Katibu Mkuu
Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel ameitaka hifadhi
ya ranchi za taifa (NARCO) kwa kushirikiana wadau wengine wa sekta ya Mifugo
kuhakikisha Nchi inakuwa na Mifugo ya kutosha na yenye afya kwa ajili ya
kukidhi mahitaji ya bidhaa zitokanazo na mifugo wakati huu wa janga la Ugonjwa
wa homa kali ya mapafu unaosababishwa na virusi vya Corona (Covid 19) na hata
mara baada ya janga hilo kuisha.
Prof. Elisante Ole
Gabriel aliyasema hayo mapema leo (18.04 2020) mchana alipofanya ziara katika
Wilaya ya Muleba mkoani Kagera lengo likiwa ni kukagua utekelezaji marekebisho
ya upimaji wa ramani ya Ranchi ya Mwisa II ili kutenga eneo
lililopendekezwa kuhamishia wananchi waishio ndani ya Ranchi hiyo.
"Wakati huu wa
hili janga la Corona mahitaji ya nyama Afrika na duniani ni makubwa sana na
yanaweza kuongezeka maradufu mara baada ya janga hili kuisha hivyo ni lazima
tujipange ili kuhakikisha tunakuwa kitovu cha usambazaji wa bidhaa zitokanazo
na mifugo duniani na NARCO mnapaswa kujitokeza kifua mbele kuwa hilo mnaliweza
na lipo ndani ya uwezo wenu" Aliongezea Prof. Ole Gabriel.
Alisisitiza katika
kutekeleza hilo NARCO wanapaswa kutafakari vizuri na kuchagua ranchi moja
ya kimkakati kati ya 14 zilizopo hapa nchini ambayo watawekeza kwa dhati ili
waweze kunenepesha ng'ombe wengi watakaosafirishwa nje ya nchi zenye mahitaji
makubwa ya mifugo na bidhaa zake kwa sasa.
"Lakini pia
katika kuelekea kwenye uchumi wa kati unaotegemea viwanda 2025 ni lazima
NARCO iainishe ranchi tano za mfano ambazo wananchi na wadau mbalimbali
watafika kwa ajili ya kujifunza juu ya ufugaji wa kisasa na pia zitumike kama
shule hata kwa wanaokodisha ranchi nyingine ili nao wafike kujifunza namna ya
ufugaji bora utakaolenga kuzalisha mifugo itakayowawezesha kunufaika
kiuchumi" Alisisitiza Prof.Ole Gabriel.
Awali akisoma taarifa
ya utekelezaji wa marekebisho ya upimaji wa ramani ya Ranchi ya Mwisa II,
kiongozi wa timu ya wataalam wanaofanya kazi hiyo Bw. Fikiri Mwasenga alisema
kuwa kazi hiyo inatarajiwa kukamilika ndani ya siku 30 kuanzia hivi sasa na
mpaka sasa tayari timu hiyo imeshakamilisha kumega maeneo ya vitongoji vitatu
ambavyo ni Butera, Bionza na Rwenzige na kazi ya kupima maeneo mawili
yaliyobaki inaendelea ili kuweza kukamilisha maeneo yote matano
yaliyopendekezwa kutengwa.
Kwa upande wake Mkuu
wa Wilaya ya Muleba Mhe. Mhandisi Richard Ruyango aliishukuru Wizara ya Mifugo
na Uvuvi kwa hatua yake ya upimaji wa maeneo hayo ya ranchi ya Mwisa II kwani
hatua hiyo itaondoa na kumaliza kabisa migogoro iliyokuwepo baina ya wakulima
na wafugaji waliopo kwenye maeneo ya ranchi hiyo.
Ranchi ya Mwisa II ni
miongoni mwa ranchi 14 zilizopo chini ya hifadhi ya ranchi za taifa (NARCO)
ambapo ina ukubwa wa hekta 133,000 na inatajwa kuwa ranchi kubwa kuliko zote
hapa nchini.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni