Na. Edward Kondela
Serikali imesema itahakikisha
sekta za mifugo na uvuvi zinawaondoa wananchi katika umasikini, kupata ajira na
nchi iweze kuuza bidhaa bora za mazao ya mifugo na uvuvi ndani na nje ya nchi.
Akizungumza jana (28.12.2020)
katika siku yake ya kwanza ya ziara ya kikazi ya siku mbili Mkoani mwanza,
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki wakati akihitimisha ziara hiyo
kwenye kiwanda cha kuchinja na kuchakata nyama cha Chobo kilichopo Kata ya
Usagara Wilaya ya Misungwi amesema wizara imekuwa ikichukulia kwa uzito mkubwa
suala la viwanda ambalo litaweza kubadilisha fikra za wafugaji na wavuvi.
“Wananchi wetu waondoe
umasikini, wananchi wetu wapate ajira na sisi tuuze bidhaa za mazao haya ya
mifugo na uvuvi yaliyo bora hapa ndani na kule kwa wenzetu nje, sasa mimi
nikikuta hali ya mkwamo kwa kitu ambacho kinatusaidia kuelekea huko napata
shida.” Amesema Mhe. Ndaki
Waziri Ndaki akifuatana na
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Pauline Gekul katika ziara hiyo amefafanua
kuwa haridhishwi na baadhi ya changamoto wanazokutana nazo wawekezaji ambao
wamejikita katika kuyaongezea thamani mazao ya mifugo na uvuvi na kumuagiza
Kaimu Msajili wa Bodi ya Nyama nchini Bw. Iman Sichalwe kumpatia taarifa ya
hali ya viwanda vya nyama nchini ili apate tathmini halisi ya utendaji kazi wa
viwanda hivyo, baada ya Mkurugenzi Mtendaji wa kiwanda cha Chobo, Bw. John
Chobo kubainisha baadhi ya changamoto ambazo Waziri Ndaki amesema wizara
itahakikisha inafuatilia changamoto zinazoihusu wizara hiyo ili kuzipatia
majibu.
Kwa upande wake Mkurugenzi
Mtendaji wa kiwanda hicho Bw. John Chobo amesema kwa sasa kiwanda chake
kimesimamisha uzalishaji na kinatarajia kuanza kurejea katika shughuli zake
Mwezi Januari Mwaka 2021 baada ya ugonjwa wa Covid 19 kuathiri shughuli za
kiwanda hicho ambacho kimekuwa kikisambaza nyama katika nchi za falme za
kiarabu.
Bw. Chobo amesema
kutopatikana kwa taarifa sahihi za mifugo kumekuwa kukichangia kwa kiasi
kikubwa soko la nyama kutoka Tanzania kwenda nje ya nchi kuwekwa katika daraja
la chini kwa kuwa mifugo mingi ambayo inachakatwa viwandani haina taarifa
sahihi juu ya ukuaji wake, magonjwa na chanjo mbalimbali ambazo mfugo huo
umepatiwa.
Akiwa katika Kiwanda cha
kuchakata samaki Nile Perch kilichopo eneo la viwanda katika Kata ya Nyakato
Wilaya ya Nyamagana jijini Mwanza, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba
Ndaki akiambatana na Naibu Waziri Mhe. Pauline Gekul amewataka wawekezaji wa
viwanda vya samaki vilivyopo Mkoani Mwanza kuhakikisha wanatumia usafiri wa
ndege kutoka katika kiwanja cha ndege cha kimataifa cha Mwanza kusafirisha
minofu ya samaki ili kutangaza bidhaa zinazotengezwa hapa Tanzania.
“Tungependa kuona
usafirishaji wa minofu ya samaki unafanyika hapa nchini kwetu, badala ya nchi
jirani kwa kusafirisha kwa malori kwenda nchi za jirani, kuna uwekezekano
kabisa wa kutoa minofu ya samaki kutoka kiwanja cha ndege cha Mwanza kwenda nje
ya nchi badala ya kutumia nchi za jirani.” Amefafanua Mhe. Ndaki
Aidha, amewataka wawekezaji
wa viwanda vya samaki kuangalia namna ya kuongeza bei ya kununulia samaki kwa
wavuvi wanaopeleka samaki katika viwanda hivyo ili wavuvi hao waweze
kubadilisha maisha yao na kunufaika kupitia Sekta ya Uvuvi.
Waziri Ndaki amebainisha hayo
baada ya Meneja Mkuu wa Kiwanda cha kuchakata samaki cha Nile Perch Bw. Rupesh
Mohan kumueleza Waziri Ndaki na Naibu Waziri Gekul kuwa viwanda vya samaki
vimekuwa vikikosa malighafi ya kutosha kutokana na soko la ndani kukua na
wakati mwingine kupata samaki kwa bei ya juu, hali iliyomlazimu Waziri Ndaki
kubainisha kuwa kama bei ya soko la ndani imepanda ni dhahiri wavuvi watauza
samaki katika soko hilo badala ya kupeleka viwandani ambapo wanauza kwa bei
ndogo.
Hivyo amevitaka viwanda vya
kuchakata samaki kuangalia upya bei ya samaki wanayonunua ili wavuvi nao waweze
kunufaika na kuboresha maisha yao na viwanda pia viweze kupata malighafi za
kutosha.
Pia, Waziri Ndaki ametembelea
kiwanda cha kukausha mabondo ya samaki cha Hong Lin International Ltd kilichopo
Wilaya ya Ilemela jijini Mwanza na kufurahishwa na kiwanda hicho kwa kutumia
kiwanja cha ndege cha kimataifa cha Mwanza kusafirisha bidhaa zake kwenda nchi
za nje.
Naye Mkurugenzi wa kiwanda
hicho Bi. Wang Shenghong ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania kwa kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji hali inayomuwezesha kufanya
shughuli zake bila matatizo huku akiomba pia baadhi ya tozo zipunguzwe.
Katika siku ya kwanza ya
ziara yake Mkoani Mwanza, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki akiwa
na Naibu Waziri Mhe. Pauline Gekul wametembelea pia Maabara ya Taifa ya Uvuvi,
Wakala ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi nchini (FETA) na Kituo cha Ulinzi wa Rasilimali
za Uvuvi (FRP).
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (wa kwanza kutoka kushoto), akiwa na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Pauline Gekul (anayemfuata) pamoja na Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Uvuvi Dkt. Rashid Tamatamah (wa kwanza kutoka kulia), wakati Waziri Ndaki alipofanya ziara ya kikazi katika kiwanda cha kukausha mabondo ya samaki cha Hong Lin International Ltd kilichopo Wilaya ya Ilemela, jijini Mwanza. (28.12.2020)
Waziri wa Mifugo na Uvuvi
Mhe. Mashimba Ndaki akiwa na Naibu Waziri wa wizara hiyo Mhe. Pauline Gekul
walipofanya ziara ya kikazi katika kiwanda cha kuchinja na kuchakata nyama cha
Chobo kilichopo Kata ya Usagara Wilaya ya Misungwi Mkoani Mwanza, ambapo Waziri
Ndaki amesema viwanda vya namna hiyo vina nafasi kubwa ya kubadilisha fikra za
wafugaji kufuga kisasa. (28.12.2020)
Waziri wa Mifugo na Uvuvi
Mhe. Mashimba Ndaki na Naibu Waziri wa wizara hiyo Mhe. Pauline Gekul
wakiangalia mabondo ya samaki baada ya kukaushwa tayari kwa ajili ya
kusafirishwa kwenda nje ya nchi, wakati walipofanya ziara ya kikazi katika
kiwanda cha kukausha mabondo ya samaki cha Hong Lin International Ltd kilichopo
Wilaya ya Ilemela, jijini Mwanza. (28.12.2020)
Waziri wa Mifugo na Uvuvi
Mhe. Mashimba Ndaki akiwa na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Pauline Gekul
wakati walipofanya ziara ya kikazi katika Maabara ya Taifa ya Uvuvi iliyopo
Kata ya Nyegezi Wilaya ya Nyamagana Mkoani Mwanza na kushuhudia namna maabara
hiyo inayofanya kazi kwa kufanyia uchunguzi sampuli za samaki kutoka viwandani.
Wa kwanza kushoto ni Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia
Uvuvi Dkt. Rashid Tamatamah. (28.12.2020)
Waziri wa Mifugo na Uvuvi
Mhe. Mashimba Ndaki (wa pili kutoka kushoto), akiwa na Naibu Waziri wa Mifugo
na Uvuvi Mhe. Pauline Gekul (wa pili kutoka kulia) pamoja na Katibu Mkuu Wizara
ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Uvuvi Dkt. Rashid Tamatamah (wa kwanza
kutoka kushoto), wakati Waziri Ndaki alipofanya ziara ya kikazi katika kiwanda
cha kuchakata samaki cha Nile Perch kilichopo kata ya Nyakato, Wilaya ya Nyamagana
jijini Mwanza. (28.12.2020)