaimu Mkurugenzi wa Utafiti na Mafunzo wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Hassan Ally Mrutu akitoa elimu kwa wafugaji hao juu ya ufugaji bora wenye tija na Uhimilishaji. (22/04/2020) 
Mtafiti wa Mifugo Bi. Neema Urassa (wa kwanza kulia) Mfugaji Bw. Mohammed Soa wataalam wa Mifugo Bw. Michael Mwinama (wa kwanza kushoto) na Juma Mohammed (wa pili kutoka kushoto) wakiongea na kumuelimisha mfugaji uyo namna ya kufuga kibiashara na  uhimilishaji na faida zake  kwenye kijiji cha Kondomwelanzi wilaya ya mkuranga mkoani Pwani. (22/04/2020) 
Wataalam wa Mifugo wakichagua na kuangalia ngo'mbe wanaofaa kwa ajili ya kupandikizwa/ uhimilishaji kwa mmoja wa wafugaji Bw. Toephil Mayega wa kijiji cha Kondomwelanzi, Wilaya ya Mkuranga Mkoani Pwani (22/04.2020) Mtafiti wa Mifugo Bi. Neema Urassa akitoa elimu na kuhamasisha wafugaji kufuga kisasa na kibiashara lengo likiwa ni kuwasaidia wafugaji kupata Mifugo mizuri na iliyo bora ili kuweza kufaidika na Mifugo yao kwenye kijiji cha Kondomwelanzi Wilaya ya Mkuranga Mkoani Pwani (22/04/2020) 
Hakuna maoni:

Chapisha Maoni